Ni wakati mwingine wabunge kutetea michezo

Muktasari:

Waziri alilipa Bunge kazi ya kujadili mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/18 na mwongozo wa kuandaa mpango na bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/18.


Wiki iliyopita,Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango aliwasilisha bungeni mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/18 na mwongozo wa kuandaa mpango na bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/18.

Waziri alilipa Bunge kazi ya kujadili mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/18 na mwongozo wa kuandaa mpango na bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/18.

Katika mapendekezo hayo, Waziri aliainisha vipaumbele vya Serikali ambavyo ni makaa ya mawe Mchuchuma, Chuma Liganga, kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa Standard Gauge na matawi yake, kuboresha Shirika la Ndege la Tanzania, ujenzi wa mitambo ya kusindika gesi mkoani Lindi, uanzishwaji wa kanda maalum za kiuchumi, uanzishwaji wa kituo cha biashara cha Kurasini, kusomesha vijana katika stadi maalum (mafuta na gesi, uhandisi na huduma za afya), uanzishwaji wa mji wa kilimo Mkulazi, ununuzi na ukarabati wa meli kwenye maziwa makuu, ujenzi wa barabara za Kidahwe-Kanyani-Kasulu-Kibondo-Nyakanazi (km 310) na Masasi-Songea-Mbamba Bay (km 868.7).

Mapendekezo mengine ni uendelezaji wa maeneo ya viwanda vidogo (SIDO) katika mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na Arusha, uendelezaji wa eneo la viwanda TAMCO na EPZ/SEZ, bandari kavu (Pwani), mradi wa magadi soda (bonde la Engaruka), kufufua kiwanda cha General Tyre, mradi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi bandari ya Tanga na uwekezaji wa sekta binafsi katika viwanda hasa vile vinavyotumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini.

Waziri Mpango alitaja vipaumbele vingine ni elimu na mafunzo ya ufundi, afya na maji. Pia, katika mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji, Serikali itaendelea na miradi iliyoanza kutekelezwa katika mpango wa maendeleo wa taifa kwa mwaka 2016/17 na miradi itakayotekelezwa chini ya utaratibu wa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi.

Maeneo mengine yatakayozingatiwa katika mapendekezo ya vipaumbele hivyo ni kuhamishia shughuli za makao makuu ya Serikali Dodoma, mazingira na mabadiliko ya tabianchi, utawala bora na utawala wa sheria, miradi katika maeneo ya wanyamapori, misitu, ardhi, nyumba na makazi na madini.

Katika vipaumbele hivi utaona, Serikali haijataja kabisa miradi ya maendeleo ya michezo na utamaduni kuwa ni moja ya vipaumbele vyake katika mapendekezo iliyotoa kwa wabunge.

Sasa, ni wajibu wa wabunge kuhakikisha wanaingiza miradi ya maendeleo ya michezo na utamaduni katika mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/18 na mwongozo wa kuandaa mpango na bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/18.

Wabunge wanatakiwa kuelewa kwamba michezo nchini haiwezi kufanikiwa bila Serikali kusaidia. Serikali inatakiwa kusaidia kwa kutenga fedha za kutosha katika bajeti ya Wizara inayohusika na michezo kila mwaka kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya michezo. Miradi hiyo ni viwanja mbalimbali vya kawaida vya michezo tofauti mitaani, elimu kwa walimu wa michezo watakaofundisha michezo kwenye shule na mitaani na miradi mingine mingi ya michezo.

Serikali na wabunge wanatakiwa kuelewa kwamba michezo inatoa ajira pana, pia michezo ni biashara kubwa inayotoa kazi kwa watu mbalimbali.

Wabunge wanatakiwa pia kuhakikisha Serikali inaipa kipaumbele michezo kwani bila hivyo, michezo yetu itaendelea kupoteza dira, kwani hakuna mchezo ambao tunaweza kusema unaafadhali kimataifa, hakuna mbadala wa wachezaji, hakuna programu za vijana, yaani inafikia mahali kijana mwenye kipaji anakosa mahali pa kwenda kwa kuwa hakuna mifumo mizuri ya kuwaendeleza. Hatujachelewa, tusimamie hapa.