Namna mbalimbali za usafishaji macho na ulimi kujikinga na magonjwa

Sunday March 19 2017

 

By Freddy Macha:Kutoka London

Maendeleo ya kiteknolojia yametuletea faraja na maafa. Teknolojia ya karne ya 21 inatumia tarakimu zinazoitwa “digitali” kwa lugha ya kitaalamu. Digitali inatokana na neno “digit” inayomaanisha sifuri hadi tisa. Unapofungua chochote kinachotumia kompyuta: simu, tarakilishi, televisheni, magari, kamera na taa za barabarani huendeshwa kwa mkusanyiko wa ‘matarakimu’ yenye mkusanyiko kama: 101110111000.

Maendeleo ya kidigitali yanaendelea kuzagaa Afrika na juu ya furaha kuna uelewa finyu. Muhimu kabisa ni afya ya miili yetu.

Magari, viwanda, moshi wake na kelele zinatudhuru sana bila kujua.

Macho yetu yanadhurika na juu ya vumbi la kawaida la Bongo, kuna uchafu wa mazingira. Zamani nikiishi Brazili nilishangaa nilipoanza kuwa na kipele kilicholjaa mafuta chini ya jicho moja. Nilipokwenda kwa mganga akaniambia kwa vile kope zangu hazisafishwi sawasawa, uchafu wa mazingira umeathiri jicho kutofanya kazi sawa sawa kila ninapofunga na kulifungua kuzuia takataka.

“Lakini nanawa , natumia sabuni...”

Mganga akaniambia, sabuni haisafishi kila kitu.

Nikaelekezwa kutumia maji maalumu ya kusafisha kope za macho.

Nilifanyiwa opereshini kuondoa kile kivimbe.

Miji yote ya Kizungu huuza maji haya yanayoitwa Oprex au Eyewash. Nikiwa likizo Tanzania miaka kumi iliyopita niliwahi kuyanunua. Lakini baada ya kuyatumia kirefu nikavimba tena. Wakati huo naishi London. Mganga akaniuliza nasafishaje macho?

“Natumia Eyewash...”

Mganga : “Aghali sana na kuna bora zaidi yake.”

Akanielekeza niwe natumia unga wa magadi. Kwa Kimombo, Bicarbonate of Soda. Si wa aghali. Huuzwa kimkebe kidogo. Unga huu wa Soda una zaidi ya matumizi hamsini. Mbali ya kupika ni kusafisha. Unaweza kutumia miguuni, hasa kama vidole vyako hunuka. Ukishaoga unapaka na kumwaga mwaga katikati ya vidole.

Au makwapani, kama unakikwapa, baada ya kuoga.

Macho, je?.

Unauweka kwenye kijiko au kisahani chenye maji baridi masafi yaliyochemshwa. Unatumia kipamba cha kusafishia masikio. Lengo ni kusafisha kope za macho tu. Unaweza pia kuchovya kwa pamba kusafishia uso mzima.

Jambo la pili ni meno. Wengi tunapiga mswaki mara mbili kwa siku. Kawaida unatakiwa upige kila unapokula chakula – hasa vyakula vya sukari na chumvi nyingi.

Na kupiga mswaki si tu kusafisha meno. Yabidi pia uondoe mabaki ya chakula kati kati ya meno. Mabaki haya huondoka kwa uzi unaouzwa maduka ya dawa. Unaitwa Dental floss, au floss kwa kifupi. Sina hakika kama waganga wa meno Tanzania wanasisitiza matumizi ya ‘floss’, lakini kwa uzunguni, ni muhimu sana.

Uzi huu unauzwa kila duka la chakula na masoko bomba. Kuna ‘floss’ nzito (kwa wenye meno yenye nafasi, kama mwanya) na mwembamba kwa wenye meno zisizo na nyufa.

Jingine ni ulimi. Wahindi wameboea katika utamaduni huu na huuza kichuma (tongue lleaner) kilichojipinda. Lakini mimi binafsi hutumia kijiko kikubwa kuukwangua ulimi. Utashangaa namna ndimi zetu zinavyobeba utoko na ukoko wa taka.

Wengi tunadhani ukipiga mswaki juu ya ulimi imetosha. Sivyo.

Tovuti : www.freddymacha.com

Advertisement