Nidhamu ya matumizi huchangia mafanikio kiuchumi

Muktasari:

Ili kuyafikia mafanikio ya kiuchumi, nidhamu katika matumizi ya fedha ndiyo nguzo pekee inayoweza kumfikisha mtafutaji yeyote kwenye kiwango cha mafanikio anachokitaka.

Habari za leo rafiki msomaji wa makala zangu za uchumi binafsi. Ni furaha yangu kujua unaendelea vyema na majukumu yako. Ni wakati mwingine tena tunaenda kujifunza pamoja juu ya mambo mbalimbali ili tuweze kuyafikia mafanikio tuliyojiwekea kila siku.

Ili kuyafikia mafanikio ya kiuchumi, nidhamu katika matumizi ya fedha ndiyo nguzo pekee inayoweza kumfikisha mtafutaji yeyote kwenye kiwango cha mafanikio anachokitaka.

Hili linawezekana hata kama kipato cha mtu huyo ni kidogo kiasi gani, atamudu kufikia malengo aliyojiwekea. Ipo mifano mingi kuthibitisha hili miongoni mwa jamii inayokuzunguka.

Bila shaka umewahi kuwaona watu wanaofanya kazi katika kampuni moja. Inawezekana wakwawa wanafanya kazi moja na kulipwa mshahara sawa lakini wakawa na mafanikio tofauti.

Mmoja wao anaweza kujenga nyumba ya kisasa ya kuishi yeye na familia yake huku wenzake wakiendelea kupanga. Unaweza kukuta mmoja huyo ana miradi yake nje ya kazi au anatafuta vyanzo vingine vya kumwingizia kipato nje ya muda wa kazi huku wenzake wakisubiri mshahara mwisho wa mwezi kana kwamba hakuna maisha bila mshahara.

Kubwa linalowatofautisha watu hawa ni nidhamu ya matumizi ya fedha zao wanazozipata kutokana na mshahara wao wa kila mwezi.

Zipo nguzo nne za kuyafikia malengo ya mafanikio kiuchumi katika maisha ambazo ni nidhamu katika matumizi ya fedha, kufanya kazi kwa bidii na kujituma, kutoa huduma bora kwa wateja na upekee na ubunifu unaweza kuhimili ushindani katika soko.

Leo tutazungumzia nidhamu katika matumizi ya fedha. Kuna wajasiriamali wengi tu wanaofanya biashara ya kuuza mbogamboga sokoni au wafanyakazi walioajiriwa katika kampuni binafsi au serikalini ambao wangetamani kufanikiwa ila hawajafahamu changamoto zinazowakabili.

Ni kawaida kukuta mjasiriamali wa mbogamboga ambaye kipato chake ni kidogo akimiliki nyumba nzuri na anasomesha watoto wake katika shule nzuri lakini aliyeajiriwa na kupata mshahara mzuri kila mwezi akiwa hana hata kibanda, lakini ana madeni yasiyoisha.

Tofauti iliyopo kati ya wawili hawa ni moja tu. Mmoja wao ana nidhamu ya fedha, mwingine hana nidhamu hiyo wala hana malengo yoyote kuhusu maisha yake. Bila nidhamu ya fedha ni vigumu kufanikiwa kimaisha.

Watu wengi wameshindwa kusonga mbele na kuyafikia mafanikio yao na badala yake kujikuta wakidumaa kiuchumi kwa kukosa nidhamu hiyo. Watu wa aina hii, maisha yao yote, miaka nenda rudi, yanakuwa ni yale yale, hayabadiliki. Maisha mazuri yenye kila kitu wanayasikia au kuyaona kwa wengine.

Siri ya mafanikio ipo katika kila matumizi ya kila senti inayopita mikononi mwako. Ni muhimu kwa yeyote mwenye nia ya kuyapata malengo ya kiuchumi kujitathimini ni kwa vipi anatumia kila senti inayopita mkononi mwake.

Ni haki ya kila mmoja kufahamu endapo sehemu ya kila senti inayopatikana inawekwa akiba ili iongezeke ama inatumika kuzalisha senti nyingine au inaelekezwa kwenye matumizi yaliyopo mara moja na kuisahau.

Kutokuwa na nidhamu ya fedha kumewasababishia baadhi ya watu kufilisika na kugeuka kuwa ombaomba bila kujali kabla ya kufilisika walikuwa matajiri wenye fursa hata ya kukopa fedha kwenye taasisi za fedha; kubwa na ndogo.

Katika dunia ya sasa bado kuna baadhi ya watu wamegeuka kuwa watumwa wa maisha kutokana na tabia yao ya kutaka kujionyesha kwa watu kwamba wanazo fedha za kutumia hata kama fedha hizo wanazipata kwa shinda.

Kwa hakika kabisa, watu wa aina hii, hufika mahali wakayajutia maisha yao pindi kipato anachokichezea leo kutokana na kutokuwa na nidhamu ya fedha kuyeyuka, kwa sababu ya kuendekeza starehe. Kwa wafanyakazi, hushindwa kufanya chochote wakiachishwa au kustaafu.

Wanasahau kwamba katika dunia ya sasa, heshima ya mtu inakuwepo kutokana na mafanikio aliyonayo kiuchumi hasa ushiriki wake kikamilifu katika shughuli za kijamii zinazohusiana na maendeleo yao kwa ujumla.

Hata hivyo, msingi mkuu wa nidhamu ya fedha ni familia. Wazazi hawana budi kuwa mfano bora wa nidhamu katika matumizi ya fedha kwa watoto wao ili nao, kwa kuiga mfano wa maisha ya wazazi wao, waweze kufanikiwa kiuchumi.

Nidhamu ya fedha inaongezeka endapo itafundishwa kuanzia ngazi ya familia. Mtu aliyewekewa misingi imara ya kutunza fedha ana nafasi kubwa ya kufanikiwa. Hata ambaye hakuwa na bahati hiyo anaweza kujifunza kabla hajatimiza ndoto zake.

Ninaamini, yeyote anayeamua kuchukua hatua ya kuthubutu kubadilisha tabia yake juu ya nidhamu katika matumizi ya fedha zake, mafanikio ya maisha yatapatikana kwa njia ya mteremko tu.

Kila mmoja anayo nafasi ya kufanikiwa endapo ataizingatia kanuni hii. Fanya uamuzi sasa kwani bado hujachelewa.

Nikutakie wakati mwema wa kuendelea kusoma makala hizi na kama kuna swali karibuni tujadili kwa pamoja.