Ndugai ni Solon mpya katika Bunge la Tanzania?

Spika wa Bunge, Job Ndugai

Muktasari:

Solon aliunda chombo ambacho kiliitwa Bunge la Wananchi, kikaitwa Ekklesia, yaani Bunge la Waathens (Athenian Assembly).

Tangu zama za kale, wakati jamii zilikuwa makabila, Ugiriki ya Karne tano kabla ya ujio wa kalenda, alikuwapo mtawala aliyeitwa Solon ambaye alitaka kuona mawazo ya wananchi yanaheshimiwa na utawala.

Solon aliunda chombo ambacho kiliitwa Bunge la Wananchi, kikaitwa Ekklesia, yaani Bunge la Waathens (Athenian Assembly).      

Ekklesia iliwekewa utaratibu wa wananchi bila kujali hali zao za kimaisha, matajiri na maskini, walishiriki katika Bunge hilo na kuamua masuala yote yaliyohusu jamii yao ya Athens.

Fundisho ambalo unaweza kulipata kupitia kwa Solon ni kuwa demokrasia ni wito ndani ya mtu. Ndiyo maana wapo watawala hupenda kuongoza kidemokrasia kwa sababu huo ni wito ndani yao.

Watawala wengine huongoza kidemokrasia kwa kulazimishwa na Katiba pamoja sheria za nchi, wakati wapo ambao huamua hata kuvunja sheria na kusigina Katiba ili kuyafunga madirisha yenye kuingiza mwanga wa demokrasia katika nchi kisha kuruhusu giza la udikteta lishamiri.

Solon bila kuwapo na sheria zenye kutaka ushirika wa wananchi kwenye utawala wake, yeye mwenyewe aliona hawezi kuongoza jamii ya Waathens peke yake, akataka maoni ya wengi yawe yanaamua kuhusu jamii yao.

Wakati watawala wengine hulazimisha hata kuvunja Katiba ili watawale peke yao kidikteta, Solon aliweka mwanzo mpya wa ushirika wa wananchi katika kuongoza Serikali yake. Waathens walijadili, wakapingana kisha wengi wakashinda kuhusu uamuzi mbalimbali wa jamii yao.

Solon hakuamua kuiingiza Athens vitani mpaka Ekklesia ilipokaa, kujadili na kupiga kura ya pamoja. Ekklesia ilichagua mahakimu wa mahakama zao (Areopagus) na kumuidhinisha kiongozi wa jeshi lao (Strategoi) pamoja na masuala mengine yote.

Hivyo, Solon ni alama ya demokrasia kwenye jamii yoyote, vilevile ni mfano wa mtawala mwenye nidhamu juu ya uhuru wa maoni ya watu. Solon ni kielelezo cha uongozi shirikishi, kwamba vema wananchi waonekane wakishiriki katika kujadili na kuamua masuala muhimu ya nchi yao.

Ndugai ni Solon?

Solon aliweka misingi ya utu, uhuru na demokrasia, kwamba kila mtu kwenye jamii ya Athens aliheshimiwa utu wake, alikuwa huru kutoa mawazo yake bila kubughudhiwa kisha mawazo ya wengi yalipita kwa njia ya kura.

Kipindi cha Solon utaratibu wake alitaka kila mwanaume aliyevuka hatua ya utoto, apate mafunzo ya kijeshi kwa miaka miwili kisha moja kwa moja alipata sifa ya kuwa mjumbe wa Ekklesia.

Wanaume hao walitakiwa kuwasilisha ndani ya Ekklsia mawazo yao, vilevile ya dada na mama zao, na kwa waliooa waliwatolea maoni pia wake zao. Hivyo ndivyo Solon aliweza kusimika misingi ya kidemokrasia kwenye utawala.

Baada ya hapo Waathens waliandika Katiba yao kwa kufuata utaratibu huo ulioanzishwa na Solon, kisha watu wakaanza kujifunza utamaduni huo wa kuheshimu mawazo ya wananchi kabla ya mfumo wa uwakilishi kuundwa na kupewa nafasi.

Mfumo huo wa uwakilishi ndio ambao umeenea duniani, maana haiwezekani nchi iwe na Bunge lenye wajumbe ambao ni watu wote kwenye nchi wenye sifa ya umri wa utu uzima.

Hilo Bunge litakuwa na ukubwa gani la kumchukua kila mtu mzima kwenye nchi? Inatakiwa pia wakati Bunge likiendelea, shughuli nyingine za uzalishaji mali ziendelee kwa ajili ya maendeleo ya nchi. Hivyo uwakilishi ni muhimu.

Tanzania pia mfumo ni huo, lipo Bunge ambacho ni chombo kinachobeba tafsiri ya mawazo ya kila mwananchi. Ushiriki wa wananchi kwenye Bunge ni kwa sababu wao kupitia majimbo (wilaya zao za uchaguzi), humchagua mwakilishi wao (mbunge) na kumtuma akawasemee bungeni.

Spika wa Bunge, Job Ndugai ndiye kiongozi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ikiwa kiongozi wa Bunge anaamua kuweka utaratibu mzuri kwa wabunge wake anaowaongoza ili wawasemee wananchi wanaowawakilisha bila kubagua, hiyo ndiyo njia ya kumuenzi Solon.

Ndugai kila mara

Pamoja na Ndugai kueleza wabunge wasikamatwe bila kupewa taarifa, alionya pia kuwa nchi ikiendeshwa kibabe kutatokea uharibifu. Alitaka kuwapo maelewano badala ya Bunge na Serikali kuonyeshana ubabe, jambo ambalo alisema litaharibu nchi.

Ubora huo wa Ndugai ulijionyesha tangu Mkutano wa Nne wa Bunge. Ndugai hakuwapo bungeni katika mkutano wa tatu ambao ulikuwa mkutano mrefu wa Bunge la Bajeti ya mwaka 2016/2017.

Mkutano wote wa tatu Ndugai alikuwa kwenye matibabu nchini India, hivyo kiongozi mkuu wa Bunge alibaki Naibu Spika, Dk Tulia Ackson ambaye misimamo yake iliwafanya wabunge wa upinzani kugomea vikao karibu vyote.

Wapinzani walisema Tulia alikuwa akiwaburuza, kwa hiyo wakaweka msimamo wa kutokaa bungeni kila alipoongoza vikao vya Bunge. Naye Tulia akakalia kiti kwenye vikao vyote. Hakuumwa wala kupata udhuru.

Kauli bora ya Ndugai aliyoitoa baada ya kurejea nchini kutoka kwenye matibabu ni kuzungumza na wapinzani, kisha alipokuwa anafungua Mkutano wa Nne wa Bunge, Septemba, mwaka jana, Ndugai alisema anataka Bunge moja.

Ndugai alisema, Rais wa sasa wa Marekani ambaye wakati huo alikuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Republican, Donald Trump ana msemo wake “Naweza” na Rais wa 44 wa nchi hiyo, Barack Obama husema “Ndiyo Tunaweza.” Ndugai akasema chaguo lake ni msemo wa Obama kwa sababu anataka umoja.

Umahiri wa Ndugai katika kuwaunganisha wabunge ndio ambao unanifanya nimwone kama mpenda sauti ya kila mmoja bila kubagua kama alivyokuwa Solon. Watanzania wanahitaji Bunge moja lenye nguvu, siyo kugawanyika na kubeba upande kisha wachache kusiginwa kama wasio na haki ya uwakilishi.

Luqman Maloto ni mwandishi wa habari, mchambuzi na mshauri wa masuala ya kijamii, siasa na sanaa. Ni mmiliki wa tovuti ya Maandishi Genius inayopatikana kwa anwani ya mtandao www.luqmanmaloto.com