NGUVU MPYA KIKOSINI Makocha, wakongwe wawataja mapro zaidi ya Msuva na Samatta

Muktasari:

  • Asilimia kubwa ya vigogo ambao wanatawala kwenye soka la Afrika vikosi vyao vya timu za taifa zimeundwa na wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa nje ya mataifa yao kwenye ligi zenye ushindani zaidi.

Uzoefu wa michezo ya kimataifa kwa wachezaji wa Kitanzania ni mwarobaini unaotajwa kuwa utaisaidia Taifa Stars kuwa moto wa kuotea mbali ndani na nje ya Afrika.

Asilimia kubwa ya vigogo ambao wanatawala kwenye soka la Afrika vikosi vyao vya timu za taifa zimeundwa na wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa nje ya mataifa yao kwenye ligi zenye ushindani zaidi.

Mchambuzi wa kituo cha luninga cha Sky Sports, Thierry Henry ambaye aliwika enzi zake za uchezaji soka na klabu kama Monaco, Juventus , Arsenal na Barcelona aliwahi kutoa mtazamo wake juu ya mafanikio ya mataifa makubwa duniani.

Henry ambaye anaamini kwenye uwekezaji wa vijana anasema kuwa kujengeka kwa wachezaji hutegemea kiwango cha ushindani na idadi ya mechi wanazocheza kwa msimu mzima ni rahisi kocha kutengeneza muunganiko kwa wachezaji ambao wako tayari kiushindani.

Idadi ya nyota wa Kitanzania ambao wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi ni kubwa kulingana wale ambao wamekuwa wakiitwa kila siku huku wengine wakionekana kufungiwa vioo.

Miongoni mwa nyota hao ni beki wa zamani wa Simba, Emily Mgeta anayechezea VFB Eppingen (Ujerumani); John Lema wa Sturm Graz (Austria), Said Muhando wa Chiasso FC (Uswisi), Maurice James wa Eletrico FC (Ureno), Ali Bwando wa Roda (Uholanzi), na Gloire Amanda anayechezea Whitecaps ya Canada.

Hao ni baadhi ya msururu wa wanasoka ambao jarida hili lina mawasiliano yao, ukiacha Mbwana Samatta aliyezoeleka, wachezaji wa Tanzania wako wengi ambao pamoja na kwamba hawaitwi, wenyewe shauku yao kubwa ni kuitumikia timu ya taifa.

Jarida hili limefanya mahojiano na nyota wa zamani wa Ligi Kuu Bara pamoja na makocha mbalimbali wamemtaka Mayanga kuendelea kutoa nafasi kwa nyota wanaocheza kwenye ligi za ushindani.

Maneno ya nyota wa zamani

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa amesema moja ya nguzo inayoweza kutusaidia ili kuwa na nguvu ya kushindana na mataifa makubwa ni kuwaita nyota wote wa Kitanzania wanaocheza nje ya nchini.

“Kuna mataifa yanagombania wachezaji kwa hiyo inatakiwa tutambua umuhimu wao, kama tungekuwa na ligi bora na yenye ushindani ingetusaidia wachezaji wetu kujengeka.

“Lakini huko kwenye ushindani huo hatujafika bado kwa hiyo kilichopo ni kuwageukia nyota wetu ambao wanacheza nje ili kutumia uzoefu na uwezo wao wa ushindani,” anasema Pawasa.

Nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua amesema tunaweza kuwa taifa la ajabu kama tutashindwa kuwatumia wachezaji wetu wa Kitanzania wanaocheza nje.

“Ukifuatilia wenzetu Ghana, Mali, Tunisia, Senegal, Nigeria, Uganda na mataifa mengineyo karibu nusu wa wachezaji wao wanatoka Ulaya na wamekuwa wakiitwa mara kwa mara kwenye timu zao za taifa.

Hiyo ilimsaidia kocha wa Uganda alikuwa akiwaita na waliisaidia Uganda kucheza Fainali za Afrika baada ya muda mrefu. Mara ya mwisho ilikuwa 1978 na ikacheza fainali za mwaka jana huko Gabon japo hawakufanya vizuri sana.

“Ushauri wangu, ungetengwa mchezo hata mmoja wa kirafiki halafu wakaitwa wachezaji wote wa Kitanzania ambao sura zao ni ngeni kwetu ili watizamwe, tunaweza kupata wachezaji wa kutusaidia kwa kiwango kikubwa,” anasema Chambua.

Kiungo wa zamani wa Yanga, Ali Yusuph ‘Tigana’ anasema kuitwa kwa wingi kwa nyota wa Tanzania wanaocheza nje kutaongeza changamoto kwa wachezaji ndani.

“Kimsingi wanatakiwa kuitwa ili walisaidie taifa, lakini pia natizama kama moja ya njia ambayo itawafanya wanaocheza ndani kuona kumbe inawezekana na mwishowe wakaongeza juhudu ili wapige hatua na wao kutoka,” anasema Tigana.

Anasema kuwa inawezekana wachezaji wa Tanzania hawana moto wa kutoka nje kutokana na kwamba hakuna kinachowahamasisha. “Motisha pekee ni kama hiyo ya kuwaita wachezaji wengi wa Tanzania wanaocheza nje na tuone vitu vyao na kuwavuta wengine.

“Hata tukitumia wachezaji wa nje, kunashtua mataifa mengine. Wao wataleta wakali wao na sisi tukileta wakwetu labda tukawachanganya kidogo na wa hapa kwa kuwa na wao wana vipaji, tunaweza kufika mbali

Nyota wa zamani wa Yanga, Ally Mayay ‘Tembele’ ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka anasema kuwaita ni jukumu la kocha kutokana na mipango yake.

“Hatuwezi kumpangia kocha wachezaji wa kuwaita lakini ni vyema kutoa nafasi kwa sura mpya ambazo zinaweza kusaidia pindi ambapo Samatta na Msuva wakitokea wamepata majeraha waweze kuokoa jahazi,” anasema mchambuzi huyo.

Hata hivyo, Tembele anasema mataifa mengi yamekuwa na utaratibu wa kuwaamini wachezaji wao wanaocheza soka la kulipwa kwenye ligi kubwa barani Ulaya.

Naye mshambuliaji wa zamani wa Simba na Yanga, Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ametoa angalizo kwa kusema hao nyota wanaocheza nje wafuatiliwe vya kutosha.

“Sio kila mchezaji anatakiwa kucheza timu ya taifa, kuna wengine wanacheza nje ya nchi lakini unaweza ukakuta nidhamu zao ni mbovu, kiukweli wachezaji wa kimataifa tunauhitaji nao mkubwa, lakini wafuatiliwe na sidhani kama kuna utamadunia wa kufuatilia watu,” anasema mshambuliaji huyo.

Wanachosema makocha wa Ligi Kuu

Kocha wa Njombe Mji, Ally Bushiri anasema lazima tumpe muda Mayanga wa kufanikisha mipango yake na sio kumuingilia kwa kumpangia yale ambayo tunayaona kwetu ni sahihi.

“Kuwa na wachezaji wanaotoka kwenye ligi za ushindani ni faida kwenye taifa lolote lakini hutegemea sana na mipango ya kocha, unaweza kuwa na wachezaji wenye majina makubwa lakini mafanikio yasipatikane,” anasema Bushiri.

Kocha wa Tanzania Prisons, Abdallah Mohammed amesema kutoa nafasi kwa wachezaji wapya wa Tanzania ambao wanacheza kwenye ligi kubwa kunaweza kukiimarisha kikosi.

“Inaweza kuchukua muda kuelewana lakini kama wakiwa anatoa nafasi kwa mmoja baada ya mwingine mara kwa mara basi tunaweza kuwa na kikosi bora maana hao wanaocheza nje watakuwa na uwezo mkubwa wa ushindani,” anasema kocha huyo wa Tanzania Prisons.

Kocha msaidizi wa Majimaji ya Songea, Habibu Kondo anasema wachezaji wanao cheza nje wanaweza kuongeza ushindani wa namba Taifa Stars.

“Kama wapo waitwe maana wakiwepo watatufanya kuwa na machaguo mengi na hata kocha hatoumizwa kicha kama akishindwa Samatta na Msuva basi watafanya kazi wengine ambao wana uwezo kama hao,” anasema.

Kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma anasema kuwa mchezaji anayecheza kwenye ligi kubwa anaweza kuwa na vitu vingi vya ziada ambavyo vinaweza kwenda na mipango ya kocha.

Naye kocha wa JKT Tanzania, Bakari Shime amesema kupata taarifa sahihi za wachezaji wanaocheza nje inaweza kuwa changamoto kwa benchi la ufundi la Taifa Stars.

“Kungekuwa na wepesi kama kocha angekuwa anahusika mwenyewe kwenye ufuatiliaji kwa maana ya kwenda viwanjani, lakini vinginevyo ni ngumu kuchukua uamuzi wa kumwita mchezaji ambaye hujamwona.

“Pengine atengewe uwezeshwaji wa kuwatembelea wachezaji hao na kuona viwango vyao pindi wanapokuwa wakicheza,” anasema kocha huyo.

Wasikie Ninje na Mayanga

Kocha wa Ngorongoro Heroes, Ammy Ninje anaamini kuwa utaratibu wa kuwa na wachezaji Taifa Stars na vikosi vingine vya vijana vinaweza kusheheni nyota wengi wa Kimataifa kutokana na ufuatiliaji unaoendelea.

“Wapo Watanzania ambao wanacheza nje ni kweli lakini asilimia kubwa wamechukua uraia wa mataifa mengine, nashirikiana na Mayanga wanaoendelea kupatikana tutawatumia.

“Binafsi nimeanza na Abdul Nasry kutoka Senegal kwenye Akademi ya Aspire, milango kwa wengine ipo wazi,” anasema Ninje.

Hata hivyo naye, Mayanga anayeinoa Taifa Stars anasema kuwa Watanzania waendelee kumpa muda kwa kuwaita mmoja mmoja nyota wenye uraia wa Tanzania ili kuona ni kwa namna gani wanaweza kuisaidia nchi.

“Mpango nilionao ni kutoa nafasi kwa wachezaji ambao wanacheza nje ya nchi lakini nafasi hiyo siwezi kutoa kwa wakati mmoja eti niwaite wote, ikumbukwe nina kazi ya kuendelea kuijenga timu.

“Nikisema nifanye hivyo imna maana nitaharibu na kazi ambayo tayari nimeianza na tumefika pazuri, wachezaji ambao nina mawasiliana nao na wanacheza nje nafuatilia maendeleo yao,” anasema kocha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar.