Nidhamu yako ya chakula itakuepusha na shinikizo la damu

Muktasari:

Moyo husukuma damu kwenda sehemu zote za mwili kupitia kwenye mfumo maalumu unaoundwa na mishipa hata ile midogo zaidi iitwayo capillary. Ikitokea damu ikatoka kwenye mfumo wake ndiyo huitwa shinikizo la damu, hali inayotokea baada ya msukumo kuwa mkubwa kiasi cha kuifanya mishipa ya arteries kuzidiwa.

Moyo ni kiungo muhimu mwilini kutokana na jukumu lake la kusukuma damu ambayo inatakiwa ifike kila sehemu kwa muda wote. Moyo ni kiungo ambacho hakijawahi kupumzika kuanzia binadamu azaliwe na hakitapumzika mpaka atakapofariki dunia, ili kutekeleza jukumu hilo.

Moyo husukuma damu kwenda sehemu zote za mwili kupitia kwenye mfumo maalumu unaoundwa na mishipa hata ile midogo zaidi iitwayo capillary. Ikitokea damu ikatoka kwenye mfumo wake ndiyo huitwa shinikizo la damu, hali inayotokea baada ya msukumo kuwa mkubwa kiasi cha kuifanya mishipa ya arteries kuzidiwa.

Shinikizo la damu likidumu kwa muda mrefu, husababisha kiharusi au kupooza kwa baadhi ya viungo au upande wa mwili.

Si rahisi mtu kujijua kama anaugua presha kwa kuwa ni ngumu kidogo kuzitambua dalili zake na kibaya zaidi hauna maumivu kama yalivyo magonjwa mengine. Mtu yeyote anaweza kujijua kama anaugua akifanyiwa vipimo vinavyotakiwa.

Kutokana na maendeleo ya teknolojia, kipo kipimo ambacho kila mtu anaweza akanunua na akakitumia akiwa nyumbani kwake na kujipima ugonjwa huu. Kina umbo dogo na huvaliwa kama saa ya mkononi kinapopima shinikizo la damu.

Kipimo cha presha huwa katika milimetres of mercury (mmHg) na huonyesha namba ambazo zipo juu ya namba nyingine. Kwa mfano, kama kipimo kimesoma 120/80mmHg maana yake shinikizo lako la damu ni 120 kwa 80.

Matokeo hayo humaanisha unapokuwa umefadhaika kipimo cha juu cha msukumo wa damu, yaani systolic huwa 120 na 80 ni kiwango cha msukumo wa damu unapokuwa umetulia, yaani dystolic.

Walio hatarini

Unene ni chanzo cha tatizo hili. Kunenepa huko kunajumuisha moyo, hivyo kuufanya ushindwe kutimiza majukumu yake sawasawa na mhusika kuugua shinikizo la damu.

Kipimo kizuri cha afya njema ni mtawanyiko sahihi wa mwili au Body Mass Index (BMI), kipimo ambacho wengi huwa hawajui wanapofanyiwa hospitalini kila wanapopimwa uzito na kuulizwa umri kabla huwajaonana na daktari kwa uchunguzi zaidi.

BMI huangalia umri na kuulinganisha na uzito pamoja na urefu. Baada ya kutaja umri na kupimwa uzito mapokezi, daktari anaweza akakupima urefu ili kujua iwapo uzito wako ni mkubwa au mdogo kuliko inavyotakiwa, kabla haujaenda maabara kwa vipimo zaidi.

Kuwa na uzito uliopitiliza ni dalili ya shinikizo la damu na ukipimwa upo uwezekano mkubwa wa kugundulika hivyo. Katika matukio machache, baadhi ya watu wenye uzito mdogo hugundulika na shinikizo la damu pia. Kwa kawaida, BMI inatakiwa kuwa kati ya 22 na 25

Wazee hasa wenye zaidi ya miaka 50 wapo kwenye hatari shinikizo la damu kutokana na kuchoka kwa viungo vingi vya mwili. Takwimu zinaonyesha takriban asilimia 60 ya wazee wenye umri huo duniani kote huwa ni wagonjwa wa maradhi haya.

Kadri mwili unavyochoka hata njia za damu mwilini nazo hushindwa kumudu kufanya kazi sawasawa. Inashuriwa, kwa wazee, kununua kipimo cha shinikizo damu ili aweze kujichunguza maendeleo yake na kuchukua hatua zinazostahili kila inapobidi na kumfanya aishi maisha marefu zaidi.

Kudhibiti

Kwa kawaida ugonjwa huu huwashambulia zaidi watu wasiofanya kazi nzito, wala kushiriki mazoezi hasa ya viungo. Inapendekezwa kuushughulisha mwili walau kwa kutembea au kukimbia taratibu kabla hujaianza siku yako.

Mazoezi ya viungo hasa ya asubuhi, yamethibitika kitaalamu kuwa hushusha shinikizo la damu kwa takriban 8mmHg mpaka 6mmHg iwapo yatakuwa endelevu.

Viazi vitamu na vitunguu maji

Ukila viazi vitamu robo kilo katika kila mlo wako basi utagundua kuwa unapata nafuu ya shinikizo la damu. Hoja hapa ni kuwa ulaji wa matunda na mboga zenye madini ya potassium ni muhimu katika kushusha shinikizo la damu.

Utafiti uliosimamiwa na mbobezi wa dawa ya kinga kutoka Chuo Kikuu cha Northwestern cha Marekani, Profesa Linda Van Horn, unaonyesha ulaji wa vitunguu maji viwili vikubwa kila siku humarisha afya.

Vyakula maalumu

Vipo vyakula maalumu au food supplements vinavyotengenezwa kwa ajili ya kurekebisha shinikizo la damu. Hivi vinakupa uhakika wa maisha, kwani vimetengenezwa kwa ajili hiyo hasa.

Baadhi ya vyakula hivyo ni garlic tablet au nutrient drink ambazo zina mchanganyiko mzuri unaohitajika.

Mwandishi ni daktari, anapatikana kwa namba: 0768 215 956