Wednesday, February 14, 2018

Nafasi ya wanasiasa katika kulinda amani uchaguzi wa Jumamosi

 

Jumamosi ya wiki hii wananchi katika kata tisa na majimbo mawili wanakwenda kupiga kura katika uchaguzi mdogo wa madiwani na ubunge.

Uchaguzi huo utafanyika katika majimbo ya Kinondoni, Dar es Salaam na Siha mkoani Kilimanjaro. Kata ambazo zinafanya uchaguzi ni Isamilo wilaya ya Chamagana, Manzase (Chamwino), Madanga (Pangani), Mitunduruni (Singida), Kanyelele (Misungwi), Buhangaza (Muleba) na kata za Donyomurwak, Gararagua na Kashashi wilayani Siha.

Katika mahojiano haya Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kailima Ramadhani anaeleza mambo ambayo wapiga kura na wadau wengine wa uchaguzi wanatakiwa kuyazingatia katika kufanikisha uchaguzi huo mdogo.

Swali: Nani anastahili kupiga kura katika uchaguzi wa Jumamosi?

JIbu. Wenye haki ya kupiga kura Jumamosi ni wale wote ambao walijiandikisha kwenye daftari la wapigakura lililotumika katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Jumla ya watu 361,781 ndio wanategemewa kupiga kura katika uchaguzi huu. Kati ya hao ukiondoa wapigakura 2,705 wa Kata ya Kimagai katika halmashauri ya Mpwapwa ambako mgombea wa CCM alipita bila kupingwa, wanabaki wapigakura 359,076.

Vyama vyote vya siasa vilishapewa nakala ya daftari hili, hivyo ni vema kila chama kikawapatia nakala mawakala wao ambao watakuwa kwenye vituo vya kupigia kura.

Ila tuwakumbushe tu vyama vya siasa kuwa nakala ya tume katika kituo, ndiyo nakala itakayokuwa sahihi iwapo kutatokea tofauti.

Swali: Itakuwaje kwa wale ambao wamepoteza kadi ya kupigia kura?

Jibu: hao wanaweza kutumia vitambulisho vya taifa, hati za kusafiria au leseni za udereva. Matumizi ya vitambulisho hivyo yatazingatia masharti yafuatayo:

Kwanza, lazima mpigakura awe aliandikishwa kwenye daftari mwaka 2015.

Pili, majina yake yawe katika orodha ya wapiga kura katika kituo husika. Majina na herufi za majina hayo yaliyopo katika kitambulisho yafanane kwa herufi na mtiririko na yale yaliyopo katika daftari.

Sura ya mpigakura iliyopo katika kitambulisho ifanane na iliyopo katika daftari.

Hati ya kiapo (Affidavit) cha kuthibitisha majina zaidi ya yale yaliyomo kwenye daftari hakitaruhusiwa kutumika.

“Lengo la Tume ni kuwapa fursa na haki walioandikishwa kuwa wapiga kura, lakini wangeweza kuikosa haki hayo kwa kukosa kadi za kupigia kura sababu ya kupotea au kuharibika au kuchakaa.”

Swali: Kuna vituo vingapi vya kupigiakura na mambo gani ya kuzingatiwa kwenye vituo?

Jibu: Vituo 907 vitatumika kupiga kura. Vituo hivi ndivyo vilivyotumika mwaka 2015. Lakini, kwa kuwa mgombea wa kata ya Kimagai amepita bila kupingwa, kata hiyo haitafanya uchaguzi.

Kata hiyo ina wapiga kura 2,705 na vituo vinane. Hivyo vituo vya kupigia kura vimebaki 899.

Wasimamizi wa uchaguzi watavipatia vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mdogo orodha ya vituo vya kupigia kura.

Orodha ya wapiga kura ilishabandikwa katika kila kituo cha kupigia kura tangu Februari 9, 2018 ikiwa ni siku nane kabla ya siku ya upigaji kura na hivyo kila mpiga kura aende kwenye kituo chake ambako jina lake limebandikwa.

Kwa wananchi wa kata za Kigogo, Kijitonyama na Mwananyamala kuna vituo ambavyo vimehamishwa kutoka vituo vilivyotumika uchaguzi wa 2015 na kuhamishiwa maeneo mengine kwa sababu mbalimbali. Wananchi wa maeneo hayo wanashauriwa kwenda katika vituo vilikohamia ili wakahakiki majina yao kabla ya siku ya kupiga kura.

Swali: Kwenye vituo vya kupigia kura kutakuwa na mawakala wa vyama, kazi yao ni nini?

Jibu: Kazi za mawakala wa upigaji kura, kutambua wapigakura, kuwakilisha na kulinda maslahi ya mgombea au

wagombea katika kituo cha kupigia kura; na kazi nyingine ni kushirikiana na msimamizi wa kituo na wasimamizi wasaidizi wa kituo ili kuhakikisha taratibu zinazohusu upigaji kura na uchaguzi zinafuatwa.

Swali: Sifa ya wakala wa chama cha siasa ni ipi?

Jibu: Wakala wa chama cha siasa atakubalika kusimamia uchaguzi iwapo atakuwa na barua ya uteuzi kutoka chama chake cha siasa ambayo inafafanua jina lake, anuani yake na kituo atakachoenda kusimamia.

Pia wakala anatakiwa kuwa ameapa kiapo cha kutunza siri kupitia fomu namba sita (6). Kiapo hicho kitafanyika siku saba kabla ya siku ya kupiga kura.

Wakala huyo anakuwa na sifa pia iwapo atakuwa na barua ya kumtambulisha kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo kwenda kwa msimamizi msaidizi wa kata. Kama kuna wakala atakuwa hana sifa hizo, huyo hastahili kusimamia uchaguzi.

Swali: Siku ya kupiga kura, vituo vitafunguliwa saa ngapi?

Jibu: Vituo vya kupigia Kura vitafunguliwa saa 1.00 asubuhi na vitafungwa saa 10.00 jioni. Baada ya saa 10:00 jioni askari atasimama nyuma ya mtu wa mwisho aliyepo kwenye mstari.

Swali: Baada ya upigaji kura kukamilika, kura zitahesabiwa wapi?

Jibu: Kura zitahesabiwa katika vituo vya kupigia kura. Kituo cha kupigia kura kitageuka kuwa cha kuhesabia kura baada ya upigaji kura kukamilika.

Hata hivyo, kwa sababu za kiusalama msimamizi wa kituo kwa kushauriana na mawakala wa upigaji kura anaweza

kuelekeza kura zikahesabiwe eneo lililo jirani litakalofaa, tofauti na lile ambalo kura zimepigwa.

Swali: Kitu gani kinafuata baada ya kuhesabu kura?

Jibu: Baada ya kura za kila kituo kuhesabiwa mbele ya mawakala na kubandikwa katika kila kituo, matokeo ya vituo vyote vya kupigia kura katika kata husika hujazwa kwenye Fomu Na. 24C mbele ya mawakala wa kujumlisha matokeo.

Msimamizi msaidizi wa uchaguzi baada ya kujiridhisha na kuthibitisha matokeo ya kura za kila mgombea atatangaza mgombea aliyepata kura halali nyingi zaidi kuwa ndiye mshindi.

Kifungu cha 86 cha sheria hiyo ya uchaguzi kinafafanua kuwa kutokuwepo kwa mawakala wakati wa upigaji au kuhesabu au kujumlisha kura katika muda na mahali palipoteuliwa, hakutabatilisha utekelezaji wa

majukumu ya Tume yaliyofanyika kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.

Kifungu cha 82 cha sheria ya uchaguzi, jukumu la kutangaza matokeo ni la Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Swali: Tunafahamu kuwa uchaguzi huu unahusisha waangalizi wa uchaguzi. Nini wajibu wa waangalizi hao?

Jibu: Watazamaji wa uchaguzi wa ndani ndiyo wanaoruhusiwa katika uchaguzi mdogo.

Kazi ya watazamaji wa uchaguzi ni kuona kama uchaguzi unafanyika kwa mujibu wa Katiba, sheria, taratibu, kanuni za uchaguzi na maelekezo yaliyotolewa na Tume ya Taifa yaUchaguzi.

Watazamaji watafanya kazi yao baada ya kukubaliwa na kupewa idhini na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Mtazamaji hatakiwi kuingilia kwa namna yoyote kazi na majukumu ya Tume ya Taifa Uchaguzi.

Swali: Waandishi wa habari ni muhimu katika kuripoti uchaguzi huu, je Tume imeandaa mazingira yao kufanya kazi kwa ufanisi?

Jibu: Kipengele cha 9.15 cha kitabu cha Maelekezo kwa wasimamizi wa uchaguzi kinafafanua kuwa waandishi wa habari wanaruhusiwa kuingia katika vituo vya kupigia kura kwa idhini ya msimamizi wa uchaguzi.

Swali: Una ujumbe gani kwa wapiga kura na vyama vya siasa?

Jibu: Vyama vya Siasa vitimize wajibu wao ipasavyo kwa kuhamasisha wanachama wao walioandikishwa kuwa wapigakura wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura siku ya Jumamosi kumchagua mbunge na diwani wanayemtaka.

Ni imani ya tume kuwa viongozi wa vyama vya siasa watakuwa chachu ya kuwaongoza na kuwaelekeza wanachama, wafuasi na mashabiki wao katika kushiriki uchaguzi kwa amani na utulivu.

Mwandishi wa Makala hii ni Ofisa Habari Mwandamizi wa NEC. Anapatikana kwa simu 0788 014 648

-->