Ndoto ya ualimu ilivyopotea kwa Khalfani

Muktasari:

  • “ Nilikuwa napenda ualimu tangu mdogo, ningependa kufundisha sayansi,” anasema.

Pamoja na ulemavu wa macho alionao, hakuacha kuwa na ndoto ya kutaka kuwa mwalimu. Ni ndoto aliyokuwa nayo Khalfan Machaku, mkazi wa eneo la Songe Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga. Tangu utotoni alitaka kuwa mwalimu tena wa masomo ya sayansi.

“ Nilikuwa napenda ualimu tangu mdogo, ningependa kufundisha sayansi,” anasema.

Leo akiwa na umri uliojongea, anakiri kuwa ndoto hiyo ilishayeyuka. Khalfan hataki kusikia neno elimu na hata akipatikana wa kufadhili masomo, anasema hatokubali kusoma zaidi ya miaka mitatu.

“ Kwa sasa sitamani kusoma, muda umepita, kwa zamani nilitamani,”” anasema Khalfan ambaye jitihada za kujiendeleza zilikwama baada ya kukosa mtu wa kumuonyesha njia ya kujiendeleza.

Jitihada zake

Kipindi cha mwisho cha jitihada zake za kutaka kusoma anakumbuka kilikuwa miaka ya 1998,alipofuatwa na uongozi wa Serikali wilayani Korogwe kwa ajili ya kupatiwa nafasi ya kusoma Tanga Mjini.

Anasema kilichomkosesha kupata nafasi hiyo ni uwezo mdogo wa kifedha, kwa kuwa alitakiwa atoe anachokitaja kama ‘ kitu chochote’ ili apate fursa hiyo.

“ Niliitwa nikahojiwa wakasema watanitafuta, muda ulipofika hawakunitafuta, nikasikia nafasi zile zimejaa,” anasema na kuongeza:

“ Ilikuwa Serikali iliyokuwa ikitafuta walemavu na kwa Korogwe, aliyekuja alikuwa mkuu wa wilaya mwenyewe.

Pengine fursa hiyo ingebadilisha mwelekeo wa maisha aliyonayo sasa, maisha ya utegemezi kutoka kwa wengine.

Walemavu Kilindi

Khalfan anawakilisha watu wenye ulemavu katika Wilaya ya Kilindi, wanaokosa fursa ya elimu kwa kuwa wilaya haina shule kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa kutoona.

Sio Kilindi pekee, karibu wilaya zote mkoani Tanga hazina shule maalumu kwa ajili ya walemavu wa macho. Shule pekee ipo Tanga Mjini. Hali hii bila shaka inapeperusha ndoto za walemavu wengu akiwamo Khalfan, ambaye kama angebahatika kusoma, pengine leo angekuwa mwalimu.

Maisha yake

Kwa sasa Khalfan anajishughulisha na udalali wa mazao, kazi anayosema angalau inampatia fedha za kujikimu kimaisha.

Kinachomuuma ni kuwa akiwa Kilindi, hajawahi kufuatwa na kiongozi hata mmoja kujua mustakabali wa maisha yake.

“ Nikikutana na kiongozi yeyote kwa mfano mkuu wa wilaya au mkurugenzi wa halmashauri, nitamwambia anijengee nyumba. Jambo la pili, aniwezeshe kupata mtaji wa biashara.Naweza kufanya biashara za aina nyingi.” anaeleza.

Wito kwa Serikali

Khalfan anaisihi Serikali kuwa karibu na watu wenye ulemavu na kuwaendeleza.

“ Kwa wale ambao hawajasoma, Serikali iwasaidie kimaisha kwa namna inavyoweza,” anaeleza.

Pamoja na jitihada mbalimbali za Serikali za kuhakikisha watu wenye ulemavu wananufaika na fursa za kielimu, changamoto za uchache wa shule kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu haina budi kufanyiwa kazi.

Ni udhaifu mkubwa kuona Mkoa mkubwa kama Tanga ukiwa na shule moja inayohudumia watoto wenye ulemavu wa macho. Hadithi ya Khalfan leo ingeweza kuwa nyingine kama angepata fursa ya kusoma ndani ya wilaya anamoishi.