NDANI YA BOKSI: Ukimfuatilia Diamond... Utafeli

Muktasari:

Sura yako itanuna, lakini moyo wako utakuwa unafuata mapigo ya ‘Fire Fire fire Baby... hebu cheka na sura ya kitoto...’. Mishipa yako ya damu itakuwa inafuata mapigo ya ‘Tanga kunani vurugu mechi Mkwakwani’. 

Kuna njia mbili pekee za kuishi maisha yako. Moja ni kama hakuna kitu cha miujiza. Nyingine ni kama kila kitu ni miujiza.

Watanzania na wanamuziki wote wa Bongo wamesimama wakimtazama Diamond katika kiwango chake cha juu kabisa cha muziki. Yuko juu sana.

Ukifanya kukaa na kubishana kila siku, unatoa maombi kwa shetani. Waliobishana mwanzoni wote wanaafiki kuwa yuko juu. Walioamini kuwa yuko juu tangu alipotoa wimbo wa ‘Nenda Kamwambie’ bado wanaamini yuko juu zaidi.

Wale masela wanaokaa maskani ambao muda wote wana akili ya ubishi, wanaamini yuko juu sana.

Sura yako itanuna, lakini moyo wako utakuwa unafuata mapigo ya ‘Fire Fire fire Baby... hebu cheka na sura ya kitoto...’. Mishipa yako ya damu itakuwa inafuata mapigo ya ‘Tanga kunani vurugu mechi Mkwakwani’. Mwishowe utashindwa kubana zaidi, hata sura itaanza kuimba ‘Sambaa chumbani yeye ndo Messi uwanjani, msiniibie Simba Yanga’.

Ifikie wakati tuache kuwafananisha wanamuziki wenzake wa hapa nyumbani na yeye. Tujifunze kama siyo kujilazimisha kumtofautisha nao.

Hii itawapa mizuka ya kufanya kazi kwa bidii zaidi ili wafikie kule aliko. Kusema mwanamuziki fulani wa Bongo Fleva ni zaidi ya Diamond ni kuikosea heshima biashara ya muziki.

Anataka nini zaidi? Ana gari la kifahari? Gari siyo ishu tena katika daraja lake. Anachotamani pengine ni kupata uhuru wa kuweza kupanda basi la mwendokasi. Nimetambua kwamba ukiyapenda maisha, maisha yatakupenda kwa usawia. Ndicho kinachotokea kwa Diamond.

Anapenda maisha. Ndiyo maana tangu aanze kupata umaarufu kwenye muziki wake hajawahi kukosea njia ya kupita.

Hataki kurudi Tandale. Anataka kuhama Madale. Anawafuata wenye maisha mazuri kama alivyofanya Bob Marley.

Bob Marley alipopata umaarufu na fedha hakutaka kuendelea kukaa ghetto za Jamaica na masela wake wa kitambo. Aliwamwaga kinomanoma.

Na jibu lake lilikuwa rahisi tu. Tunatafuta pesa ili tufanyeje? Akahamia zake Miami bata ndefu kwa rasta yule mpenda wanawake.

Kuna mamilionea wangapi katikati ya jiji la Dar es salaam hawatazamwi mara mbili? Kuna mamilionea wangapi katika ya jiji la Dar es salaam majina yao hayako midomoni mwa Watanzania? Mwishowe wanalazimishwa kuimbwa katika bendi.

Diamond Platinum yuko juu yao. Ngumu sana kushirikiana na Ne-Yo kama huna mtaji wa pesa na watu. Hasa watu. Inakuwa rahisi kwa staa mkubwa kushawishika kulingana na upana wa jina lako wewe unayetaka kufanya naye kazi toka Afrika Mashariki.

Diamond wa sasa anaacha kununua kiwanja Salasala au nyumba Sinza. Analipia kwa mtengenezaji wa video zake. Muziki unahitaji uwekezaji mkubwa.

Ni video ambazo hata Beyonce na Jay Z wanaweza kukaa sebuleni katika jumba lao la kifahari New York na kuzitazama.

Lakini Platinum mwenyewe anaamini hatakuwa juu ya kila mtu daima. Ndo maana unaona anavyozidi kuwekeza kwenye ardhi na biashara nje ya muziki. Anajua kuna wakati utafika ataanza kushuka chini. Atasimama katika kimo kile kile walichosimama wengi ambao walikuwepo wakapita, kama kina Awilo Longomba na wenzake.

Hakuna uchawi zaidi. Watu wana tabia ya kumchoka mtu. Si kwamba Diamond Platinumz atachokwa kwa kiwango chake, hapana. Diamond anaweza kuendelea kuwa yule yule. Katika ubora ule ule wa sauti, midundo na video.

Tatizo Watu hawapendi sana mtu mmoja akiwa juu kila siku. Wanamuziki wakubwa duniani yanawatokea haya. Kwa Bongo tena wataanza maneno ya chini chini kuwa ameisha. Baadaye watafanya kila wanaloweza kumnyanyua mtu mpya.

Kabla ya Diamond walimbeba zaidi Ally Kiba. Walipochoka walimuondoa, wakamkaribisha Platinumz.

Ndivyo maisha yetu wanadamu yalivyo. Hii ndio silika yetu watu wa ulimwengu huu. Tunapenda vitu vipya. Kitu cha muhimu zaidi kwa Platinumz ni kujitanua zaidi ya alipofika kibiashara. Atuache kabla hatujamuacha.

Kuisoma talaka yetu dhidi yake itakuwa ngumu kwake kuliko jinsi ilivyo rahisi kwake kuandika talaka dhidi yetu. Na kwa pale alipofikia Diamond siyo rahisi kushuka mpaka eneo alilokaa Mr Nice kwa sasa. Ni ngumu. Na inakuwa ngumu zaidi kutokana na namna ya uwekezaji wake kwenye muziki na biashara zingine.

Yatakuwa yaleyale ya kina R Kelly au Boys Two Men. Siyo kwamba wamefulia kimaisha bado wapo vizuri kiuchumi. Ila mazingira ya muziki yamewapa talaka wao.

Wapo kwao huko Marekani wanakula maisha, ila mboni zetu zimetengana nao kwenye runinga na jukwaani. Watu wanataka vitu vipya.

Ambwene Yessaya alitupa talaka Watanzania muda mrefu. Anaimba nyimbo na kutengeneza video zake kwa ajili ya watu wa mataifa ya nje ya Tanzania.

Haishangazi kuwa anabakia kuwa mwanamuziki wa kwanza kupata umaarufu zaidi nje ya mipaka yetu na wala hapandi jukwaa la Fiesta.

Nyimbo zake zipo kwa ajili ya Channel O, MTV Base, Trace na kwingineko. Angeendelea kuimba nyimbo kama ‘Yule’ na nyinginezo tungempa talaka kabla hajatupa talaka.

Lakini akaibuka kuwa mtu mjanja na makini akaachana na sisi mapema. Na siyo hayo tu, pia AY kwa kipindi kirefu alishaacha kutegemea pesa za shoo na albamu. Kitambo anafanya biashara ambazo pengine ndizo zinazomuingizia chapaa kwa wingi kuliko muziki.

Peter na Paul Okoye maarufu kama P Square walimjua AY kabla ya Diamond. Kuna watu wenye akili timamu wanaomzunguka Platinum. Ni hao hao wanaomkuza zaidi katika vyombo vya habari kiasi kwamba jina lake halitoweki kwa sababu mbaya au nzuri.

‘Diamond afumwa katika gari na Wema’.. ‘Diamond amsaidia maskini shilingi milioni moja’… ‘Diamond alala chumba cha mabilioni Malaysia’.

Watu wote walifanya kazi hii wakimuuza katika soko la ndani zaidi kwa wakati ule.

Achana na video yake ya Number One. Alitokea Mnijeria mmoja mfupi na mdogo kiumri kwa Diamond. David Adedeji Adeleke aliyezaliwa November 21, 1992 a.k.a Davido.

Huyu ndiye aliyechangia Diamond jina lake kutapakaa kwenye viunga vya majiji mengi Afrika. Ngumu sana kumtenga Davido na ustaa wa Diamond Afrika.

Hapa ndipo unapoona kuwa Diamond na watu wake wanaomzunguka wako makini sana kutumia fursa. Tofauti sana na wanamuziki wenzake wa Kitanzania.

Wengi wao wanaamini katika kipaji kuliko kujiongeza. Drama za Diamond na Wema na saga za Diamond na Zari wake. Ni mambo ambayo yanatufanya tushindwe kumuondoa Diamond kwenye vinywa na masikio yetu.

Mr Nice alishindwa katika hatua hii. Zaidi ya nchi ambazo zinazungumza Kiswahili, hakwenda mbali zaidi.

Na tatizo alitegemea nyimbo zake zijitangaze kuliko watu wake wa masuala ya biashara kumtangaza.

Platinumz hajapitia njia hii ya Mr Nice. Yeye kapitia njia za kina P Square, Davido, Jay Martins, Jose Chameleon, Cabo Snoop na wengineo.

Kinachoendelea hivi sasa ni stress tupu kwa wasanii wengi wa Bongo. Kuna vitu wanashindwa hata kupost mitandaoni kwa sababu kitakachopostiwa na Diamond kitatazamwa zaidi.

Akiposti gari yake atakuwa zaidi yao. Akiposti nyumba zake atakuwa zaidi yao. Akiposti video za shoo zake ni zaidi yao. Akiposti picha ya ofisi yake atakuwa zaidi yao. Kila kitu yuko hatua kumi mbele yao.

Diamond anapoingia kwenye kituo cha redio kufanyiwa interview, shughuli zote zinasimama. Kila kitu kinamuangalia yeye mpaka viyoyozi vya studio vinamnyenyekea.

Maiki zinatoa sauti kwa adabu. Zinajua kuna mwamba yupo mjengoni siku hiyo.

Hilo lipo kwa kituo chochote cha redio. Sasa aende msanii mwingine kwenye studio hizo. Atakavyotazamwa ni kama naye ni miongoni mwa wafanyakazi wa kituo hicho. Hakuna mtangazaji wala mfanyakazi anayeshituka.

Kuna tofauti kubwa sana kwa Diamond na wanamuziki wenzake wa Kitanzania. Anawapa wakati mgumu sana wa kuongeza bidii. Waache kuumizwa na kile kinachotokea kwa Diamond hivi sasa. Wafanye kazi bora na kujituma watanyenyekewa.

Badala kuwaza kuwa unastahili kuwa kama Diamond kimaisha. Fanya kazi kwanza kwa kujituma ili uanze kufikiria hilo. Huwezi kustahili kuishi maisha ya Diamond kwa kuendelea kuishi kama digidigi.

Jitokeze. Fanya kazi. Jitume. Usiogope kuwa kiherere. Usifuatilie kile anachofanya Diamond kwa sasa. Hakijaja kama bahati mbaya kwake aliyaandaa haya mazingira aliyonayo hivi sasa.

Ukiacha kujituma kivyako na kufuatilia hatua za Diamond wa sasa hivi... utafeli. Kuna wakati maisha yanahitaji kitu kingine zaidi.