Njia inayofaa kwa CCM mpya kupita

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akishiriki kupalilia katika shamba la Mage Kolimwa (wapili kulia), katika Kijiji cha Mlimanyoka, Kata ya Nsalanga, wilala ya Mbeya mjini.Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Malengo ya chama cha siasa ni kushinda chaguzi na kukamata dola. Na kwa jinsi hii; ili kujiaminisha mbele ya umma, ni kuwa thabiti kwa kauli na kusimamia maamuzi yanayowekwa.

Mafanikio ya kweli hujengwa katika nidhamu ya kile unachokiamini na kukisema. Kauli thabiti, utekelezaji na usimamizi wa maazimio unayojiwekea iwe kwa mtu binafsi, shirika au taasisi ndiyo msingi mkuu wa kufikia mafanikio.

Malengo ya chama cha siasa ni kushinda chaguzi na kukamata dola. Na kwa jinsi hii; ili kujiaminisha mbele ya umma, ni kuwa thabiti kwa kauli na kusimamia maamuzi yanayowekwa.

CCM inajipanga upya kupitia uchaguzi ndani ya chama. Msingi mkuu wa uchaguzi huu ni kwa namna watu wasio waadilifu wataondoka kwenye uongozi wa chama. Mabadiliko ni mfumo na kwa namna ya pekee Watanzania wanataka kuona sura halisi ya mabadiliko kutoka CCM.

Leo nawaandikia wana CCM, chama changu ambacho katika majukumu yangu ya kila siku, ninatekeleza Ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2015.

Utekelezaji wa ilani utakipa fursa ya kuaminiwa tena. Lakini, wakati wakitegemea utekelezaji wa Ilani kati ya 2015-2020, watalazimika kujipambanua na kujitafakari kiundani namna taswira yao inavyoweza kuwabeba.

Ni shauku yangu kuwaona wananisikiliza. Malengo ya chama ni kushinda uchaguzi na kupata ridhaa ya kuunda Serikali.

Hivyo basi, msingi wa makala ya leo ni kuwaasa wanachama na viongozi katika ujenzi wa safu imara ya kuwawezesha kupata ushindi katika chaguzi zijazo.

CCM na mabadiliko

Sura halisi ya mabadiliko huanzia CCM na ni huko kuliko na ubingwa wa kufanya yasiyotarajiwa. Ni mabingwa wa kimapinduzi na uzuri wake hawaishiwi mipango wala hazina ya fikra ya kutekeleza mipango hiyo.

Baada ya kuasisi dhana ya kujivua gamba ni dhahiri wamekuwa mashujaa katika kusimamia wanachokiamini, na CCM si waoga kutembea kwenye njia zao.

CCM ni chama kisichoweza kuyumba kuhusu hazina yake ya viongozi na mifumo yake ya kuandaa na kutengeneza viongozi wa chama pamoja na wa Serikali. Kwa minajili hii, ni mabingwa wa kuleta maingizo mapya na mambo yanakwenda sawa. Ustahimilivu wa kuvumilia kukosolewa na kujielekeza kwenye misingi yake ni vitu vinavyotakiwa kuonyeshwa wakati huu wanapochaguana kuliko wakati mwingine wowote.

CCM ni chama kikongwe, na kwa Afrika ni viwili au vitatu vilivyobaki kati ya vile vilivyopigania uhuru wa Afrika ndani na nje ya nchi zao. Vingine ni Zanu-PF ya Zimbabwe na ANC ya Afrika Kusini.

Kimfumo, inasadikiwa kuwa ni vyama viwili tu ambavyo mifumo yake ni imara na mambo yake yote huendeshwa kwa misingi isiyotetereka, ambavyo ni CCM na CPC cha China.

Hivyo, tunapowaandikia kuwashauri tunajua wazi mawaidha yetu yanakwenda kwenye chama ambacho baada ya kuyasoma haya watachukua muda kuyajadili na kuyahifadhi ama kwa matumizi ya sasa au ya baadaye.

CCM wanao uamuzi wa kujitafsiri kwa upya na kujijengea taswira njema miongoni mwa Watanzania. Mifumo ya kiuongozi na utawala kuanzia ndani ya shina, tawi, kata na wilaya inawapa uwezo wa kujijenga imara katika ngazi ya mkoa na Taifa.

Msingi wa mashina umewafanya kuenea mahala pote katika Taifa hadi katika vijiji na vitongoji.

Tunatambua, wamemaliza chaguzi za jumuiya ngazi ya wilaya, na wanaedelea mchakato wa uchaguzi wa chama ngazi ya wilaya.

Tunatoa maoni yetu wakati huu muafaka tena kupitia gazeti linalosomwa na wasomaji wengi kuliko jingine lolote. Ni matumaini kuwa mawaidha haya watayazingatia wanapokwenda kuchagua mwenyekiti, mwenezi na wajumbe wa kamati za siasa za wilaya.

Udhibiti wa wanachama

Kwa mara ya kwanza nikiwa na akili timamu nashuhudia uchaguzi wa CCM usio na mbwembwe wala purukushani. Nashuhudia wapiga fitina wakifanya hayo kwa tahadhali kubwa, si kwa kuwa hawana hizo mbwembwe bali kwa kuzingatia udhibiti mkubwa wa nidhamu ya wanachama uliowekwa.

Tunaweza kuwa tumepunguza makelele mitaani na kupata viongozi waadilifu, lakini tunaweza kuwa tumepunguza makelele, na kuwa tumetoa mwanya wa wahalifu kujipanga na kuwa wamefanikiwa kujenga makelele ndani ya chama.

Hili ni jambo la kufanyia uchunguzi mkubwa na likigundulika basi msisite kuchukua hatua kwa watakaodhihirika.

Kwa kuwa tumefanikiwa sana kudhibiti hali, na kwa kuwa hatukuwa na muda wa kutafakari athari za udhibiti, lazima tujiandae sasa kuwajenga kiuwezo mkubwa wa kiadilifu viongozi wetu.

Hatukuwa na uhakika kuhusu usiri wa mipango yetu, hasa ngazi ya wilaya na kwa hivi yaweza kuwa imevujisha yale tuliyokuwa tunajipanga nayo. Msingi huu unaturejesha katika ujengaji wa uadilifu kwa viongozi baada ya uchaguzi huu.

Rushwa katika uchaguzi

Kwa kuwa mfumo wa udhibiti ulikuwa mkali, haikuwa rahisi kwa wajanja wa kugawa khanga, vitenge, fedha na pombe kukusanya watu na kuwafanyia takrima.

Kwa kuwa mbinu iliyotumika mpaka sasa ni usiri wa majina ya wagombea mpaka siku ya uchaguzi, tunadhani ilikuwa mbinu ya kuwafanya wanaogombea kuchanganyikiwa kwamba ama wafanye kampeni au wasifanye.

Jambo moja la hakika ni kuwa katika vikao vya maamuzi, wagombea walikuwa na watu wao, na hao wanaweza kuwa waliwapa taarifa kuwa wameteuliwa kugombea ikiwa uadilifu wao uko ngazi ya chini.

Kama hili lilitokea, ndipo tunarejea wito kwa chama kufanya uchunguzi wa kina na likidhihirika, ni lazima kuchukua hatua kali kwa wahusika.

Mifumo ya mabadiliko si rafiki na haipendwi. Fikiria wajumbe waliozoea nyakati za uchaguzi kuwa ni za mavuno, na mwaka huu wametoka patupu, wanawazia nini kuhusu mabadiliko?

Fikiria waliozoea kushinda kwa rushwa, na mwaka huu wamebanwa na kushindwa, wanawaza nini kuhusu mabadiliko?

Fikiria wale wapiga dili wenye ushawishi wa makundi, kwamba mwaka huu haipo na hakuna mlipaji, wanawaza nini kuhusu mabadiliko?

Mabadiliko ya kimfumo na kimuundo na utendaji ndani ya CCM yameondoa makundi ya wajivuni na kufutilia mbali kabisa sura ya rushwa za kugawana kama pipi.

Hatuna uhakika kudhibitiwa kwa asilimia mia moja, lakini tunao uhakika hawakujiachia kwa asilimia mia moja.

CCM inayohubiri mabadiliko imeamua kujitambulisha kihivyo na ni shauku ya Watanzania na wanachama wake kuona waliokuwa wanakichafua chama wanaondolewa na waadilifu wanatamalaki.

CCM isiyumbe

Huu ni mwaka wa CCM kujizaa upya, ni mwaka wa kujielekeza kwenye kujivua gamba kweli. Inawezekana wapo wachache waliovuka kikwazo cha chujio na wakafanikiwa kupita kwa hila. Inawezekana bado wapo wanaojipanga kuunda safu zao hasa kwa ajili ya chaguzi zijazo za Serikali, na wana nguvu ya kudhibiti mifumo halali wakipanda mifumo yao haramu. CCM lazima ijitambue vema, kuwa hakuna aliye mkubwa kuliko chama na kwa namna yoyote, isimvumilie yeyote hata ikiwa kwa gharama ya kurudia uchaguzi.

Chama cha Mapinduzi lazima kijitambulishe uimara wake kwa kauli thabiti. Wanachama wake, pamoja na kutakiwa kuachana na rushwa, wawafichue wale waliohusika kwa namna moja ama nyingine kupata madaraka kwa rushwa.

Mabadiliko hayatafikiwa ikiwa kila mwanachama atasubiri wengine wawajibike kabla yake. Lazima kujitenga na woga na hofu, lazima kujishughulikia ipasavyo na bila haya wala aibu kinyume chake watahitaji kutumia nguvu nyingi kujiaminisha mbele za umma.

Siasa za matukio

CCM ikiwa chama chenye misingi imara na mifumo thabiti, ijiondoe kwa ujumla kwenye siasa za matukio. Haihitajiki kuhusika kwa namna yoyote kwenye majibizano yasiyo na mashiko badala yake ijikite katika kuelekeza Serikali kutekeleza Ilani ya uchaguzi.

Hoja za Serikali zijibiwe na Serikali na chama kihakikishe viongozi na watendaji wa Serikali wanatoa majibu stahiki hasa kwa kero zinazohusu maendeleo ya wananchi.

Chama kiwatose wapenda rushwa, kiwadhibiti wenye mienendo ya kutia shaka, kiwafute kabisa uanachama wanaoleta chokochoko ili kujenga nidhamu ya chama na wanachama wake.

Falesy Kibassa ni Msomaji wa Magazeti ya Mwananchi, Mtafiti na Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Kondoa

Simu: +255716696265/ Barua pepe [email protected]