Neeke anavyowaza makubwa mpira wa wavu

Monday October 23 2017

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

Kuna kundi kubwa la vijana wanaochipukia kwa kasi mpira wa wavu, David Neeke amekuwa akizungumzwa na wadau wa mchezo huo unaokua kwa kasi.

Neeke ambaye anaichezea Jeshi Stars, alifanya vizuri kwenye mashindano ya Nyerere Cup 2017 kwa kuiwezesha timu yake kushika nafasi ya pili baada ya kupoteza kwenye mchezo wa fainali dhidi ya APR ya Rwanda.

Chipukizi huyo amezungumza na Spoti Mikiki akisema alianza kuucheza mchezo huo tangu akiwa shule ya msingi kwenye michezo ya Umitashumta mwaka 2007.

“Kutokana na kuona kaka yangu Bulugu Neeke anacheza nikazidi kushawishika kuupenda mchezo ndio nikaamua kuanza kujifunza lakini nisingeweza mwenyewe nilienda kwa kocha, Safari Yabunika.

“Nikajifunza kwa Kocha huyo lakini yeye pia alishangaa kuona nina uwezo kubwa wa kucheza mchezo huo kwa hiyo hakupata shida kunifundisha na ninakumbuka alitamani sana niwe mtengenezaji (setter) lakini sikupenda.

“Nilipenda kucheza kama mshambuliaji, tuligombana kwa suala hilo lakini baadaye aliona ninaweza kucheza nafasi hiyo ndipo akaniamini.

“Uwezo wangu ulinisababisha kuchaguliwa kwenye timu ya Shule za Sekondari kwa ajili ya michezo ya Umisseta, Kanda ya Ziwa ilikuwa 2010,” anasema Neeke.

“Baada ya kumaliza kidato cha nne Neeke alipata nafasi ya kuanza kufanya mazoezi na timu ya Jeshi Stars na ndipo ulipokuwa mwanzo wa safari ya kutoka Mwanza na kuja Dar es Salaam.

“Nilifanya nao mazoezi kwa kipindi fulani na ukafika muda wa kusajiliwa, changamoto ilikuwa kwenye kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara, bidii ya mazoezi ilifanya nipate nafasi huku nikiwa mchezaji mdogo kuliko wote.

“ Ninapenda kumshukuru kocha wangu, Lameck Mashindano na wachezaji wote wa Jeshi Stars kwa ushauri na sapoti yao kwangu, pia ninawashukuru Mama na Baba wamekuwa mashabiki wangu namba moja wakati wote,” anasema kinda huyo.

Advertisement