Ningekuwa Meneja wa Uwanja wa Jamhuri, ningefanya mambo kumi

Muktasari:

  • Ukiangalia viwanja vitakavyotumiwa kuchezea mechi za fainali za Kombe la Dunia (angalia katikati ya jarida hili) unaweza kutokwa machozi.

Tanzania imebarikiwa kuwa na viwanja takriban katika kila mkoa, lakini utunzaji umekuwa shida na vingi vinachakaa kila inapoitwa leo kutokana na kutofanyiwa marekebisho ya kutosha.

Ukiangalia viwanja vitakavyotumiwa kuchezea mechi za fainali za Kombe la Dunia (angalia katikati ya jarida hili) unaweza kutokwa machozi.

Viwanja vimetawanyika kutoka mji mmoja hadi mwingine.

Kila mkoa una uwanja wake wa kisasa kabisa, na kwa kuwa Kombe la Dunia linakuja, basi ndiyo vimeboreshwa zaidi. Achana na habari hiyo, itakuumiza ukiifikiria.

Wiki hii kulikuwa na pambano la kukata na shoka la Ligi Kuu Bara pale mkoani Morogoro ambako vinara wa ligi hiyo, Simba walikutana na Mtibwa Sugar.

Emmanuel Okwi alifunga bao pekee lililoipa Simba ushindi wa bao 1-0.

Lakini Uwanja wa Jamhuri uliochezewa mechi hiyo unaacha maswali mengi.

Inashangaza Manispaa ya Morogoro kushindwa kuufanya kuwa uwanja huo kuwa wa kisasa zaidi. Uwanja uko katikati ya mji na unaweza kuwa kitega uchumi kizuri kwa mkoa na hata kivutio cha utalii. Si tunasikia Old Trafford inapanuliwa? Bacelona wanataka uwanja wao wa Nou Camp uingize mashabiki 100,000. Lakini Jamhuri ni aibu kusema.

Mambo kumi muhimu

Hata hivyo, kuna mambo kumi ambayo naona kama ningekuwa meneja wa Uwanja wa Jamhuri ningeweza kuyafanya ili kuuboresha. Suala la kwanza ni kushirikiana na manispaa kukarabati maeneo yote ya majukwaa hata ukatazamika. Majukwaa ya Jamhuri yameisha, hayana ladha tamu kwa macho.

Hata pale pa mgeni rasmi, hapafai kabisa kuitwa Jukwaa Kuu.

Ningetumia wataalamu wa viwanja wajenge kama si kukarabati majukwaa kuzunguka uwanja.

Kiukweli, jukwaa la mzunguko kumekuwa na mazingira ambayo si rafiki kwa watazamaji mpira kwani kuna matope ambayo yanatokana na mvua zinazonyesha uwanja hapo.

Ukuta bora zaidi

Mbali na jukwaa, ukuta unafaa kuboreshwa, Mimi ningeubomoa na kujenga bora zaidi na wa kisasa. Kila eneo la kuingilia, ningeliboresha ili mashabiki waingie bila bughudha ikiwemo kuongeza milango na kuondoa msongamano usiokuwa lazima. Milango ya uwanja imejengwa kizamani.

Uzio uwanjani

Ningebomoa uzio wote unaotenganisha wachezaji na mashabiki na kutengeneza mwingine mpya na imara kuufanya uwanja wa Jamhuri kuonekana wa kisasa. Huu uliopo unaweza kusababisha maafa ikitokea umeelemewa kama moja ya picha inavyoonyesha.

Sehemu ya kukimbilia Mbali na eneo la kuchezea mpira, ningetengeneza barabara ya kukimbilia ya kisasa. Ningetandika tartan kwa ajili ya wakimbiaji. Hakutakuwa na suala la mchanga au kukimbilia kwenye lami.

Majani

Ningeifumua eneo la kuchezea soka baada ya ligi kumalizika na kuwafuata watu wa kawaida, hata hawa Boko Veterans kujua walifanyaje kuboresha tofauti na ilivyo Uwanja wa Jamhuri. Hata Uwanja wa Namfua, Singida una sehemu nzuri ya kuchezea.

Ningenunua hata mbegu za majani na kupanda. Ndani ya miezi sita, pitch ya Uwanja wa Jamhuri, siyo ile tena ya kutimka vumbi na mashimo yanayotengeneza enka za wachezaji kwa sasa.

Usaalama milangoni

Pia suala la usalama ni muhimu. Ningeboresha sehemu za kutokea na kuingia. Mpira unapomalizika, usalama ni mdogo, mashabiki huingia uwanjani na kujaa katikati ya uwanja. Unapoingilia inatakiwa ndipo unapotoka. Hakuna suala la kujaa uwanjani baada ya mpira. Ningekuwa meneja, nikaujenga uwanja, hakuna biashara ya kuingia uwanjani.

Kwanza kitendo cha mashabiki kutinga uwanjani ni hatari

kwa wachezaji, viongozi wa timu au hata waamuzi ambao muda mwigine baadhi ya mashabiki hujikuta wakipandwa na ghadhabu.

Kudhibiti mashabikii

Ningekuwa meneja, kusingekuwa na mashabiki kuingia hadi katika vyumba vya kubadilishia nguo jambo ambalo linaweza kuwa hatarishi kwa mtu ambaye anaweza kukusudia kufanya kitu.

Vyoo bora

Ningewajengea vyoo mashabiki kila eneo la jukwaa na miundombinu yake kuunganishwa kwenye chemba moja kwa uwanja mzima lakini pia kukiwa na mifumo sahihi ya maji na majitaka.

Vyumba vya wachezaji

Ningejenga vyumba vya kisasa vya kubadilisha, vyoo na mabafu ya kisasa kabisa ambayo hata timu kutoka nje zinaweza kuja kuweka kambi Morogoro kwa mazoezi kutokana na hali yake ya hewa.

Eneo la waandishi

Eneo lingine muhimu, ningedizaini eneo kwa ajili ya waandishi wa habari. Hapo kungekuwa na mawasiliano ya kila namna, internet na hata WiFi.

Morogoro yapo makampuni makubwa, wadau wa soka na hata nguvu ya Serikali inaweza kuchukua hatua na wakatatua matatizo ya uwanja huo na kuwa wa kisasa ambacho kinaweza kutumika kwa mechi yoyote.

Uwanja huo unaweza kuwa faida kwa wakazi wa Morogoro kwani hoteli zitatumika pindi patakopokuwa na mechi kubwa, biashara aina nyingi zitafanyika, na hata utalii.