Ndoto ya Chiswanu kumiliki kiwanda cha viti vya walemavu

Erasto Chiswanu akionyesha kiti kinachotumia umeme, alichokitengeneza kwa ajili ya matumizi ya walemavu wa miguu. Picha na Asna Kaniki

Muktasari:

  • Kwa vijana waliomaliza elimu ya juu hawahitaji tena kuajiriwa kwani, ubunifu kwao ni ajira pekee.
  • Katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia ubunifu, unatajwa kama chachu ya watu hasa vijana katika kujipatia ajira.

Hivi sasa ubunifu ndiyo njia pekee inayoweza kumkomboa kijana aliyemaliza masomo yake.

Kwa vijana waliomaliza elimu ya juu hawahitaji tena kuajiriwa kwani, ubunifu kwao ni ajira pekee.

Katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia ubunifu, unatajwa kama chachu ya watu hasa vijana katika kujipatia ajira.

Erasto Chiswanu aliyemaliza masomo ya uhandisi wa umeme katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, (DIT) anasema ubunifu kwake ni ajira tosha.

Kijana huyu ameunda kiti cha walemavu kinachotumia umeme. Anasema kiti hicho hakihitaji kusukumwa bali hujisukuma chenyewe kwa kutumia mfumo huo wa umeme.

Anasema kiti hicho alichokitengenezwa mwaka huu, kimemgharimu kiasi cha Sh 2.7 milioni kuanzia maandalizi hadi kukamilika kwake.

Anasema lengo la kubuni kiti hicho ni baada ya kuona kuwa watu wenye ulemevu wanapata shida kutafuta msaada wa kusukuma kiti wanapohitaji kutembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Kiti hicho kinatumia betri na kina uwezo wa kutembea umbali wa kilometa tano hadi saba kwa saa.

“Kwa matumizi ya hapa mjini mgonjwa anaweza kukitumia kwa muda mrefu bila kuisha chaji, lakini hata kama kitatumika kwa umbali mrefu ikitokea kikazimika betri inaweza kuchajiwa tena na kuendelea kufanya kazi” anasema. Anasema ubunifu huo ambao kwake ulikuwa mgumu, umekuja baada ya kuona karibu kila kitu kimeshabuniwa, hivyo alitaka kuwa tofauti na wengine.

“Nilijiandaa mapema kuwa nitatengeneza kitu cha aina yake. Nilipokuwa mwaka wa tatu fikra zangu zililenga kubuni kiti hiki maalumu na cha kisasa kwa ajili ya walemavu” anasema na kuongeza’

“Kwanza nilifikiria kuhusu walemavu, wazee na wagonjwa wanavyoshindwa kutembea sehemu mbalimbali kwa kukosa kitu cha kumsaidia.”

Baada ya kupata wazo hilo, anasema alipeleka mapendekezo yake kwa mwalimu juu ya utengenezaji wa kiti hicho.

Kazi na jasho

Haikuwa kazi rahisi kwa Chiswanu kukamilisha kiti hicho, kwani anasema kila mara aliwaza kiti hicho kiwe katika mfumo upi.

“Mwaka jana Novemba, nilianza kuwaza, kwamba sawa kiti kitajiendesha kwa kutumia umeme, lakini wasiwasi wangu ni jinsi ya kukikamilisha, maana kiti hiki ndiyo mara ya kwanza kubuniwa hapa nchini vingine vinapatikana Afrika ya Kusini na India.

“Nilianza kufikiria kichwani ni namna gani hicho kiti kinaweza kutumika, nikawaza vifaa gani nitumie, kiwe cha aina gani, kiwe na muonekano gani” anasema.

Changamoto

Chiswanu anasema kama sio kujipa moyo na kuonyesha jitihada zake asingeweza kukamilisha mradi wake kwani hata walimu iliwachukua muda kuelewa alivyowapelekea pendekezo lake. Anasema changamoto kubwa aliyokumbana nayo ni mtaji.

“Vifaa vinauzwa kwa bei ghali na ndiyo maana vingine nimetumia vya kawaida kwa kuwa nilikosa mtaji,’’anasema.

Matatizo ya kiufundi nayo yalichangia kukwamisha umalizaji wa haraka wa kiti hicho, kwani anasema alilazimika kurudia mara nne hadi kukamilika.

Akatishwa tamaa

Chiswanu anasema changamoto nyingine aliyokumbana nayo ni baadhi ya wanafunzi wenzake kumkatisha tamaa.

“Wakati nahangaika, wanafunzi wenzangu walishauri niachane na hicho kiti kwani kitanigharimu kiasi kikubwa cha fedha. Mimi niliichukulia kama changamoto kwani nilitegemea wao waniunge mkono na kunitia moyo” anasema.

Kuhusu mafanikio, anasema: “Nimeweza kujulikana kupitia ubunifu wangu, hasa tunapokwenda katika maonyesho mbalimbali kila mtu amefurahia ubunifu wangu,”.

Matarajio

Chiswanu ana ndoto ya kuwa na kiwanda kikubwa, ili aweze kutengeneza viti vingi ambavyo atasambaza katika maeneo tofauti.

“Sio siri uhandisi upo kwenye damu na lengo langu ni kusaidia wasiojiweza, kwani wazee, wagonjwa na walemavu wanashindwa kutembea maeneo mbalimbali kwa kukosa mtu wa kusukuma viti vyao” anasema.

Kwake dhamira siyo kutengeneza viti hivyo, bali pia kutoa mafunzo kwa vijana wengine.

Wito kwa Serikali

Anatoa rai kwa Serikali kuwawezesha wanafunzi wabunifu, kwa kuwawezesha rasilimali fedha katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kiubunifu

“Mimi naamini endapo Serikali itatushika mkono kwa kutenga bajeti kwa ajili ya ubunifu tutafika mbali na vijana hatutohangaika kutafuta ajira baada ya masomo” anasema na kuongeza:

“Nchi nyingi zinafanya ubunifu na kwa kiasi kikubwa zinanufaika kwa ubunifu huo, hivyo ni jukumu la Serikali kuhakikisha kuwa nchi inasonga mbele kwa kutumia teknolojia mbalimbali kama hii niliyofanya.”