Monday, July 17, 2017

Namba nyingine ya Taifa Stars hii hapa, iko Austria

By Eliya Solomon, Mwananchi

Dar es Salaam. Wiki iliyopita, Kocha wa Taifa Stars ambaye juzi alikuwa na majukumu ya mashindano ya CHAN dhii ya Rwanda, alisema ataanza kuwaita wachezaji wa Tanzania wanaocheza nje ya nchi.

Alisema kuwa ni wakati sasa wa kuwatumia Watanzania hao waliotawanyika klabu mbalimbali za duniani, Ulaya, Amerika, Afrika na kwingineko.

Spoti Mikiki limekuwa mstari wa mbele kuwaibua wachezaji hao ambao kutoka pembe za dunia na katika mahojiano, kila mmoja anataka japo aitwe kwenye timu ya taifa kwa kuwa bado wanakumbuka fadhila pamoja na kuchangia uwezo wa uwanjani kuipigania Taifa Stars.

Wiki iliyopita, Spoti Mikiki ilifanya mahojiano na mchezaji wa Tanzania, Orgenes Mollel anayecheza soka la kulipwa nchini Ureno kwenye klabu ya Daraja la Kwanza ya F.C. Famalicão ambaye aliomba Mayanga amjumuishe timu ya taifa.

Ni kama Kocha Mayanga amesikia ombi lake kwani alisema kuwa Mollel ni kati ya wachezaji wa mwanzo watakaokuwa kwenye hesabu ya kuitwa kwenye mechi za kalenda ya Fifa, baadaye Septemba.

Spoti Mikiki limemuibua mchezaji mwingine wa Tanzania, ambaye ni hazina ya Taifa Stars kwani ni kijana mdogo na uchanga wa umri na uzoefu wa nje, ni faida kwa Taifa Stars, Michael  John Lema (18)  ambaye anacheza soka la kulipwa nchini  Austria

Pata undani wake sasa

Katika mahojiano na Spoti Mikiki kutoka Graz, Austria, Lema (18)  anasema anacheza soka la kulipwa katika  timu ya SK Sturm Graz ya Ligi Kuu Austria.

Austria ni moja ya mataifa yaliyoendelea kisoka chini ya Shirikisho la Soka  Ulaya (UEFA) na mara kadhaa timu za nchi hiyo zimekuwa zikipata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Lema anasema kuwa wakati wowote anaweza kupandishwa kikosi cha kwanza kutokana na kiwango kizuri alichokionyesha  msimu uliopita  wa 2016/2017 ambapo aliichezea  SK Sturm Graz II Ligi Daraja la Tatu ngazi ya taifa.

Kwa mfumo wa Austria, timu za Ligi Kuu zina nafasi ya kutoa vikosi vyao B ili kushiriki Ligi Daraja la Tatu kwa lengo la kuwapa nafasi vijana wao kupanda viwango na hata timu hizo zikifanya vizuri hazipewi  nafasi ya kuwa Ligi moja na timu mama.

Ndivyo ilivyo kwa SK Sturm Graz na  timu yao  B ambayo ni SK Sturm Graz II inashiriki ligi hiyo.

Kiu ya Taifa Stars

Lema anaelezea namna anavyotaka kuitumikia Taifa Stars japo aliwahi kuichezea timu ya Taifa la Austria chini ya miaka 19.

“Sihitaji kuendelea kuichezea Austria, nilichezea timu zao za vijana  kwa kuwa nilijua bado nitakuwa na nafasi ya kuichezea Tanzania kwa siku zijazo ndio maana nimesema sina nia ya kutaka kuendelea kuichezea timu yao tena isije kutokea utata baadaye.

“Mimi ni Mtanzania kabisa wa asilia ambaye nimezaliwa  Itigi mkoani Singida, wazazi wangu wote ni Watanzania na wanaishi wote nchini Tanzania.

“Ujio wangu huku ulikuwa nikusoma na nilikuja 2009 na kwa sababu ya kipaji changu ilinifanya kuwa najihusishe na soka, kwa bahati nzuri walinichukua kwa kunifundisha kuanzia ngazi ya  akademi,” anasema Lema.

Winga huyo anayeishi nchini humo kwa rafiki wa mama yake anaelezea pia matumaini yake ya kupandishwa kwenye kikosi cha kwanza cha timu yake hiyo inayoshiriki Austrian Bundesliga.

“Kocha wa timu ya kikosi cha kwanza, Franco Foda amekuwa akivutiwa na uwezo wangu na ilikuwa nipande msimu uliopita lakini alitaka nikomae zaidi kwanza mara baada ya kupanda kutoka kwenye akademi.

“Kucheza kwangu daraja la tatu na SK Sturm Graz II kumenikomaza na kunifanya kuwa na uwezo wa kupambana dakika zote bila kuchoka wala kuhofia chochote.

“Ninachosubiri ni  kupandishwa awamu hii ili nicheze kikosi cha kwanza, ujue hata kocha wangu wa timu B Joachim Standfest ameniambia jina langu ni miongoni mwa majina aliyoyapendekeza kupandishwa.” anasema mchezaji huyo.

Hata hivyo Lema alimalizia kwa kusema mzalendo ni yule ambaye  yupo tayari kupigania taifa lake katika mazingira  yoyote na kwamba yuko tayari kuja endapo kocha wa Taifa Stars atamuita hata kwenye timu ya U-20

Kupita hoja hiyo, anaamini kuwa yeye ni mzalendo na kusema kuwa anatarajia kuja Tanzania kwa mapunmziko hivi karibuni na hatosita kulitembelea Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, ili wamtambue na pia kuonana na kocha wa Stars, Mayanga.

-->