ELIMU NA MALEZI : Namna ya kutambua na kukuza kipaji cha mtoto -2

Muktasari:

  • Kufurahia kile unachokifanya kazini au katika shughuli nyinginezo, kunategemeana na namna unavyotumia vipawa ulivyozaliwa navyo.
  • Pia, tulibainisha umuhimu wa wazazi kufanya kazi ya kuwasaidia watoto kubaini vipaji vyao mapema. Kufanya hivyo ni kujaza pengo la mitalaa yetu, ambayo kimsingi haifanyi mengi katika kuibua na kukuza vipaji vya watoto.

Katika makala yaliyopita tuliona mambo yanayoweza kujenga kipaji cha mtu na uhusiano wa kipaji na mafanikio katika maisha.

Kufurahia kile unachokifanya kazini au katika shughuli nyinginezo, kunategemeana na namna unavyotumia vipawa ulivyozaliwa navyo.

Pia, tulibainisha umuhimu wa wazazi kufanya kazi ya kuwasaidia watoto kubaini vipaji vyao mapema. Kufanya hivyo ni kujaza pengo la mitalaa yetu, ambayo kimsingi haifanyi mengi katika kuibua na kukuza vipaji vya watoto.

Katika makala haya tunaangalia mbinu unazoweza kutumia kama mzazi kubaini na kukuza kipaji cha mwanao.

Kuwa karibu na mwanao

Huwezi kumfahamu mtoto vizuri kama huna muda naye. Unapotumia muda wa kutosha na mtoto, utaweza kufahamu mambo yake mengi.

Uhusiano wa karibu utakupa nafasi ya kufanya mazungumzo, kucheza na hata kuona mambo ya msingi anayoyapa uzito. Huwezi hufahamu kitu kinachomvutia mwanao bila kujenga ukaribu naye.

Unapojenga ukaribu na mtoto, ni vyema kumpa nafasi ya kusema na kufanya yale anayoyapenda bila hofu ya kukosolewa. Mtoto anapokosolewa anajenga sura anayojua ndiyo inatarajiwa na mzazi. Ni vigumu kumfahamu mtoto wa namna hii anayevaa sura isiyo yake.

Jenga mazingira rafiki kujifunza

Mazingira yana mchango mkubwa katika kukuza vipaji. Hakikisha mtoto anapata fursa ya kujaribu uwezo wa namna tofauti. Kupitia kujaribu hiki na kile, atapata kile kinachomtambulisha.

Katika kujenga mazingira mpe mtoto vifaa anavyovihitaji. Tangu akiwa mdogo wekeza katika vifaa vya kukuza uwezo wowote alionao. Mpe mpira, rangi, vifaa vya kucheza muziki, vitabu na vifaa kama hivyo. Unapofanya hivyo bila kupendelea uwezo fulani, ni rahisi mtoto kuonyesha wapi uwezo wake unaelemea zaidi.

Changamoto hapa ni mzazi kujaribu kuweka mazingira yanayosadifu kile anachokipenda yeye. Kwa mfano, mzazi anayependa muziki, anaweka mazingira yanayohamasisha muziki pekee na sio uwezo mwingine. Kufanya hivi hakuwezi kumsaidia mtoto kugundua kipaji chake. Kutamshawishi mtoto kuwa kile asicho.

Ikiwa unatamani kugundua kipaji cha mwanao, yafanye mazingira yampe fursa ya kutumia uwezo wa aina mbalimbali. Weka mazingira yanayohimiza maeneo yote kama vile michezo, sayansi, sanaa, lugha, uhusiano, ufundi na mengineyo.

Mwonyeshe mifano ya vipaji tofauti

Mtoto ana tabia ya kuiga mambo anayoyaona katika mazingira yake. Anaweza kuvutiwa kuwa daktari kwa sababu hao ndio watu anawaowasikia katika mazingira yake. Lakini kama ungeweza kumfahamisha vipawa mbalimbali, angegundua eneo jingine tofauti.

Ili kuhakikisha kuwa mtoto haishii kuiga yale anayoyaona katika mazingira yake, unahitaji kupanua uelewa wake kwa kumpa mifano halisi ya vipaji ambavyo pengine havifahamu. Tafuta watu maarufu waliofanikiwa katika maeneo yao na mfahamishe mwanao awaelewe.

Kwa mfano, unaweza kumsimulia mtoto habari za wanasayansi maarufu na kazi walizozifanya. Mtafutie filamu na vitabu vinavyoelezea namna wanasayansi hao wanavyokumbukwa kwa mafanikio yao. Mpeleke kwenye maeneo halisi anakoweza kushuhudia namna wanasayansi hao wanavyofanya kazi zao.

Fanya hivyo kwa fani mbalimbali. Unapomfahamisha aina mbalimbali za vipaji unalenga kupima hamasa ya mtoto kujitambulisha na watu wanaomgusa zaidi. Kwa kuwa zoezi la kumfahamisha mtoto vipaji hivi halifanyiki kwa siku moja, mtoto anaweza kuonyesha mapenzi na watu wa aina fulani. Mtoto anaweza kuanza kuvutiwa na vipaji fulani zaidi kuliko vingine. Huo ndiyo mwanzo wa kubaini kipaji cha mtoto.

Tambua uwezo wake

Baada ya kumpa mtoto fursa ya kuchunguza mazingira yake, ni dhahiri ataanza kuonyesha uwezo fulani mahususi. Katika saikolojia, uwezo huu mahususi unaweza kuganywa katika makundi kadhaa.

Kundi la kwanza ni watoto wanaopenda vitu badala ya watu. Hawa wanatumia muda mrefu kushughulika na vifaa, wanafurahia kuharibu na kutengeneza. Pia, wanapenda ukimya, wanapenda kufuata utaratibu usiobadilika. Vipaji vyao viko katika ufundi na kufanya kazi na vitu.

Lakini wapo watoto wasio na muda na watu lakini hawana muda na vitu pia. Hawa muda mwingi wanautumia wakiwa pekee yao. Hawana mazungumzo mengi.

Hawa wanaweza kuwa na vipaji vya kuchambua mambo, kudadisi nadharia na utundu wa akili. Wanauliza maswali yanayofikirisha, ni wachunguzi, hawaamini mambo kirahisi. Hawa eneo lao ni sayansi.

Vilevile, wapo wenye mapenzi na sanaa. Hawa ni wabunifu, wanajua kuongea kitu kikaeleweka kwa maneno machache. Wanapenda uhuru wa kuumba mawazo ambayo wakati mwingine hayapo na ni wabunifu. Kipaji chao ni utunzi, uimbaji, utamaduni, uchoraji na ushairi.

Kundi la nne ni wapenda watu. Ni marafiki wazuri, wanapenda kufanya mambo yao kwa ushirikiano na wengine lakini hawana kawaida ya kuwatawala wengine. Kuwa pekee yao ni kama adhabu lakini wanapokuwa na wenzao hawajifikirii wenyewe. Wanaridhika kuwasaidia wengine kupata wanachokitaka. Kipaji chao ni kuwasaidia wengine.

Pia lipo kundi la watoto wanaopenda watu lakini wanakuwa rahisi kuonekana. Wanapokuwa na wenzao ni rahisi kusikilizwa kwa sababu ni waongeaji, wanajiamini kupindukia, wanapenda kusikika na kuelekeza. Hawa kipaji chao kiko kwenye uongozi, usimamizi na siasa.

Pia, wapo watoto wanaopenda michezo. Ingawa ni kweli katika umri fulani michezo ni hitaji la kila mtoto, watoto wa kundi hili wana kawaida ya kuonyesha uwezo usio wa kawaida katika ujuzi wa michezo inayohitaji uwezo maalumu wa matumizi ya viungo vya mwili.

Tafuta ushauri wa kitaalamu

Ni vizuri kuelewa kuwa tabia, mitazamo na utashi wa watoto hubadilika kadri wanavyokua. Kama tulivyosema, mtoto anaweza kuonyesha kuvutiwa na watu fulani kwa sababu za juujuu zisizodumu.

Ni vyema kutafuta msaada wa wataalamu wanaoweza kumchunguza mtoto kitaalamu kubaini kipaji chake halisi. Katika nchi yetu, msaada huu unaweza kutolewa na watu waliobobea kwenye masuala ya saikolojia na unasihi.