NDANI YA BOKSI: Tunasubiri wastaafu, wafe tuwape wanachostahili?

Muktasari:

Ni karibuni tu tumepoteza wadogo zetu huko Karatu kwa ajali ya gari, kifo tumeumbiwa na ni lazima kila mtu atakufa. Ila njia ya kupata umauti hutofautiana.

Kuna wapendwa wetu wengi ambao tumebaki nao kwenye dunia hii kupitia sauti tu. Video ama maandishi yao. Ardhi inameza sana watu. Dogo Mfaume kishatangulia. Alipigania uhai wake kwa kupambana kuacha matumizi ya dawa za kulevya.

Mpaka mauti yanamfika alikuwa ‘sobber house’, na aligoma kuondoka pale kurudi kitaa. Aliamini kuwa akirudi kitaa atashindwa kukwepa ushawishi wa kurudia tena ‘uduwanzi’ wa kubwia unga.

Alitaka kuwa salama. Na Mungu akataka awe salama zaidi kwa kumchukua jumla. Dogo Mfaume hatutamuona tena katika uso wa dunia hii.

Unaposoma hili andiko mchizi yupo ardhini kazungukwa na udongo. Mungu ampumzishe mahala anapostahili. Ameni.

Ni karibuni tu tumepoteza wadogo zetu huko Karatu kwa ajali ya gari, kifo tumeumbiwa na ni lazima kila mtu atakufa. Ila njia ya kupata umauti hutofautiana.

Mungu awape wapesi wale watoto majeruhi wanaoendelea na matibabu Marekani.

Kabla yake Dogo Mfaume, kuna wasanii wengi sana ambao walitangulia mbele ya haki lakini kabla ya umauti wao tuliwachukulia poa poa tu.

Walipoondoka jumla kwenye mboni za macho yetu kila mtu akajivisha ushahidi wa mema yao. Kila mtu alisifia na kufafanua ubora wa Ngwair, uwezo wa Kanumba, ukali wa Sharomilionea na wengine.

Lakini kabla ya mauti yao hakuna aliyesema sifa zao kwa kiwango sawa na kile baada ya mauti yao.

Tuache kusubiri wafe ndipo tuwasifie kana kwamba kutoa sifa kunaweza kuwarejeshea pumzi zao. Unafiki na akili za Waswahili ni kama mvua na Krismasi. Ni kulwa na doto. Hakuna sababu ya kusubiri afariki ili usifie uwezo wa kuandika wa Mwana FA kwenye muziki wa kizazi kipya.

Kutoka enzi za kina Miriam Odemba, Miriam Ikoa, Happyness Magesse mpaka katika utawala wa Flaviana Matata, Gigy Money, Lulu Diva, Linnah na kina Ruby. FA kaendelea kuwepo katika ubora ule ule.

Wako wapi waliokuwa na JB na Richie Richie, kwenye Mambo Hayo? Wao wameendelea kukomaa na sanaa kwa kiwango cha juu huku wakiutawala uwanja mbele ya wasanii wengi wapya. Lakini hizi sifa huwezi kuziona kwenye vinywa vya waswahili hawa jamaa wakiwa bado hai. Wanasubiri watangulie ndipo wamwage sifa nyingi, huku wengine wakishindana kwa mavazi na miwani ya giza misibani.

Ukitaka kujua kazi za msanii Bongo. Na ukitaka kumuelewa kwa mapana msanii wa Kitanzania. Subiri afariki.

Utajua kila kizuri chake na kuaminishwa kuwa hakuna tena kama yeye. Kabla ya hapo akiwa hai utayajua mabaya yake yote ya kweli na ya kusingiziwa.

Ufalme Bongo huletwa na waswahili baada ya mswahili mwenzao kufariki.

Akiwa hai huwezi kujua thamani yake. Huwezi kusikia kazi zake wala huwezi kuelezwa msaada wake kwa jamii inayomzunguka. Ndivyo ulivyokuwa kwa Ngwair. Wengi walijua ufalme wake na mengi juu yake baada ya kufariki. Alipambwa kila kona na nyimbo zake kupigwa kila dakika.

Wakati tayari tuliaminishwa na hao hao wapambaji kuwa amekwisha na hana jipya. Ndivyo ufalme ulivyokuwa hata kwa Kanumba, alikwezwa zaidi baada ya kufariki.

Kabla hajasukumwa usiku ule na kupelekea kufariki dunia, unadhani Kanumba alijua kuna watu wanaweza kuzimia kutokana na mapenzi yao kwake?

Aliishi kama msanii na kutambua ana thamani ila si kwa kiwango kile cha sifa za baada ya kufariki.

Unadhani marehemu Albert Mangwair alikuwa na uhakika kama bado thamani na ubora wa nyimbo zake unathaminiwa kwa kiwango hiki? Unadhani alikuwa anajua kama Mablogger wengi walikuwa wanajua uwezo wake kwa kina na kupelekea kuupamba kwa namna waliyompamba?

Wasanii wengi wana thamani kama hizi ila hatuzisemi na matokeo yake tunasubiri wafe tuseme. Wakifariki tunajivisha urafiki kwake na kujisingizia kuwa tuliwasiliana naye saa moja kabla ya mauti yake.

Unadhani baada ya kifo cha Kanumba hakuna msanii mkali mwingine wa filamu mwenye kuhusudiwa na kuthaminiwa kwa namna ile? Ila nani anasema?

Nani anaweza kusimamana na kuusifia uwezo wa Jacob Stephen katika upana na ubora wake? Tunaendelea kusemea chumbani kuwa jamaa mkali ila yakitokea ya kutokea kila mmoja atataka kusema. Wakati mwingine inauma sana kufa bila kujua thamani yako halisi.

Miezi kadhaa kabla Ngwair hajatangulia, tulimpita na tukadiriki kumbania nyimbo zake na wakati mwingine tulisema kachuja.

Ila vipi baada ya kifo chake? Hata zile redio zilizopiga nyimbo zake mwaka 2012 kwa mara ya mwisho zilipiga nyimbo zake saa 24, tena wakimwita mfalme. Inauma sana. Thamani hii anaipata akiwa katika maisha mengine kabisa! Akiwa chakula cha funza na mifupa kuwa sehemu ya udongo.

Leo kila mtu anamsema Diamond katika namna isiyofaa. Anaitwa mchawi, atasemwa hili atasemwa na lile. Ila ni nani anasema uwezo wa kuimba wa Diamond?

Nani anamtaja kama msanii aliyefanya mapinduzi katika suala la malipo na ubora wa shoo? Nani anapoteza muda wake kusema Diamond kaivusha boda Bongo Fleva kuliko yeyote hapo kabla? Hakuna!

Ila kama ingetokea la kutokea kila mmoja angemsema vizuri na kumuita kila jina bora analotamani kuitwa sasa na asiitwe.

Wakati mwingine ni vyema tukajifunza kutoa pongezi wakati huu bado wanatumia pumzi zao, tukiwa nao mitaani, tukiwatazama majukwaani na runingani.

Kama tunavyosahau mabaya yao wakifa, pia wakati mwingine tutoe pongezi wakiwa bado wako hai.

Ndiyo, tuwakosoe ila pia tuwapongeze inapobidi. Kama ilivyo sasa kwa nini usitoe pongezi kwa mtu kama Ray? Mtu kama JB, mtu anayeonekana kama anatembea na ufunguo wa soko la filamu? Wanafanya vizuri na wanafaa kupongezwa.

Leo vijana wengi wanatamani kufanya muziki. Unajua kwa nini? Wengi wameguswa katika nafsi zao na uwezo pamoja na mafanikio ya kina Diamond.

Kama kina Nature walivyofanya kina Godzilla kurap ndivyo umahiri wa akina Diamond unavyofanya leo kina Rayvanny wafanye wanachokifanya. Sasa kwa nini tusiwape sifa wanazostahili kwa wakati huu? Najua katika mioyo ya wengi kuna thamani na ubora wa Nature. Najua katika upande wa ukweli watangazaji wengi wanajua umuhimu wa kupiga nyimbo za Lady Jaydee. Ila kwa nini sasa hawapigi?

Tuache unafiki, tuishi katika dunia ya kweli na haki. Ni vyema kila anayestahili kupewa na apewe. Hii imekuwa sifa kuu ya Wabongo. Hata Jakaya Kikwete ubora wake tunauona baada ya kupumzika Msoga.

Alipokuwa Magogoni na lile tabasamu lake tulimtupia kila aina ya neno lisilofaa. Tulimuonea vya kutosha. Akatuacha. Tunamtamani leo.

Ilikuwa hivyo kwa Mkapa, kwa Mwinyi na mtangulizi wao Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Wote baada ya kustaafu tukaona umuhimu wao.

Haifai kuacha kupiga nyimbo nzuri ya Nature. Kisa? Jamaa yuko katika game kitambo apishe na wengine. Haifai! Anayestahili na apewe.

Kuna mengi yanazungumzwa baada ya vifo vya wasanii. Kama ni ya kweli kwa nini katika uhai wao wasipewe sifa hizo?

Dogo Mfaume ukikutana na Ngwair mpe sifa alizopewa baada ya kifo chake ajue thamani aliyoiacha nyuma yake.