NATOA HOJA: Labda na sisi tusubiri hadi itimie miaka 39 Afcon

Muktasari:

  • Wachezaji piganeni mcheze fainali za Afrika, kule mtaonekana kirahisi duniani kuliko kujichimbia Simba, Yanga na Azam.

Uganda, taifa la Afrika Mashariki, taifa lililo Ukanda wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki, Cecafa limetumia miaka 39 kujipanga ili wacheze fainali za Afrika.

Leo hii, Uganda si wenzetu tena. Hivi sasa wako kwenye mji wa Libreville nchini Gabon wakisubiri kuanza mtanange wa kuwania ubingwa wa Mataifa ya Afrika. Uganda wamepangwa Kundi D pamoja na Ghana, Misri na Mali.

Fainali za mwaka huu, zimepangwa kuanza Januari 14 na zitamalizika Februari 5, ambako bingwa wa mwaka huu atapatikana. Ivory Coast ndiye bingwa mtetezi kwa sasa.

Ninakumbuka Peter Tino aliisawazishia Tanzania bao dakika 85 lililoipa Tanzania tiketi ya kucheza fainali za Afrika 1980 Lagos, Nigeria. Tino alifunga bao kwenye Uwanja wa Dag Hammarskjoeld mjini Ndola, ilikuwa furaha kwelikweli sawa na Uganda waliopata bao dakika ya 34 dhidi ya Comoro lililowapa tiketi ya Gabon lililofungwa na Farouk Miya, dogo anayecheza soka klabu ya Standard Liège ya Ubelgiji.

Kufuzu kwa Uganda ilikuwa furaha, magazeti yote, TV, redio na mitandao ya kijamii Uganda, kila mmoja alikuwa akiandika chake ali mradi kuonyesha mafanikio yaliyofikiwa na Uganda Cranes.

Kocha wa Uganda, Milutin ‘Micho’ Sredojevic alihojiwa na gazeti la The Monitor ni nini siri ya mafanikio hayo, akasema siri kubwa ni ushindi hasa mechi za ugenini.

Alisema kikubwa waliweka mkakati kwamba wanahakikisha wanapata matokeo ugenini.

Matokeo ya ugenini huwa ni ziada iwe kwa mechi ya kwanza au ya marudiano, lakini wao walisema lazima washinde ama sare ugenini.

Suala la kupoteza halikuwemo kwenye hesabu. Hiyo iliisaidia, wakashinda mechi mbili kati ya tatu za ugenini walizocheza.

Tanzania ilicheza fainali za 1980 na sasa ni miaka 37, leo Uganda inacheza fainali ikiwa na miaka 39, labda na sisi tusubiri hadi tufikie miaka 39 kama Uganda.

Ninasema hivyo kwanini, Tanzania yetu, kila kitu ni miujiza tu, kila kitu ni zimamoto, kila kitu tunataka mafanikio ya papo kwa papo, hiyo haipo. Kinachotakiwa ni maandalizi ya muda mrefu kwa kuweka malengo kwamba lazima tucheze fainali za mwaka fulani kuliko kupapasa gizani.

Mwaka 2006 wakati Marcio Maximo anaingia, tuliweka nadhiri kwamba Tanzania lazima icheze fainali za Afrika 2008 zilizofanyika Ghana,

Kama wachezaji wangegangamala, tusingepoteza mechi kizembe, Tanzania ilikuwa na nafasi kubwa. Ni uzembe tu.

Taifa Stars ilifanya vizuri, ilikuwa ipate matokeo tu mechi ya Septemba 8, 2007 lakini ikafungwa na Msumbiji 1-0 mbele ya mashabiki wake. Imebaki historia.

Inatakiwa mikakati, mipango, mwelekeo na dhamira ya dhati kabisa kuwa lazima Tanzania icheze fainali za Afrika 2019.  Tukiweka dhamira, ikapigwa kampeni ya kitaifa, mbona inawezekana tu.

Tatizo la sisi wabongo ni bla bla nyingi na kwa staili hii, tutasubiri sana, na tutaendelea tu kugawana timu za kushabikia; mimi Cameroon, mimi Ghana itakuwa hivyo…

Hatuandai vijana, hatutengenezi timu mbadala za taifa, hatujengi misingi ya wachezaji kucheza nje, hatuna na tuitaishia kubadili makocha wa taifa kwa wachezaji wanaoibuka Simba, Yanga na Azam.

Vinginevyo labda tunaweza kufika fainali za Afrika kwa kudra za Mungu tukifikia miaka 39 kama Uganda. Tusubiri.