NDANI YA BOKSI: Fleva ile kaja nayo Aslay

Bongo Fleva katika wakati wake. Ilipokuwa ikichanua makucha yake. Hakuna muziki uliyobaki salama zaidi ya Bongo Fleva yenyewe. Taarabu ilishika adabu yake. Dansi ilisaluti na fleva za Mchiriku na aina ya ngoma kama hizo zilitoweka kabisa.

Kila kitu kilikuwa chini ya Bongo Fleva. Wanamuziki walitembea vifua mbele kama wamemwagiwa maji ya baridi mgongoni.

Ogopa sana mtoto wa Uswahilini toka Vituka kama siyo Yombo Dovya huko, anaposumbua masikio ya watoto wa kishua Oysterbay na Masaki.

Bongo Fleva ndo kitu pekee kilichovunja daraja la Uswahilini na Ushuani. Muziki huu ukafanya watoto wa kishua wajichanganye Uswahilini bila kulazimishwa ili tu wapate nafasi ya kuzoeana na Kibra Sir Nature.

Mastaa wa muziki huu walitokea Uswahilini wakaleta swaga za uswazi kitaa.

Wakati kabla ilikuwa fahari kuonekana unatokea Masaki au Obey. Ikawa kinyume chake sasa. Ukaanza ufahari wa kuonekana mtu unayetokea uswahilini kama Inspekta Harun Babu ni ujiko.

Bonge moja la dili. Kila kijana alitaka kutoka kimaisha kwa muziki huu. Na wapo ambao walitoka kimaisha bila kushika maiki wala kupanda jukwaani. Hawa waliitwa mapromota ingawa kiukweli hawakustahili kuitwa hilo jina. Maana ni miongoni mwa watu waliowapa stress kubwa wanamuziki kwa wakati ule.

Ukumbi wa Diamond Jubilee ulikuwa maarufu kuliko Jux wa sasa. Pale ndipo ulipokuwa unafanyika utakaso wa albamu za masela hawa waliogeuza kelele na maneno ya Uswazi kuwa pesa.

Wakajenga nyumba wakanunua magari. Wakapanga nyumba bora na kumiliki warembo classic kwenye jiji la Makamba wakati huo.

Wanamuziki wa muziki wa Bongo Fleva walikuwa wanathaminiwa zaidi kuliko wacheza soka na waigizaji popote pale. Yaani ilikuwa inawalazimu kina Sinta wajimilikishe mbavu za mtoto wa uswazi Nature ili washine kitaa.

Nature aliugeuza ukumbi wa Diamond Jubilee kama mali yake. Shamba la bibi. Mgodi wake. Aliujaza aliupindua na kuna wakati aliubomoa kabisa.

Siyo kwa makusudi bali ni ujazo wenye mbanano wa watu wengi kupindukia.

Ukisikiliza fleva za wakati ule na sasa. Unaweza kudhani kuwa wanamuziki wa wakati ule wanatokea sayari ya Jupita na hawa wa sasa wanatokea mwezini. Tofauti kubwa sana. Ukisikiliza kwa makini utaona tofauti kuanzia midundo mpaka swaga.

Wakati Chamilione alitamani kuwa Mr Nice. Wakati Nameless aliomba Mungu walau afanane ni TID kama siyo Chillah. Hivi sasa wanamuziki wetu wanatamani kuwa Davido. Fleva za Kinaijeria zimewashika kichwani na kupoteza ile ladha ya kina Latifah wa MB Dog.

Latifah aliyewageuza mateja wa Kibera Nairobi kuwa wanamuziki hata kwa kusikiliza muziki tu.

Latifah aliyefanya Matatu ya Kenya yageuke ukumbi wa disko kwa biti nzito za Majani toka Bamaga Dar es Salaam.

Tofauti ya sasa na zamani ni kwamba waliopo sasa wanapiga pesa ndefu kuliko wale wa wakati ule.

Walipiga pesa lakini siyo kwa level kama hizi za kina Shettah na wenzao. Kuna tofauti kubwa sana.

Mandojo na Domokaya wangetoka leo dunia ingesimama. Ingesimama kuwapisha Wamandavaku wavuruge akili za watu.

Muziki wa sasa umekuwa mwepesi wenye keshi. Zamani ulikuwa muziki mzito bila malipo. Malipo yalikuwepo lakini siyo kama hii leo. Zamani ili uweze kupata pesa nzuri ilikuwa lazima uhangaike sana. Utoe albamu. Ikubalike. Wadosi wakupe pesa ya maana. Uzinduzi ufanyike na upate wadhamini. Uzunguke kila mkoa kutangaza albamu kwa shoo.

Hii leo kamuulize Lavalava baada ya singo moja tu akueleze tofauti yake na kabla ya singo. Muziki wa sasa rahisi na wenye ukwasi.

Alichonacho Ruby hivi sasa nyumbani kwake au kwenye akaunti yake, kupitia muziki wake tu siyo mengine. Huenda ilimchukua miaka kadhaa Stara Thomas kupata kupitia muziki wake wa wakati ule.

Muziki wa sasa ni kama ndondi za Mayweather. Nyepesi zenye keshi. Muziki rahisi na pesa yake inapatikana kirahisi.

Kinachotokea leo kwa Aslay siyo uchawi wala miujiza. Siyo kwamba ameandikiwa na malaika na kutengenezewa na majini nyimbo zake.

Ni ile fleva ya wakati ule. Alichofanya Aslay kapita nyuma ya hawa ‘Machizi Unaijeria’. Karudi kule kwa kina Rahisa wa TID. Kwa Wanokunoku ya kina Mandojo na Domokaya.

Kaleta fleva ambayo masikio ya watu waliimiss na wale wa kizazi cha sasa hawakuwahi kuisikia kwenye midomo ya kina Jux, Vanessa, Ruby, Baraka The Prince na wenzao.

Ben Pol alituonjesha kwenye Moyo Mashine. Na ngoma ilistahili tuzo ile basi tu hizi Team Mitandaoni ziliondoa ndoto yake.

Sasa Aslay kaamua akandamize jumla. Ndo maana kila kona nyimbo zake zinatafuna muda wa masikio ya watu.

Fleva za kitambo enzi za kina Mr Paul na Buzi, zimekuwa kama kitu kipya kwa watu.