Ni mambo ya fedha tu pale Msimbazi

Muktasari:

  • Kuna wale wanaocheza kila mmoja alilamba Sh300,000, waliovaa tu Sh200,000 na kuna wasiocheza wale nao walikula kilo na nusu.

Achana na asilimia za posho baada ya kushinda, achana na mishahara, unaambiwa Msimbazi wachezaji walikuwa wakiogelea noti ile mbaya msimu huu.

Kuna wale wanaocheza kila mmoja alilamba Sh300,000, waliovaa tu Sh200,000 na kuna wasiocheza wale nao walikula kilo na nusu.

Ndivyo unavyoweza kusema kwa jinsi nguvu ya fedha ilivyoipa jeuri Simba kuvunja unyonge wa kucheza misimu mitano mfululizo pasipo kunusa harufu ya ubingwa wa Ligi Kuu

Hakuna namna unayoweza kutenganisha mafanikio ambayo Simba imeyapata kwenye Ligi Kuu msimu huu kwa kutwaa ubingwa na nguvu kubwa ya kiuchumi waliyokuwa nayo kulinganisha na timu nyingine.

Simba ilikuwa imara kifedha jambo lililowasukuma wafanye usajili mzuri ulioipa kikosi chenye ubora msimu huu. Maandalizi ya kutosha kabla ya kuanza kwa msimu lakini pia timu ilipata huduma zote muhimu kama mishahara na posho, matibabu, kambi pamoja na usafiri kwa wakati na zinazokidhi viwango.

Kaimu Rais wa Simba katika moja ya mahojiano na Spoti Mikiki alisema wachezaji Simba hakuna mwenye deni na klabu.

Hata hivyo, fedha hizo ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, hazikuokotwa barabarani bali zimetokana na nguvu ya ushawishi ambayo uongozi wa klabu hiyo ulikuwa nao kwa wadhamini na wafadhili.

Makala hii inakuletea wanaoipa Simba jeuri ya fedha hata kuondolea wachezaji msongo wa mawazo.

MO Dewji

Nani asiyefahamu jinsi mfanyabiashara huyu mkubwa nchini ambaye pia ni shabiki na mwanachama wa Simba alivyorudisha heshima ya Simba msimu huu kutokana na jinsi alivyotoa fungu kubwa la fedha kuhakikisha timu hiyo inatikisa Ligi Kuu msimu huu?

Pia vyanzo vya mapato vya Simba kupitia udhamini na michango ya wadau havifiki hata asilimia 40 ya bajeti yote ambayo klabu hiyo iliweka msimu huu

Kiasi kikubwa cha fedha ambacho kilibakia ili Simba itimize bajeti yake ya Shilingi 4.7 bilioni ambayo ilitengwa kwa ajili ya msimu huu kilitolewa na Dewji ambaye alichangia zaidi ya asilimia 70 ya bajeti ya Simba.

SportPesa

Bajeti ya Simba msimu huu ilikuwa ni takribani Sh4.7 bilioni ambayo inajumuisha masuala kama usajili, kambi, mishahara na posho kwa wachezaji, maofisa wa benchi la ufundi pamoja na wafanyakazi wa klabu, huduma za matibabu pamoja na gharama za uendeshaji.

Sportpesa ni miongoni mwa wadau wakubwa waliofanikisha pakubwa Simba kutwaa ubingwa msimu huu.

Sportpesa imewapa Simba Sh 950 milioni kama fedha za udhamini ambazo ni sawa na asilimia 20 ya bajeti yote ya klabu hiyo msimu huu.

Bajeti ya usajili ya Simba msimu huu ni takribani Sh 1.2 bilioni hivyo fedha ambazo Sportpesa wanawapa ni kama zaidi ya asilimia 79 ya bajeti nzima.

Azam Media

Kampuni ya Azam Media nayo ni miongoni mwa wadau walioibeba Simba msimu huu kupitia fedha za udhamini ambazo wameipa kama malipo ya haki za matangazo ya televisheni.

Azam Media wameipatia Simba takribani Sh 499 milioni ambazo ni malipo ya haki za matangazo ya Ligi Kuu ambapo kila klabu inapewa kiasi cha Sh 184 milioni lakini pia Sh 315 milioni ambazo Simba wanapewa kwa ajili ya malipo ya kipindi cha televisheni cha Simba TV ambacho kinarushwa na Azam TV.

Vodacom

Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom ambayo ndio mdhamini mkuu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, yenyewe inaipatia Simba kiasi cha Sh 108 milioni ambazo pia kila timu ya Ligi Kuu hupatiwa.

Michango ya mashabiki

Pia Simba imekuwa ikipata fedha ambazo hukusanywa na mashabiki, wapenzi na wanachama wake kupitia makundi mbalimbali ya kwenye mitandao ya kijamii.

Fedha zinazotolewa na mashabiki wa Simba ni motisha ya Sh 10m na wahusika wakuu ni Simba Headquarters.