Najua tu naonekana mgeni

Muktasari:

  • Dk Msolla akaita wachezaji wake, kati ya aliowaita alikuwemo Ammy Ninje. Watu wakawa wanajiuliza “huyu Ammy Ninje ni nani? Katokea wapi” Mbona hatukuwahi kumsikia?”

Mwanzoni mwa miaka ya 2000, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilimteua Dk Mshindo Msolla kuinoa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Dk Msolla akaita wachezaji wake, kati ya aliowaita alikuwemo Ammy Ninje. Watu wakawa wanajiuliza “huyu Ammy Ninje ni nani? Katokea wapi” Mbona hatukuwahi kumsikia?”.

Akamtetea,akisema anamfahamu na alikuwa anamfuatilia huko England. Itakumbukwa hakucheza mechi nyingi kwa kuwa alibanwa na majukumu ya timu yake huko nje.

Juzi juzi, TFF ilimtangaza Ninje kuwa kocha wa Kilimanjaro Stars iliyoko Kenya kushiriki Kombe la Chalenji, na jana ilicheza na Libya.

Lakini bado wadau wanajiuliza “huyu Ninje ni nani hasa? Asili yake ni wapi” kwa kuwa anaonekana kama ni mgeni kwenye kikosi hicho cha Tanzania Bara.

SI MGENI TANZANIA

Kwanza Ninje anasema yeye si mgeni kwani ni msaidizi wa kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga tangu alipoteuliwa.

Amekuwa na timu kipindi chote na zaidi ndiye msimamizi wa timu na Mayanga ni kama anaratibu. Kimsingi anasema kuwa anaonekana mgeni kwa kuwa hafundishi timu yoyote ya Ligi Kuu kama ilivyo makocha wengine wazawa.

“Ninasaidiana na Mayanga Taifa Stars hivyo mimi si mgeni kama wengi wanavyodhani,” anasema Ninje katika mahojiano na Spoti Mikiki.

“Nina ujuzi wa kutosha ambao nimetoka nao Uingereza ambako ndiko nilipojipatia elimu ya ukocha na uzoefu kwa kukaa chini ya makocha kadhaa Uingereza na Tanzania.”

CHALENJI

Ninje anaipeleka Tanzania kwenye michuano ambayo haina rekodi nzuri ya mafanikio, lakini haonekani kuwa na hofu nayo.

“Nimejipanga, ninafahamu Chalenji haina mabadiliko sana,” anasema.

“Haya ni mashindano ambayo kila mchezo una umuhimu wake, itatulazimu kupata matokeo ya ushindi kwenye kila mchezo utakaokuwa mbele yetu. Ninafurahia kuwa na kikosi kizuri chenye wachezaji wepesi kushika maelekezo.

“Kikubwa ni Watanzania kuniunga mkono, mengine watajionea wao wenyewe uzuri. Hayo mashindano huenda yakaonyeshwa hivyo wataiona timu yao itakavyokuwa ikipambana.”

Kabla ya kuondoka nchini Kili Stars ilijikita hasa kwenye mazoezi na kufanyia kazi mfumo wa namna ya uchezaji kwa kuanzia eneo lake la nyuma. Mara nyingi katika mazoezi, Ninje alionekana kutaka timu yake ianzishe mashambulizi kutokea kwenye ngome; mabeki wa kati au pembeni kulingana na hali ya mchezo.

KUNDI A

Katika mashindano ya Kombe la Chalenji, ambayo hushirikisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na majirani pamoja na kualika timu za nje ya ukanda, Tanzania Bara imepangwa Kundi A pamoja na Kenya, Libya, Zanzibar.

Ninje anakubali kuwa hilo si kundi jepesi, lakini ana matumaini ya kufanya vizuri.

“Tumejiandaa vizuri hivyo hatuna cha kuhofia. Timu zote tunazichukulia kwenye daraja moja,” anasema.

“Katu hatuwezi kuibeza timu yoyote kwa sababu kwenye soka ile ambayo hauipi nafasi, inaweza kuonyesha maaajabu ambayo husababishwa na uzembe.

“Dharau inasababisha kutofanya kitu kwa ufasini, ndiyo maana ninasema tumejipanga.”