Namna ya kumsaidia mtoto kukabiliana na msiba

Muktasari:

Watoto wadogo wanaweza wasitambue kuwa kifo ni milele. Wanaweza kutegemea kuwa marehemu atarudi hata kama utajitahidi kwa namna gani kuwaelewesha kuwa hatorudi. Watoto wanaweza kuuliza maswali hayohayo mara kwa mara, kutaka kujua kuhusu ugonjwa fulani kwa undani zaidi, kujua nini kinatokea kwenye mwili na roho na vinaenda wapi na wengine wataongeza ukaribu na baadhi ya wanafamilia kwa kuogopa kuwa kifo kitawachukua.

Watoto na watu wazima hukabiliana na hali ya kuondokewa na wapendwa wao kwa njia tofauti. Mapokeo ya mtoto hutegemea umri, kiasi gani anaelewa na kiasi gani watu wa karibu nae wanajali.

Watoto wadogo wanaweza wasitambue kuwa kifo ni milele. Wanaweza kutegemea kuwa marehemu atarudi hata kama utajitahidi kwa namna gani kuwaelewesha kuwa hatorudi. Watoto wanaweza kuuliza maswali hayohayo mara kwa mara, kutaka kujua kuhusu ugonjwa fulani kwa undani zaidi, kujua nini kinatokea kwenye mwili na roho na vinaenda wapi na wengine wataongeza ukaribu na baadhi ya wanafamilia kwa kuogopa kuwa kifo kitawachukua.

Baada ya kuondokewa na mpendwa wao, baadhi ya watoto hupenda maisha yaendelee kuwa kama zamani; wacheke, wacheze na kufurahia maisha kama kawaida. Watoto wengine hupata ugumu wa kulia na wengine watalia kila mara au ghafla tu. Wengine watakuwa na hasira, watakuwa wagomvi kwa wenzao, na wengine watakuwa na huzuni hata kushindwa kupata usingizi.

Mara nyingi ni vigumu kwa watoto kuelezea hisia zao wakifikwa na msiba na wengine hujihisi kuwa chanzo cha kifo cha mpendwa wao. Watoto wanaohisi hivi ni vizuri wakaelezwa kuwa hawahusiki na kifo na hakuna haja ya kuwa na wasiwasi kuwa ndugu mwingine wa karibu atakufa. Ni vizuri kuwasaidia watoto kuongea kuhusu hisia zao ingawa pia watoto wengi hawapendi mazungmzo marefu. Cha kufanya ni kuwahakikishia kuwa upo kwa ajili yao muda wowote na wakati wowote wakihisi huzuni na upweke hasa nyakati za usiku.

Mapendekezo yafuatayo yanaweza kuwasaidia watoto kukabiliana na nyakati za huzuni.

Kuwa muwazi na mueleze kile kilichotokea kwa njia rahisi anayoweza kuelewa. Tumia maneno kama ‘kifo’ na ‘amefariki’, usifunike kwa kumwambia amelala, amesafiri, au namna nyingine yoyote. Mtoto akiuliza maswali yajibu kama unaweza na kama hauwezi, usidanganye au kutunga hadithi ya uongo.

Kubaliana na hisia za mtoto. Mtoto anapofikwa na msiba anaweza akawa na mwenendo wa tabia ambao haukuitegemea, hivyo ni muhimu uwe umejiandaa. Usikasirike mtoto anapokuwa na hasira juu ya kifo cha mpendwa wake au anapoonekana kutojali juu ya kifo cha mzazi au mpendwa wake. Ni vizuri pia kumruhusu mtoto kulia na si kumkaripia badala yake muoneshe upendo na kumbebeleza.

Jaribu kurudisha mazingira katika hali yake ya kawaida kwa haraka iwezekanavyo. Hii itategemea nani anaishi na mtoto kwa wakati huo. Mtoto atajisikia kuwa yuko salama kama ratiba haitabadilika hivyo jitahidi kufuata zile ratiba za kila siku ktika suala la muda wa kula, kucheza, kuoga na kulala.

Ongea kuhusu mpendwa aliyefariki. Jaribu kukumbuka nyakati za furaha mlizokuwa nazo ila usimlazimishe mtoto kuongea habari hizo kama hataki.

Mruhusu mtoto kutumia kitu chochote cha mpendwa aliyefariki zikiwemo nguo au kitu chochote mzazi alichopenda kutumia mara kwa mara. Hii humkumbusha mtoto maisha yao ya pamoja, kusahau majonzi na kurudi katika hali ya kawaida.

Msimulie au msomee hadithi za kwenye Biblia au Koran, au hadithi za wanyama zinazohusu kifo. Hadithi hizi humfanya mtoto aone kuwa kifo ni jambo la kwaida katika maisha na kumfanya awe muwazi kuuliza maswali na hata kusimulia kumbukumbu nzuri alizonazo, pia mruhusu mtoto kuhudhuria mazishi au taratibu nyingine za kifamilia.

Kuwa mvumilivu. Kumbuka maumivu huchukua muda kuisha. Jaribu kumsaidia na hata kujibu maswali hata kama atauliza kwa kuyarudia rudia.