Nguzo za umeme kwenye mbuga za wanyama hatari

Muktasari:

  • Na hapa ni lazima tuzingatie jambo moja muhimu. Maendeleo tunayoyatamani hayana lengo la kumfurahisha mtu mmoja au kikundi cha watu. Ni maendeleo ya taifa letu, maendeleo yetu sote na ya vizazi vijavyo. Ndio maana tutaendelea kusisitiza kwamba, kwenye suala la maendeleo ni muhimu kusikiliza kila wazo la kila Mtanzania ni muhimu, hata wale wanaoitwa wapinzani.

Ingawa kujadili mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge ni kitu kisichohitajika hivi sasa maana wakubwa tayari wamefanya uamuzi, kwetu sisi tunaofikiri Tanzania ni yetu sote na kila wazo linahitajika, tunafanya hivyo bila kusukumwa na ushabiki wa kisiasa, bali kuangalia ustawi mzima wa taifa letu. Siasa zinakuja na kupita, viongozi wanakuja na kupita, lakini taifa letu litadumu. Jukumu letu kubwa ni kuhakikisha tunakabidhi taifa lililo safi na salama kwa vizazi vijavyo.

Na hapa ni lazima tuzingatie jambo moja muhimu. Maendeleo tunayoyatamani hayana lengo la kumfurahisha mtu mmoja au kikundi cha watu. Ni maendeleo ya taifa letu, maendeleo yetu sote na ya vizazi vijavyo. Ndio maana tutaendelea kusisitiza kwamba, kwenye suala la maendeleo ni muhimu kusikiliza kila wazo la kila Mtanzania ni muhimu, hata wale wanaoitwa wapinzani.

Tunajua kwamba kila mtu ana mapenzi yake na kila mtu angepata madaraka ya kuliongoza taifa letu, angependa kutekeleza mapenzi yake. Mataifa yaliyoendelea kwa kuona hatari hii ya kila mtu kutaka kutekeleza mapenzi yake, waliamua kutunga sheria na taratibu za kuwaongoza. Walitengeneza Katiba ya kuwaongoza. Na wanaheshimu sheria hizo na taratibu.

Kwa vile na sisi tunalilia maendeleo. Na tunaendelea kujiaminisha kwamba maendeleo hayana siasa wala vyama, basi tukubali kuuimarisha wimbo huu wa Maendeleo hayana siasa. Tukubali kuonyesha jambo hili kwa matendo na hatua ya kwanza kabisa ni kuendeleza mchakato wa Katiba iliyotokana na mawazo ya Watanzania wote.

Tunapoona ujenzi wa kufua umeme unaanza bila kuzingatia taratibu na sheria za kutunza mapori ya akiba na vivutio ya utalii, na kukaa kimya ni dalili za unafiki na ishara za kutolipenda taifa letu la Tanzania. CCM, wanasema “Nitasema ukweli daima.” mbona sasa wanakaa kimya kwa hatua hii ya kupitisha nguzo za umeme kwenye mbuga za wanyama?

Wanaogopa kuitwa wapinzani na wasaliti wa chama? Usaliti mkubwa ni kuogopa kusema ukweli, ni kuogopa kuitetea na kuilinda Tanzania. Ni lazima tukumbuke kwamba hata wapinzani ni Watanzania na wala si Warundi au Waganda. Kwa pamoja tutalijenga taifa letu. Tuseme ukweli na tuusimamie.

Majuma mawili yaliyopita katika moja ya taarifa yake ya habari, ITV ilionyesha ujenzi wa nguzo za umeme kuelekea Stiegler’s Gorge katika mbuga ya pori la akiba la Selous.

Taarifa hiyo ya habari pia ilimuonyesha Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani akiisisitizia Tanesco haja ya kumaliza kazi hiyo haraka kadiri iwezekanavyo ili kumruhusu mkandarasi atakayejenga bwawa la maji la kusukuma mitambo ya kufulia maji hapo Stiegler’s Gorge aweze kutumia nishati hiyo katika shughuli zake za ujenzi.

Ni wazi sasa kuwa Serikali imepania kutimiza azma yake ya kujenga mradi huo na hivyo kupuuza wito ambao umekuwa ukitolewa na wana mazingira juu ya hatari ya mradi huo kwa mazingira ya pori hilo la akiba la Selous.

Sisi kama waandishi au wananchi hatuna kabisa ubavu wa kuipinga Serikali na hasa ikiamua kufanya inachotaka na kupuuza ushauri. Wajibu wetu ni kusimama na kusema ukweli. Wajibu wetu ni kutoa mawazo yetu. Walatini, wanasema kilichoandikwa kimeandikwa. Kama hakisomwi leo, kitasomwa kesho na vizazi vijavyo. Sasa hivi kuna utamaduni wa kuitwa msaliti au mpinzani, ukitoa mawazo tofauti. Huu si utamaduni wa kulijenga taifa letu, bali wa kulibomoa. Kuamini kwamba watu zaidi ya milioni 50, wanaweza kuwa na wazo moja kwa wakati mmoja, ni kujidanganya na kupuuza nguvu za Mungu, ambaye anaumba watu wenye mawazo tofauti na mapenzi tofauti.

Ndiyo maana baadhi yetu bado tunasimama na msimamo uleule na kusema kwamba hata kama Serikali imeamua, kama ilivyoonyesha, bado kuna haja ya kutekeleza kwanza utafiti wa athari za kimazingira (SEA) ambao huangalia athari ambazo zinaweza kuletwa na ujenzi wa bwawa kwa mradi husika.

Tunapoona nguzo zikielekezwa kwenye mbuga za wanyama, tunajiuliza kama SEA katika mradi huu ilifanyika. Ingefanyika jambo hili hatari kwa maisha ya wanyama lisingetekelezwa kwa njia hii ya kusimika nguzo, bali wangetumia njia nyingine ya kupitisha umeme chini ya ardhi badala ya kuanza kusimika nguzo ambazo tunataka tusitake athari yake itaonekana hata kabla ya kumaliza kulijenga bwawa lenyewe.

Uzuri wa SEA ni kwamba pia inaangalia wingi na upatikanaji wa maji kwa ajili ya bwana hilo, jambo ambalo husaidia wajenzi kujua ni aina ya mitambo watahitaji kufunga katika eneo hilo ili kupata kile wanachotaka kwa thamini ya pesa walizotumia. Tumeshuhudia mara nyingi kiwango cha maji kikienda chini kwenye miradi ya kufua umeme tuliyonayo sasa hivi. Ukame ambao chanzo chake ni tabia na utamaduni uliojengeka wa kutotunza mazingira na kuanzisha miradi mikubwa yenye kutumia maji mengi bila kufanya utafiti kwanza, limekuwa ni tatizo la kudumu. Je, kwa mradi huu mkubwa wa kufuata umeme tumefanya utafiti wa vyanzo vya maji kuelekea Selous?

Upande wa pili, SEA inasaidia kutoa athari ambazo zinaweza kutokea, hivyo hilo humsaidia mkandarasi kupunguza matokeo ya athari hizo kwa kufanya ujenzi ambao utazuia matatizo hayo.

Na SEA kwa kawaida inatakiwa kufanyika kabla ya kutekeleza chochote kile, kwa mfano, pamoja na ujenzi wa nguzo hizo za umeme badala yake kupitisha umeme chini ya ardhi kama ilivyofanywa katika mbuga za taifa za Serengeti na Ngorongoro.

Sheria za hifadhi za kimataifa zinakataza ujenzi wa nguzo za umeme katika mbuga za wanyamapori au mapori ya akiba yenye wanyama na badala yake zinashauri ujenzi wa umeme chini ya ardhi. Tanzania hatuwezi kuishi kisiwani, tunaishi kwenye ulimwengu huu wa utandawazi. Sheria za kimataifa, tunataka tusitake ni lazima tuzifuate. Roho nzuri na nia njema za kutaka kujenga bwawa la umeme kwa gharama zozote hizo haiwezi kuwa sababu tosha kuvunja sheria za kimataifa.

Inaweza kabisa Tanesco na wizara ya nishati zinafahamu hilo, lakini ziliamua kujenga nguzo ili kuepuka gharama. Ni wazi kuusafirisha umeme kupitia chini ya ardhi ni gharama ukilinganisha na kutumia nguzo. Kupanga ni kuchagua, kwa vile sisi tumechagua kujenga bwawa hilo, ni lazima tukubali kuzibeba gharama hizo.

Na kwa vile kwa upande mwingine tunataka kuboresha biashara ya utalii, jambo ambalo limeisukuma Serikali kununua ndege sita, tatu ndogo na tatu kubwa, basi si rahisi kufanikiwa katika biashara ya utalii hii kama tunaanzisha miradi ya kuangamiza utalii huu.

Kama ambavyo nimewahi kuandika katika moja ya makala zangu, ili kufanya manunuzi ya ndege kwa ajili ya Shirika la Ndege la Tanzania kuwa na tija, basi Serikali na vyombo vyake vinapaswa kuboresha vivutio vya utalii.

Hivi sasa biashara hiyo ya utalii inaliingizia taifa dola za Marekani bilioni mbili kwa mwaka. Lakini sehemu kubwa ya fedha hizo zinaingizwa na vivutio vya utalii vilivyoko kaskazini mwa nchi kama vile Serengeti, Tarangire, Ngorongoro na Mlima Kilimanjaro.

Ili kuboresha biashara ya utalii, Serikali na vyombo vyake inapaswa kuangalia vivutio vya utalii vilivyoko kusini mwa nchi kama vile pori la akiba la Selous, mbuga za taifa za Ruaha na Katavi.

Huwezi kuboresha vivutio hivi vya utalii vilivyoko kusini mwa nchi kwa kujenga nguzo za umeme kwenye hifadhi ya taifa au mapori ya akiba ya wanyamapori. Ikiwa unataka kupitisha umeme katika mapori hayo ya akiba au mbuga za wanyama, basi unafanya hivyo kwa kupitisha umeme huo chini ya ardhi ili kuwaachia wanyama pori maeneo ya juu ya ardhi kwa ajili ya kujidai.

Kwa kuwa Serikali imeamua kuendelea na ujenzi huo wa bwawa la maji katika Stiegler’s Gorge, basi ni vyema kuanza kwanza na utafiti wa SEA, utafiti ambao utaupa ujenzi wa bwawa hilo dira. Kwani bila kuwa na dira katika ujenzi huo, Serikali isije ikashangaa kama ikishindwa kupata tija kutokana na mradi huo.

Ni kweli ujenzi wa mradi huo unaweza kuleta megawati 2,100. Lakini swali ni je, zitapatikana kila siku na kwa kipindi chote cha mwaka? Uhakika wa kupata maji ya kutosha kwa ajili ya mradi huu tutaupata tu ikiwa tutafanya utafiti wa kina kupitia kwa SEA.

+255754 6331 22