UCHAMBUZI: Ni vigumu kutenganisha uhuru wa habari na demokrasia

Muktasari:

Azimio hilo, kwa kiasi kikubwa lililenga kutambua uhuru na uwajibikaji kwa jamii kwa wahariri katika vyombo vya habari.

Machi mwaka 2011, Baraza la Habari Tanzania(MCT) lilipitisha azimio la Dar es Salaam juu ya uhuru wa uhariri na uwajibikaji.

Azimio hilo, kwa kiasi kikubwa lililenga kutambua uhuru na uwajibikaji kwa jamii kwa wahariri katika vyombo vya habari.

Pia, azimio hilo lilitaka wahariri na hata waandishi kutambua majukumu yao makubwa kijamii, kiuchumi na kisiasa ili kujenga vyombo vya habari huru, katika upatikanaji wa haki za watu na kuamua mambo yao yanayozingatia sheria bila kuingiliwa na chombo kingine.

Katika azimio hili, kuliwekwa msingi wa kutambua na kuheshimu haki za watu, uhuru wa kuamua mambo ya kisiasa, kiuchumi na kimaendeleo kwa kuzingatia sheria na mikataba ya kimataifa.

Baraza la habari lilijielekeza kufuatwa mkataba wa Afrika wa haki za binadamu wa mwaka 1982 na azimio la ulimwengu la haki za bindaamu la mwaka 1948.

Kwa ujumla azimio lilitosha kuwa msahafu kwa wahariri na wanahabari wengine katika utendaji kazi wao na kutambua wao wanawajibika kwa umma.

Wahariri walitakiwa kuachwa kuingiliwa katika uamuzi wao na vyombo vingine, wakiwapo wamiliki, taasisi nyingine na kupinga ushawishi na upendeleo ambao utadhoofisha uhuru wa uhariri.

Kwa ujumla azimio hili, linaendana na matakwa ya Katiba ya nchi Ibara ya 18(a) inachoeleza kila mtu ana uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake.

Katika Ibara hiyo ya 18 kifungu (d) pia kinaeleza kila mtu anahaki ya kupewa taarifa wakati wowote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii.

Azimio hili linaendana na Ibara ya 21(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, ambayo inaeleza kuwa kila raia anayo haki na uhuru kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo muhimu yanayomuhusu, maisha yake au yanayohusu taifa. Nimenukuu Azimio la Dar es Salaam juu ya uhuru wa uhariri na uwajibikaji, matamko ya kimataifa ya haki za binamu na Katiba ya nchi ili kuonyesha uhusiano wa uhuru wa habari na demokrasia.

Hivyo ni wazi unapokosekana uhuru wa habari inaweza kuathiri moja kwa moja demokrasia kwa kuwa mambo haya yanakwenda pamoja.

Katika siku za karibuni kumeibuka sintofahamu juu na masuala ya uhuru wa habari na demokrasia hasa kutokana na matamko ya kuwapa tahadhari wanahabari juu ya kuandika ama kuripoti habari zenye mlengo wa uchochezi.

Ni jambo jema kukumbushana juu ya wajibu wa kila raia na mwanahabari ili kuhakikisha wanajitenga na uchochezi wa aina yoyote ile na ili kulinda amani na utulivu katika taifa letu.

Hata hivyo, matamko kama haya ni vizuri kutanguliwa na dhamira njema ili kuondoa uwezekano wa kuwa na msukumo fulani wa masilahi ya kundi la watu wachache.

Kama ambavyo wamekuwa wakisema wasomi na wanasiasa kuwa Tanzania ni ya Watanzania wote hivyo katika kipindi hiki ni vyema matamko na sheria zilenge kulisaidia Taifa kusonga mbele na siyo kuleta migogoro.

Kwa hali ilivyo sasa wahariri na wanahabari wanapaswa kufanyakazi kwa umakini mkubwa zaidi ili kujilinda na dosari zozote ambazo zinaweza kutafsiriwa kama ni uchochezi.

Hata hivyo, mazingira kama haya yaweza yasiathiri wanahabari, lakini yanaweza kuleta shida kwa makundi mengine kutokana na kutiliwa shaka uhuru wao wa kujieleza na kutoa maoni.

Mussa Juma ni mwandishi wa gazeti hili anapatikana kwa baruapepe: [email protected] na simu 0754296503