Ni muhimu wachezaji kupata mlo kamili

Muktasari:

Baadhi ya wanamichezo unaweza kuwakuta katika mitaani wakila kiholela katika sehemu za nyama choma, chipsi mayai, vijiwe vya supu na huku wakibugia soda au vinywaji vya kutengenezwa viwandani.


Tunaposema mlo kamili ni ule uliozingatia kanuni za wataalamu wa lishe ambao una makundi yote ya vyakula ikiwamo vyakula vya wanga, protini, mafuta, vitamini, madini na virutubisho mbalimbali.

Baadhi ya wanamichezo unaweza kuwakuta katika mitaani wakila kiholela katika sehemu za nyama choma, chipsi mayai, vijiwe vya supu na huku wakibugia soda au vinywaji vya kutengenezwa viwandani.

Ulaji wa vyakula hivi vinaweza kumweka katika hatari ya kunenepa au kuongezeka uzito uliokithiri kwani vyakula hivyo vina wanga kwa kiasi kikubwa, mafuta mengi na sukari nyingi.

Wataalamu wa lishe wanashauri wanamichezo kuepuka vyakula hivyo na badala yake mwanamichezo ajikite kutumia matunda au juisi za matunda freshi na mboga mboga na nafaka za mbegu.

Lishe ya wanamichezo huwa ni tofauti na ya mtu wa kawaida, wao wanatakiwa kula mlo kamili na huku akipangiwa ratiba na aina ya vyakula kwa kila mlo mkuu anaokula.

Katika ratiba hiyo, hutakiwa kula vyakula ambavyo vitamjenga mwili na kumpa nguvu pasipo kupata uzito uliokithiri au kumnenepesha.

Uzito au unene unaweza kumfanya kushindwa kuhimili vishindo vya mchezo anaoshiriki, kushuka kiwango au kutopanda kiwango.

Kwa kawaida angalau inatakiwa mlo wa mwanamichezo uwe na milo mikuu mitatu na milo mitatu ya katikati kabla ya mlo mkuu (snacks).

Vyakula vya katikati ya mlo ni kama vile matunda, juisi, mboga mbichi na vyakula jamii ya karanga.

Ikumbukwe kuwa michezo karibu yote inahitaji kuwa na nguvu, ukakamavu, mwili unaodumu na kustahimili mchezo kwa muda mrefu kwa kiwango kile kile.

Lakini mambo haya hayawezi kuja kirahisi hivi hivi bila kufuata na kushikamana na ushauri wa wataalamu wa afya, wataalamu wa mazoezi ya viungo na wataalamu maalumu wa lishe.

Wapo watalaamu ambao wao wamejikita tu katika lishe za wanamichezo ambao kitaalam hujulikana kama sports nutritionist lakini si vibaya katika maeneo yetu kuwatumia wataalam wa lishe waliopo.

Wapo wataalamu wa lishe katika idara za afya za halmashauri za miji na ambao hawajaajiriwa waliomaliza katika vyuo vikuu ikiwamo Chuo kikuu cha sokoine, ni vizuri klabu za michezo kuanza kuwatumia.

Wataalamu hawa ndio wanaoweza kukushauri aina ya vyakula vya kula na kukupangia ratiba maalum ya mlo kamili utakayoifuata na huku pia akikifuatilia mwenendo wa uzito wa wachezaji.

Mlo kamili unaofuata ratiba maalumu huku ukiandaliwa kwa kuzingatiwa kanuni za afya ni chachu ya kumpa mafanikio mwanamichezo.

Mwanamichezo atahitajika kuwa na nidhamu kukabiliana na kutekeleza jambo hili.

Haipendezi kwa mwanamichezo kula ovyo na wakati mwingine vyakula vya mafuta huzibisha mishipa na damu haisukumwi inavyotakiwa.