Sunday, June 18, 2017

Nani anamiliki ilani ya uchaguzi?

 

Tunaendelea na shamba darasa la siasa za Tanzania na utendaji kazi wa Serikali ya “Hapa kazi tu” ya Rais John Magufuli. Katika mwendelezo huu tunajaribu kujipa hekima ya Mfalme Suleiman na kama kuna mwana wa kumfananisha kumchinja, tunaomba mwenye mwana amwache aishi, atakaye achinjwe huyo siyo wake.

Kwa mfumo wa siasa za demokrasia ya vyama vingi ulivyo, kwetu, ni utaratibu wa kisheria kwa kila chama kuwa na misingi yake kinayoijenga, kuisimamia na kuiamini – ni ilani ya uchaguzi.

Hiyo ni imani wanayoipeleka kwa umma ili waaminiwe na kupewa ridhaa ya kuongoza kwa mujibu wa Katiba. Jambo moja la uhakika ni kuwa, kila chama huiamini ilani yake na hiyo ndiyo msingi wa kutafuta madaraka ya kushika dola.

Kwa mujibu wa Katiba ya nchi, ni sheria na utaratibu kwamba chama kitakapokuwa kimeshinda, ilani yake itakuwa imeshinda endapo kitafanikiwa kupata ushindi wa kutosha kuunda Serikali.

Katiba inatupa angalizo kuu, kwamba kushinda uchaguzi ni jambo moja na kuunda Serikali ni jambo jingine. Nitafafanua.

Ibara ya 51(1) na (2) zikisomwa pamoja na Ibara 33 na 34(1) zinaainisha mamlaka ya Rais, Serikali na utaratibu wa kuunda Serikali. Yaani Serikali itakuwa inaundwa pale Rais kwa mujibu wa Katiba anapomteua waziri mkuu, na waziri mkuu hatashika madaraka yake mpaka atakapokuwa ameapa mbele ya Rais kwa kiapo kinachohusika na kiti hicho.

Lakini pia, Katiba inaweka utaratibu kwamba mbunge aliyeteuliwa (kutoka miongoni mwa wabunge wa kuchaguliwa anayetokana na chama chenye wabunge wengi), hatashika madaraka hayo (ya waziri mkuu) mpaka kwanza uteuzi wake uwe umethibitishwa na Bunge kwa azimio litakaloungwa mkono na wabunge walio wengi (Ibara 51 (1-2).

Kimsingi kwa mujibu wa Katiba, chama chenye wabunge wengi ndicho kinaunda Serikali na kwa Tanzania tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa ni CCM imekuwa inashinda nafasi ya urais na kuunda Serikali.

Kuna ilani tofauti?

Wakati tunatafuta kujibu baadhi ya maswali ya jumla yanayotusumbia. Tumeeleza kwa kifupi hapo awali kwamba tunapokwenda katika uchaguzi kila chama huwa na ilani yake. Katika ilani ndimo kuna mambo ya msingi ambayo ni ushawishi kwa wananchi kukichagua.

Kwa bahati mbaya katika chaguzi zetu tunasimamisha wagombea ambao huonekana wanavinadi vyama vyao, kumbe ni kinyume chake. Na kwa jinsi hii wagombea ndiyo hushinda na kisha kupachikwa chama.

Kwa sababu ya ilani, chama ndicho hugombea na hushinda au kushindwa kisha humpachika mgombea.

Ilani inayoshinda ndiyo hutekelezwa nchi nzima. Tumekuwa na ugoigoi fulani kulielewa na kulielewesha hili kwa umma.

Hakuna ilani tofauti kwa maeneo tofauti kutokana na dhana tu ya ushindi wa vyama tofauti, hasa kwenye Serikali za mitaa (Halmashauri).

Tangu mwaka 1995 hadi 2015 ilani ya CCM ilishinda uchaguzi na ndiyo ilitekelezwa nchi nzima. Idadi ya wabunge na madiwani wa vyama vya upinzani dhidi ya CCM imekuwa inaongezeka kila uchaguzi na hata idadi ya halmashauri ambazo vyama vya upinzani vimeshinda imeongezeka. Hizi ni dalili njema za ukuaji wa demokrasia nchini na ni msingi tunaoujenga kwamba kwa Utanzania wetu, baada ya uchaguzi ni kufanya kazi ya waliotupa ridhaa.

Katika halmashauri zote ilani ya uchaguzi iliyoshinda ni ya CCM kwa matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2015. CCM ilishinda kiti cha urais na ndicho chama kilipata wabunge wengi na kwa misingi hiyo kikapata nafasi ya kuunda Serikali.

Serikali hiyo imeundwa kwa mujibu wa sheria, Katiba na kanuni. Na kwa mujibu wa sheria hizo na katiba, ilani ya CCM ndiyo mwongozo mkuu wa utendaji kazi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali za mitaa upande wa Bara na Zanzibar.

Tunaweka hivi ili ifahamike wazi kwamba, hata katika majimbo yaliyopo chini ya vyama vya upinzani kote wanatekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM.

Urahisi wa kuyaelewa haya upo katika mfumo wa utendaji kazi wa Serikali na uhusiano uliopo kati ya Serikali kuu na Serikali za mitaa. Serikali za mitaa hufanya kazi kwa utegemezi mkubwa wa Serikali kuu na Serikali kuu hutekeleza majukumu yake kupitia Serikali za mitaa. Hii maana yake ni kwamba chama chenye ilani iliyoshinda, kinayo mamlaka makuu kwa Serikali zote na hakuna ilani nyingine itakayotekelezwa zaidi ya hiyo.

Kuteua makada

Tunajaribu kujibu kwa wepesi hoja za kwa nini Rais aliteua makada wa chama kushika nyadhifa za ukuu wa mikoa na wilaya, makatibu wakuu wa wizara, wakurugenzi wa halmashauri na teuzi nyingine.

Ni jambo rahisi, kujielewesha kwamba ili kuweza kutekeleza kwa ufanisi ilani ya uchaguzi iliyoshinda wazo kuu ni kuteua maofisa wa kuisimamia, wanaoifahamu vyema, wanaoweza kuiishi na wanaoweza kuielezea huku wakiimiliki. Kinyume chake, Serikali hiyo itakuwa imeanza kujijengea mazingira ya kupotea kwa kushindwa kuhudumia wananchi (kwa mujibu wa Ibara ya 8(2) ya Katiba ya Tanzania.

Mmiliki wa ilani

Tunaweza kupata shida kuelekeza kwa ufasaha umiliki wa Ilani. Ieleweke leo kuwa tuna hatua tatu za maisha ya ilani. Hatua ya kwanza ni mchakato wa kuijenga ilani yenyewe na hatua hii ni ndefu sana. Hatua hii ndiyo hujenga sura na taswira halisi ya nini kitakuwa kipaumbele cha chama husika pindi uchaguzi mkuu ukifika.

Ikumbukwe madhumuni makuu ya vyama vya siasa ni kushinda chaguzi na kushika dola. Hatua ya kwanza huanza mara tu baada ya uchaguzi.

Hatua ya pili hutokea kwenye kuyanadi yale matamanio yetu kwenye maandishi, kuyaandika na kuyadurusu ili yawe halisi kwa ajili ya kuyatangaza. Hatua hii ni fupi, ngumu na yenye kila aina ya changamoto. Hii ni hatua ya kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu.

Katika hatua ya kwanza na ya pili, ilani za uchaguzi ni mali ya vyama vyenye ilani. Hairuhusiwi kunakiri na kuiga yaliyomo katika ilani ya chama kimoja na kuyatumia kwa chama kingine kwa minajili ile ile ya kushinda katika uchaguzi mkuu unaofuata.

Hatua ya tatu ni baada ya uchaguzi. Katika hatua hii, ilani zilizoshindwa zote zinafifia au kuzimia kabisa na kuiacha iliyoshinda itamalaki. Ilani iliyoshinda inaanza kutekelezwa kwa kuzingatia vipaumbele, na katika utekelezaji inaweza kuboreshhwa ingawa haibadilishwi.

Ikumbukwe utekelezaji wa ilani, ni msingi wa kujenga ilani ya uchaguzi ujao na ni wajibu wa kila chama kufuatilia kwa karibu utekelezaji na kwa vyama vilivyoshindwa kutafuta makosa kutokana na ilani.

Chama kilichoshinda hufuatilia utekelezaji wa Serikali ili kisije kuhukumiwa endapo ilani hiyo haitakekelzwa ipasavyo. Katika hatua hii, ilani iliyoshinda inamilikiwa na umma. Umma una wajibu wa kufuatilia na kukumbusha utekelezaji wa ahadi za Serikali iliyopo madarakani.

Katika kipindi cha 2015-2020 ilani inayotekelezwa ni ya CCM na ni wajibu wa Serikali kuwahudumia wananchi kwa mujibu wa ilani hiyo, maana hakuna pengine penye mwongozo mwingine.

Ikiwa kuna anayedhani kuisemea ilani itakuwa ni kukiuka matakwa ya kikatiba yanayozuia mtumishi wa umma kujihusisha na vyama vya siasa, atakuwa amejisahaulisha na kujipotosha au kuihujumu Serikali kwa makusudi.

Mama mjamzito huumia sana wakati wa kujifungua baada ya kulea mimba miezi tisa, lakini furaha ya kumuona mtoto huzidi yale maumivu makali ya uchungu wa uzazi.

Furaha hiyo haitakuwa na maana ikiwa mama huyu hatamlea vema mwanaye au ikiwa atamkabidhi katika mikono ya wahalifu watakaomharibu mwanaye. Mwenye masikio na asikie.

Mungu Ibariki Tanzania

Falesy Kibassa ni msomaji wa magazeti ya Mwananchi, mtafiti na mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa

Simu: +255716696265/baruapepe fmkibassa@gmail.com

-->