FLAVIANA MATATA: Nikumbukwe kwa kuwasaidia wasichana

Mwanamitindo Flaviana Matata

Muktasari:

Akiwa na mtindo wake wa upara alishindana na hata kuvuka kutoka Afrika hadi Marekani alikotua kwenye kampuni maarufu duniani ya uwakala wa wanamitindo inayofahamika kama Wilhelmina. Pamoja na uanamitindo, Matata amekuwa na moyo wa kujitolea kwa muda mfupi aliofanya kazi ya uanamitindo nchini Marekani alianzisha taasisi yake ya Flaviana Matata inayosaidia kuwawezesha watoto yatima.

Hakuwahi kufikiria kuwa shindano la Miss Universe Tanzania 2007 aliloingia kwa kujifurahisha lingemwezesha kuwa miongoni mwa wanamitindo mahiri duniani na hata kuweza kupanda stejini kuonyesha nguo za wabunifu wa kimataifa kama vile Alexander McQueen, Tory Burch, na Vivienne Westwood.

Akiwa na mtindo wake wa upara alishindana na hata kuvuka kutoka Afrika hadi Marekani alikotua kwenye kampuni maarufu duniani ya uwakala wa wanamitindo inayofahamika kama Wilhelmina. Pamoja na uanamitindo, Matata amekuwa na moyo wa kujitolea kwa muda mfupi aliofanya kazi ya uanamitindo nchini Marekani alianzisha taasisi yake ya Flaviana Matata inayosaidia kuwawezesha watoto yatima.

Kupitia taasisi yake hiyo amekuwa akiwawezesha kupata elimu bora kwa kuwapatia vifaa vya masomo.

Haya hapa ni mahojiano yake aliyoyafanya na mtandao wa Black Enterprise:

Ni lini ulianza kujikita rasmi katika uanamitindo?

Niliiingia kwenye Miss Universe Tanzania kwa kujifurahisha tu. Hadi pale niliposhinda ndio nikaanza kufanya kweli. Kupitia shindano la dunia la Miss Universe nikaanza kutafuta fursa na kuzichangamkia.

Ulipata ugumu gani kuzoea mazingira ya Marekani?

Ilikuwa ni ngumu kidogo, hasa ukizingatia kuwa natoka kwenye nchi ya ulimwengu wa tatu. Kila kitu kilikuwa tofauti ila kilichonisaidia ni kwamba haikuwa mara ya kwanza kufika nilishaenda mara mbili kabla. Rafiki zangu walinisaidia sana, lakini hilo haliondoi ukweli kuwa nyumbani ni nyumbani.

Kwa nini uliamua kuanzisha Taasisi ya Flaviana Matata?

Nakumbuka mama yangu alivyokuwa akiwasaidia watoto kwenda shule. Nilikuwa bado mdogo, lakini hakuchoka kutueleza umuhimu wa kusaidia watoto wenye mahitaji. Pia, alikuwa akitusisitiza kuwa njia bora zaidi ya kuwasaidia watoto wenye mahitaji ni kuwawezesha kielimu na kwamba kwa kufanya hivyo utakuwa umewasaidia kujiwezesha katika maisha yao ya baadaye. Huo hasa ndio mwanzo wa Taasisi yangu.

Kufanya kazi kwako Marekani kunawawasaidiaje wasichana wa Kitanzania?

Kazi zangu huku Marekani ndio daraja ninalotumia kusaidia nchi yangu. Inanisaidia kuwaunganisha watu wanaotaka kusaidia nchi yangu. Kwa mfano wakala wangu wa Wilhelmina walinisaidia sana katika mambo mengi yanayolenga kuboresha huduma zinazotolewa na taasisi yangu. Bado ninaendelea kujifunza mambo mengi kutoka maeneo tofauti.

Unajivunia mafanikio gani tangu kuanzisha taasisi yako?

TMF bado ni taasisi changa ila nashukuru Mungu tumeweza kupiga hatua na kufanikiwa kuwapeleka wasichana 15 shule ni matumaini yetu kwa mwaka ujao tutapiga hatua zaidi.

Kwa upande wa wanafunzi wa shule ya msingi tayari tumefanikiwa kuwasambazia vifaa vya shule wanafunzi 3,000. Pia, kwa sasa tumefanikiwa kuisajili nchini Marekani. Hii itatuwezesha kuchangisha pesa kwa ajili ya kusaidia watoto wengi zaidi nchini.

Changamoto gani kubwa unazokutana nazo?

Kwa nyumbani ni watu wachache wanaoelewa maana ya kusaidia jamii. Hii inatupa ugumu katika kufanya kazi yetu, lakini muda si mrefu wataelewa tu.

Watu wanaangalia sana taasisi kubwa na siyo zile zinazochipukia kama hii ya kwetu. Hata kupata sapoti ya vyombo vya habari hasa pale tunapofanya kazi zetu pia huwa ni changamoto.

Ungependa watu wakukumbuke kwa lipi mara utakapostaafu

Si lazima tuwe mabilionea ili tuweze kufanya mabadiliko. Kidogo tunachopata tukitumie kuwasaidia wasichana wetu katika elimu kwani ndiyo urithi pekee tutakaowaachia. Maneno yako na matendo yako yawe msingi imara katika kuwajenga watoto wetu. Hivyo naamini kuwa ninachokifanya sasa kitakuwa kumbukumbu nzuri yangu ya baadaye.

Ushauri gani kwa wasichana ?

Kila siku nimekuwa nikiwasisitiza wasichana kuzingatia elimu kwani ndicho kitu pekee ambacho mtu hawezi kuwanyang’anya. Jua unataka nini. Fanya kazi kwa bidii na la zaidi saidianeni.