Wednesday, March 15, 2017

Nini hatima ya Raia wa EU nchini Uingereza?

 

By Othman Miraji

Uamuzi wa Uingereza wa kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya (EU), uliofikiwa kutokana na matokeo ya kura ya maoni iliyopigwa nchini mwaka jana, unaweza ukawaingiza mamilioni ya raia wa nchi za EU wanaoishi katika kisiwa hicho katika mtafaruku wa kisheria.

Hofu hiyo imeelezwa katika ripoti iliyopatikana katika makao makuu ya EU mjini Brussels, Ubelgiji ambayo ilitokea kwenye kamati ya Bunge la Ulaya inayoshughulikia masuala ya ajira na ya kijamii.

Ilitajwa kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza hadi sasa haijaamua raia gani watakaoruhusiwa kubakia Uingereza na wapi hawataruhusiwa.

Shida iliyoko ni kwamba Uingereza ina utaratibu mbovu na dhaifu sana linapokuja suala la mpangilio kuhusu uhamiaji. Nchi hiyo haina sajala la wakazi, hivyo ni taabu kujua ni raia gani wa nchi za Ulaya wanaoishi kisiwani humo.

Na zaidi ni kwamba ikiwa raia wote milioni 3.3 wa nchi za Ulaya wanaoishi Uingereza itabidi wasajiliwe na kujulikana yupi mwenye haki ya kubakia kuishi nchini humo, itakuwa kazi pevu ya urasimu, ambayo si rahisi kufanyika.

Serikali ya Uingereza haiwaandikishi raia wa nchi za EU pale wanapoingia nchini humo au wanapotoka. Kinyume na ilivyo kama Ujerumani, Uingereza hakuna sheria inayomlazimisha mkazi ajiandikishe serikalini na kutaja wapi anakoishi.

Mwaka 2007 Serikali ya Chama cha labour, chini ya Waziri mkuu Tony Blair, ilishindwa kuupitisha mpango wake uliotaka watu wawe na vitambulisho vya ukazi na kuwepo daftari la wakazi wa nchi nzima.

Sababu, kulikosekana uhakika wa usalama kwamba maelezo binafasi ya mtu yataweza kulindwa na kuhifadhiwa barabara.

Hadi sasa Wizara ya Mambo ya Ndani ya London haijatoa mwongozo vipi Serikali itaweza katika siku za mbele kuyatofautisha madai ya raia wa nchi za Ulaya.

Bila shaka, raia wa nchi za Ulaya wanaoishi Uingereza ni nguzo muhimu sana ya uchumi na jamii ya kisiwa hicho.

Kupata uhakika wa wao kubakia kuishi Uingereza ni jambo linalopewa kipaumbele katika mashauriano baina ya London na Brussels.

Licha ya yote hayo, bado raia wengi wa nchi za EU wanaoishi Uingereza wana wasiwasi kuhusu mustakbali wao.

Wasiwasi kama huo pia wanao raia wa Uingereza wanaoishi Ulaya Bara. Idadi ya Waingereza ambao wanataka kuchukua uraia wa Ujerumani imeongezeka sana katika miezi michache iliyopita. Kwa mfano, baada ya Uingereza kutangaza itajitoa kutoka klabu hiyo ya Ulaya, idadi ya Waingereza katika mji wa Hamburg na Berlin walioomba uraia wa Ujerumani iliongezeka sana.

Mjini Munich kati ya Juni 2016 hadi Januari 2017 Waingereza 144 wameomba uraia wa Kijerumani. Idadi hiyo ni karibu mara sita zaidi ya ile katika kipindi kama hicho mwaka wa kabla.

Ni jambo la kufurahisha, japokuwa ni la kushangaza, ukitambua kwamba Ujerumani na Uingereza zilikuwa mahasimu wakubwa na kupigana vita vikali miaka 70 iliyopita

Kwa upande mwingine, Rais wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker ana wasiwasi kama Uingereza itaweza kuuratibu uhusiano wake mpya na Umoja wa Ulaya miaka miwili ijayo baada ya kutangaza kujitoa.

Anasema haamini kwamba ndani ya miezi 24 itawezekana kuyatanzua masuala kadhaa na kuwa na mkataba utakaojenga uhusiano mpya baina ya London na Brussels. Junker alionya kwa kusema: “Anakosea sana yule mtu anayefikiri kwamba yawezekana ndani ya miaka miwili utaratibu wa namna Uingereza itakavyojitoa kutoka Umoja wa Ulaya utakamilika.” Idara anayoisimamia Jean-Claude Junker ndiyo yenye dhamana ya kufanya mashauriano na Uingereza.

Kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa Ulaya baada ya miaka miwili ndipo Uingereza itakuwa si mwanachama wa Umoja huo, na ni hapo muda wa mashaurinao utakuwa umemalizika.

Kwa dharura yawezekana Uingereza ikatoka bila ya kuweko mkataba wa makubaliano. Kipindi kabla ya kutoka kinaweza tu kurefushwa pindi nchi zote 27 wanachama zitakubali. Kwa Uingereza itabidi zaidi ya sheria 20,000 zibadilishwe kwa ajili ya nchi hiyo kujitoa, anasema Junker. Wakati huohuo Junker analaumu kwamba Uingereza tangu sasa inajaribu kufanya mashauriano ya kuwa na mikataba ya kibiashara na nchi moja moja za Umoja wa Ulaya, akishikilia kwamba mikataba ya kibiashara ni jukumu la kamisheni anayoiongoza yeye.

“Hakuna mtu yeyote, nchi yeyote iliyo mwanachama wa Umoja wa Ulaya yenye haki ya kuingia peke yake katika mikataba ya kibiashara.”

Juncher anaweka wazi kwamba katika mashauriano na Uingereza, kamisheni yake haitatetereka kubakia na misingi minne ya uhuru ndani ya Umoja wa Ulaya- uhuru wa kwenda huku na kule wafanya kazi, rasilimali, bidhaa na huduma ndani ya eneo la nchi za EU. Anasema mtu au nchi ama iwe ndani au iwe nje ya EU, haiwezi ikawa ndani na wakati huohuo ikawa nje.

Maana yake anakusudia kwamba Uingereza haiwezi kubakia na keki yake na huku inaila. Haiwezi kuwa nje ya EU na kuendelea kufaidi utamu wa kuwa mwanachama.

Wajumbe kadhaa wa Bunge la Ulaya wamepinga wazo la Uingereza kuachiwa, kwa mujibu wa sheria maalumu, kupata baadhi ya faida za uanachama pale itakapokuwa si tena mwanachama wa EU. Wanataka pale nchi hiyo itakapotoka kwenye Umoja huo isipate tena faida zozote wanazopata wanachama.

Lakini kuna wasiwasi kama nchi zote 27 wanachama wataweza kuwa na msimamo mmoja katika mashaurinao na Uingereza. Hiyo ni hofu iliyoelezwa na Jean-Claude Junker, akisema Uingereza huenda itafaulu, tena bila ya kutumia jitihada kubwa, kuwagawa wanachama wengine wa EU na kujipatia manufaa.

Kutokana na hali ilivyo sasa, Junker amevunjika moyo na EU na ametangaza kwamba hatataka tena kubakia kuwa Rais wa Kamisheni ya Umoja huo pale kipindi chake cha sasa kitakapomalizika. Kabla ya kushika wadhifa wake huu yeye alikuwa waziri mkuu na wa fedha wa Luxembourg.

Anatambuliwa kuwa ni mwanasiasa wa Ulaya aliye na uzoefu mkubwa. Tangu Novemba 2014 alipokamata cheo hicho amekabiliana na changamoto kadhaa ambazo ziliuweka Umoja wa Ulaya katika mitihani mikubwa- mzozo wa kiuchumi, ukosefu mkubwa wa ajira katika nchi za Kusini ya Ulaya, mzozo wa madeni ya Ugiriki na mmiminiko mkubwa wa wakimbizi kuja Barani Ulaya.

Mwezi huu Uingereza inatarajiwa kuwasilisha rasmi huko Brussels ombi lake la kutaka kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya, hivyo saa ya ukweli inakaribia.

Unapotembelea Uingereza hivi sasa huoni ishara yeyote miongoni mwa wananchi kwamba wanaujutia uamuzi wao wa miezi minane iliyopita wa kutaka kujitenga kutoka Ulaya. Hata Serikali inajiamini kwamba baada ya talaka hiyo nchi hiyo itaweza kupata washirika wengine wa kibiashara nje ya Ulaya na kwamba talaka hiyo haitamaanisha uhasama baina ya pande mbili.

Lililo wazi ni kwamba Waingereza wamecheza kamari walipopiga kura yao ya maoni mwaka jana. Kama watakuwa washindi na kiwango gani cha faida watakachokipata ni maswali ambayo hamna bingwa yeyote anayeweza kuyajibu kwa sasa.

Na zaidi, hamna mtu anayeweza kutabiri athari kwa raia wa pande mbili katika talaka ya aina kama hii.

-->