Njaa kikwazo cha elimu shule za msingi Mbeya

Muktasari:

  • Muda huo, wanafunzi wanaonekana kutokuwa na umakini katika somo la Hisabati. Wanaonekana kudhoofika na kuchoka hasa ikizingatiwa kuwa hawajaweka chochote tumboni tangu asubuhi.
  • Kwa mujibu wa ratiba ya shule, muda huo, wanafunzi wanapaswa kurudi nyumbani kwa ajili ya kupata chakula cha mchana kabla ya kurudi shuleni saa nane mchana kwa ajili ya kuendelea na masomo. Lakini leo, mwalimu Kyejo alichelewa kidogo kuwaruhusu.

Inakaribia majira ya saa saba mchana katika Shule ya Msingi Madaraka iliyopo Tukuyu, Wilaya ya Rungwe, Mbeya. Mwalimu Ezron Kyejo anamuuliza mmoja wa wanafunzi wa darasa la nne, “Tatu mara tatu ni ngapi?.” Mwanafunzi hajibu chochote. Anakaa kimya.

Muda huo, wanafunzi wanaonekana kutokuwa na umakini katika somo la Hisabati. Wanaonekana kudhoofika na kuchoka hasa ikizingatiwa kuwa hawajaweka chochote tumboni tangu asubuhi.

Kwa mujibu wa ratiba ya shule, muda huo, wanafunzi wanapaswa kurudi nyumbani kwa ajili ya kupata chakula cha mchana kabla ya kurudi shuleni saa nane mchana kwa ajili ya kuendelea na masomo. Lakini leo, mwalimu Kyejo alichelewa kidogo kuwaruhusu.

Baada ya kubaini hali hiyo, mwalimu huyo, anawaruhusu wanafunzi waende kujitafutia chochote kwa ajili ya kuupa mwili nguvu. Baadhi ya wanafunzi waliondoka, wengine walibaki katika maeneo ya shuleni ili kuwasubiri wenzao kwa ajili ya vipindi vya mchana.

Samuel Festo ni miongoni mwa wanafunzi wa darasa la saba ambao hawakwenda nyumbani kwa ajili ya kupata chakula cha mchana. Anasema: “Nyumbani kwetu ni mbali, siwezi kwenda na kurudi hapa kuendelea na masomo.”

Iwapo Festo angeweza kwenda nyumbani angepata chochote cha kula, kwa wengine hali ni tofauti.

“Hata nikienda nyumbani, nitapata nini kule? sipati kitu. Ni bora nibaki hapa (shuleni) hadi jioni,” anasema Isaya Peter, mwanafunzi mwingine.

Wengine wanaomudu kufika majumbani mwao siyo kana wote kwamba wanakuta chakula kipo mezani ili wale na kuwahi kurudi shuleni kuendelea na masomo. Wanapaswa kuingia jikoni na kujipikia japokuwa muda ni mfupi.

Yuster Oden, ni miongoni mwa wanafunzi wanaoweza kufika nyumbani mapema, shukrani kwa makazi yao kuwa karibu na shule. Anasema kwa kuwa wazazi wanakuwa shambani, sokoni ama kwenye shughuli nyingine za kujipatia kipato, wanafunzi hulazimika kujipikia mara warudipo nyumbani mchana.

Athari ya chakula katika taaluma

Kutokuwapo kwa huduma ya chakula cha mchana katika shule za msingi mkoani Mbeya, ni miongoni mwa sababu zinazochangia mkoa huo kushindwa kufikia lengo la taifa la ufaulu wa asilimia 80.

“Wanafunzi wanapokuwa na njaa hawajifunzi sawasawa na hii hali ipo kila mahali ambapo wanafunzi hawapati chakula cha mchana.

“Tunapowaruhusu wanafunzi hawa waende nyumbani kula kwa mujibu wa ratiba ya shule na kurudi saa nane, wengi wanashindwa kufanya hivyo. Na hata uwepo wao kiakili unakuwa mdogo,” anasema Mwalimu Kyejo ambaye amefundisha kwa takribani miaka 28.

Mwaka 2016, Shule ya Madaraka ilifaulisha kwa wastani wa B na kuwa ya sita katika Wilaya ya Rungwe. Kitaifa, Madaraka imekuwa ya 1,769 kati ya shule 8,109 ambazo zilikuwa na wanafunzi zaidi ya 40. Juhudi kubwa inatoka kwa walimu kwa kukubali kufundisha muda wa ziada hasa kwa madarasa ambayo yanakabiliwa na mitihani ya kitaifa.

Walimu katika shule hii wanasema kuwa iwapo kungekuwapo na utaratibu wa kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi shuleni hapo, wanafunzi wa Madaraka wangefanya vema kama ilivyo kwa Shule ya Msingi Nuru iliyopo nje kidogo ya mji wa Tukuyu inayotoa uji saa nne asubuhi na chakula cha mchana.

Shule ya Msingi Nuru

Kwa mujibu wa ratiba ya Shule ya Nuru, ifikapo saa nne asubuhi, wanafunzi hunywa uji uliochanganywa na maziwa na sukari na saa saba hupata chakula cha mchana, shukrani kwa utaratibu wa uchangiaji wa ada.

Shule hii ambayo lugha ya ufundishaji ni Kiingereza, ni miongoni mwa shule chache za msingi Tanzania ambazo zimeruhusiwa kuendelea kutoza ada.

Mwalimu mkuu, Herbert Mwambipile anasema: “Kiasi cha fedha kinachokusanywa kinatumika kwa ajili ya uendeshaji wa shule pamoja na kugharimia chakula cha wanafunzi wakiwa shuleni.”

Anasema kuwa siri pekee ya shule yake kufaulisha wanafunzi kwa asilimia 100 katika mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwaka jana ni uwapo wa uji na chakula cha mchana pamoja na kuwa na walimu wanaowajibika

Mbali na mafanikio hayo, Nuru iliongoza kwa shule za Serikali kwa kuwa kuwa ya kwanza kiwilaya na mkoa wa Mbeya. Kitaifa, imekuwa ya 302 kati ya shule 8,241 zenye wanafunzi chini ya 40.

Njaa shule za Mbeya

Kwa mujibu wa ofisi ya elimu ya mkoa wa Mbeya, shule za Serikali zinazotoa chakula kwa sasa ni 32 pekee na nyingi ni za wilaya ya Mbarali.

Hadi Machi, mwaka jana, takwimu kwa umma (open data) zinaonyesha mkoa huu kinara katika uzalishaji wa chakula, ulikuwa na shule za Serikali 756.

Baadhi ya maofisa wa wilaya na elimu ambao hawakutaka kuweka majina yao bayana wanasema kuwa kushuka kwa idadi ya shule zitoazo chakula kumeanza mara baada ya Serikali kuanza kutekeleza sera ya elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari.

Baadhi ya walimu nao wanasema wazazi na wananchi wengi kwa ujumla hawakuelewa lengo hilo na wanajiona hawawajibiki kwa watoto wao ikiwamo kuchangia chakula shuleni.

“Shule zetu nyingi hazitoi chakula cha mchana kwa kuwa wazazi hawachangii. Wanafanya hivyo tu ikiwa ni wakati wa mitihani ya kitaifa na wakati wa chanjo,” anathibitisha mkazi aitwaye Mama Hadija na kuongeza:

“Tangu kuanza sera ya elimu bure, wengi tuliamini kila kitu ikiwamo chakula. Lakini wazazi wengi hawana imani na walimu kwa kuhisi watachukua fedha na chakula tutakachochangia shuleni.

“Mkoa wa Mbeya bado uko nyuma ya malengo ya kitaifa wa kufaulisha kwa asilimia 80 katika ngazi ya elimu ya msingi. Kwa miaka mitatu mfululizo, mkoa huu umeshindwa kufikia lengo, jambo linalosababisha hii kuwa ajenda muhimu katika vikao vya maendeleo ya Mbeya.

“Mwaka 2014, lengo la kitaifa lilikuwa ni asilimia 70 lakini mkoa (Mbeya) ulifanikiwa kufaulisha kwa asilimia 48.8 pekee.

“Mwaka 2015 lengo la taifa lilikuwa ni asilimia 80, mkoa ulifaulisha asilimia 57.09 na mwaka jana; Mbeya iliweza kufaulisha asilimia 60.73 chini ya kiwango cha taifa,” inasomeka sehemu ya ripoti ya Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) ya mwaka jana.

Japokuwa ripoti hiyo haihitaji kukosekana kwa chakula kama moja ya sababu zinazochangia kuanguka kwa elimu ya msingi mkoani Mbeya, Mwalimu katika shule ya Nuru, Brown Kisinga anasema wataalamu katika serikali za mitaa wanapaswa kutoa elimu kwa wazazi ili kujua uhusiano kati ya kukosa chakula shuleni na matokeo mabaya.”

Anaeleza: “Mkoa huu una vyakula mbalimbali, suala hapa ni kuwaunganisha wazazi ili wachangie chakula ikiwa tunataka watoto wetu wafanye vema katika mitihani ya darasa la nne na la saba.”

Kauli ya Serikali

Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya BBC hivi karibuni, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, anasema Serikali hutoa fedha za chakula kwa ajili ya shule za msingi za bweni, hususani za wanafunzi wa mahitaji maalum.

Kuhusu shule nyingine za msingi, Simbachawene anasema: “Kwa wale wanaosoma shule za kutwa za msingi na sekondari, ni jukumu la mzazi kuchangia.”