Njia rahisi za utengenezaji wa mbolea ya mboji

Hivi ndivyo unavyoweza kuandaa mbolea ya mboji kitaalamu. Na Mpiga Picha Wetu

Muktasari:

  • Virutubisho hivyo ni pamoja na madini muhimu yanayohitajika na mmea kwa kiasi kikubwa kama vile naitrojeni, fosiforasi na potashi.
  • Haya huhitajika kwa kiasi kikubwa na ndiyo mana kila mbolea inayotengenezwa kiwandani huwekwa madini haya muhimu matatu.

Mbolea ni chakula cha mimea, ambacho ni mchanganyiko wa virutubisho mbalimbali vinavyoongezwa kwenye udongo au vinavyowekwa moja kwa moja kwenye mimea ili kuongeza ukuaji na uzalishaji wa mimea.

Virutubisho hivyo ni pamoja na madini muhimu yanayohitajika na mmea kwa kiasi kikubwa kama vile naitrojeni, fosiforasi na potashi.

Haya huhitajika kwa kiasi kikubwa na ndiyo mana kila mbolea inayotengenezwa kiwandani huwekwa madini haya muhimu matatu.

Lakini pia kuna madini mengineyo muhimu kama vile salfa, chokaa, magnesiam, shaba. Zinki, molybedenum, chuma na mengineyo.

Mbolea asili

Hizi ni mbolea zinazotokana na mabaki ya wanyama na mimea. Mbolea za asili ni kama vile mbolea vunde/mboji, mbolea ya kimiminika (liquid manure), samadi, mbolea ya kijani na matandazo.

Mbolea ya mboji

Haya ni mabaki ya mimea na wanyama ambayo baada ya kuoza kwa muda mrefu kwa ajili ya kusazwa au kuozeshwa au kuvunjwavunjwa na viumbe wadogo. Sehemu za vitu kama majani, matunda na mabaki ya mboga, ndiyo hutengeneza mbolea ya mboji.

Hatua za utengenezaji mboji

Tayarisha sehemu ya chini yenye upana wa mita moja na urefu wa mita tatu, tumia vijiti visivyooza kwa urahisi. Mfumo huu huwezesha hewa kusambaa kwa urahisi na kuvutia vijidudu wanaosaidia katika kuoza.

Hakikisha mahala ni tambarare kisha baada ya hapo tifua sehemu hiyo kisha weka fito moja katikati na katika kila kona. Baada ya hapo utaandaa matabaka yafuatayo:-

Tabaka la kwanza: Hapa utatandaza viungo visivyooza kwa urahisi kama mabaki ya mahindi (mabua yaliyokatwa katwa ) au nyasi kavu, mabaki ya miwa hadi kina au kimo cha sentimita 10 sawa na nchi 4. Kisha loanisha kwa maji.

Tabaka la pili: Tandaza viungo vinavyoweza kuoza kwa urahisi kwa mfano matunda na mabaki ya mbogamboga au nyasi mbichi zisizo na mbegu au mabaki ya jikoni (majivu) kwa kina cha sentimita 10-15

Tabaka la tatu: Tandaza samadi kina cha sentimita 5 sawa na nchi 2. Lengo la kuweka samadi ni kuchochea uozeshaji wa mboji. Pia samadi ina virutubisho vingi vya mmea kama vile naitrojeni.

Tabaka la nne: tandaza udongo kwa kina cha sentimita 2.5 sawa na nchi 1. Udongo husaidia kuzuia upotevu wa hewa ya ammonia ambayo ni matokeo ya kuoza kwa vitu vyenye asili ya mimea na wanyama.

Rudia utaratibu huu hadi kufikia kimo cha urefu wa mita moja hadi moja na nusu juu. Funika kwa nyasi au majani (kama yale ya migomba) ili kuzuia kupotea kwa unyevu.

Endelea kumwagia maji kwa kutumia keni au chombo chochote chenye matundu

Fanya kazi hii kwa muda usiozidi wiki moja. Baada ya wiki mbili hadi tatu utahitajika kupindua tabaka hizo na kutayarisha upya. Hii ni kwa sababu viungo huoza kwa wakati tofauti.

Vile viungo vilivyo juu ambavyo havijaoza, vinapaswa kuwekwa kwenye tabaka la katikati na kunyunyiziwa maji. Funika sasa kwa viungo vilivyosalia. Tabaka za awali hazitaonekana. Rudia utaratibu huu baada ya wiki tatu au kulingana na muda unaochukua viungo kuoza. Mboji inaweza kuwa tayari baada ya miezi mitatu.

Kama utakuwa ukiimwagia maji na kuigeuzageuza itachukua miezi mitatu kuwa tayari, lakini kama ukiiacha ioze yenyewe inaweza kufikia hata miezi sita mpaka kuoza.

Matumizi yake hutegemeana na ukubwa wa shamba, ila uhitaji wake hauna tofauti na samadi kama tutakavyoona katika makala zijazo.

Zingatia

Unapotumia mboji, changamoto kubwa ni kuhakikisha kuwa imeoza vizuri na namna ya kuitumia kwa usahihi.

Ikiwa mchanganyiko uliotumika kutengeneza mboji hiyo ulikuwa na ubora wa chini, mboji hiyo nayo itakuwa na ubora mdogo.

Usiache mboji ikapigwa na jua au mvua, kwa kuwa hali hii inaweza kusababisha kupotea kwa virutubisho kwenye mboji. Aidha, kinyesi cha mifugo huboresha mboji zaidi.