Nusu ya watoto kulelewa na mzazi mmoja ifikapo 2050

Muktasari:

  • Mwaka wa kwanza ulikuwa mgumu. Nilipata ugumu kwa sababu sikuwa kumuona mwanamke mwingine aliyelea mtoto bila baba. Nilikuwa wa kwanza.
  • Nakumbuka ilikuwa mwaka 2005, mtu pekee ambaye nilimwangalia kama mfano wangu ni mwanamuziki Madonna ambaye naye alikuwa analea watoto wake bila baba kwa wakati ule. Ingawa alikuwa mbali na mimi lakini nilimfuatilia na ilinipa faraja.

Binti yangu alipotimiza umri wa miezi saba nilitengana na baba yake. Aliondoka bila kuniambia anakoelekea. Ilibidi nianze maisha upya, katika umri wa miaka 28 nikiwa nimechanganyikiwa nilikabiliwa na jukumu la malezi peke yangu.

Mwaka wa kwanza ulikuwa mgumu. Nilipata ugumu kwa sababu sikuwa kumuona mwanamke mwingine aliyelea mtoto bila baba. Nilikuwa wa kwanza.

Nakumbuka ilikuwa mwaka 2005, mtu pekee ambaye nilimwangalia kama mfano wangu ni mwanamuziki Madonna ambaye naye alikuwa analea watoto wake bila baba kwa wakati ule. Ingawa alikuwa mbali na mimi lakini nilimfuatilia na ilinipa faraja.

Ndiyo. Nilipata faraja kuona kumbe hata supastaa anaweza kuachiwa malezi ya watoto. Anaweza kuachika kama mimi. Hakika hii ilikuwa faraja yangu.

Taratibu nilianza kuzoea maisha haya. Nilichogundua ni kuwa malezi ya mzazi mmoja na yale ya pamoja hayana tofauti. Kukesha na mtoto, kumwogesha, kumlisha au kumuuguza pale anapopata tatizo la kiafya.

Hayo ni maneno ya Rachel Sarajo katika kitabu chake ‘Surviving as a Single Mom’ kinachoelezea safari yake ya miaka 10 ya kumlea mtoto wake bila mzazi mwenzake.

Sarajo ni mmoja kati ya wengi, idadi ya watoto wanaolelewa na mzazi mmoja inaongezeka kila siku. Wapo wanaochagua kuwa hivyo na ambao wanajikuta kwenye ulimwengu huo bila kutarajia.

Taasisi ya utafiti Pewresearch imetoa takwimu za ongezeko la wanawake wanaolea watoto peke yao na kwamba mpaka kufikia 2050 itakuwa imefikia nusu ya wanawake wote.

Imesema tangu mwaka 1965 kumekuwa na ongezeko la wanawake wanaolea watoto peke yao (single mothers) na katika utafiti huo uliofanyika katika ya mwaka 2014 na 2015 uligundua kuwa idadi hiyo imefikia asilimia 22.

Wapo ambao huchagua kupata mtoto bila hata ndoa na hii inaweza kutokea pale mwanamke anapoona umri wa kuolewa umepita na hivyo kubeba ujauzito, lakini wapo ambao hupata watoto ndani ya ndoa lakini huachika.

Ukweli ni kwamba wapo waliopo kwenye ndoa lakini maisha wanayoishi hayana tofauti na wale walioachiwa malezi ya wa watoto. Katika kundi hili kila mtu ana changamoto yake, wengine wanashindwa kujikimu wao na watoto na wengine wengi wakiwa na uwezo wa kupatia watoto wao kila wanalohitaji isipokuwa uwepo wa baba zao tu.

Hapa nchini wanalizungumziaje

Belinda Mbogo mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka 19 ana mtoto mmoja wa kiume.

Malezi ya mtoto kwake si magumu kwa kuwa bado anaishi nyumbani hivyo ndugu na jamaa humsaidia hata hvyo kilio chake ni mtoto wake kukosa huduma muhimu.

“Siwezi kudanganya kuwa malezi yananipa ugumu kwa sababu bado nipo nyumbani, lakini ningetamani kumuona mwanangu akiwa karibu na baba yake,” anasema Mbogo.

Mkazi wa Tabata Kisukuru, Santieli Mmakasa anasema kulea mtoto bila baba siyo kikwazo ispokuwa anahitaji msaada kutoka kwa mzazi mwezake.

“Sijawahi kujutia kupata mtoto kabla ndoa au kumlea peke yangu, nampenda mwanangu na kwa kuwa nahitaji awe na maisha mazuri ndiyo maana huwa namhitaji mzazi mwenzangu anisaidie,” anasema Mmakasa.

Upo umoja wa mzazi mmoja

Mitandao nchini imekuwa na faida na moja wapo ni kuwakutanisha wanawake wanaolea watoto bila baba zao.

Mwanzilishi wa Umoja wa Wanawake Wanaolea Watoto Bila Baba (Single Mother’s Tanzania), Hasner Mwinshehe anasema alibuni wazo hilo na kuliweka mtandaoni baada ya kupata mtoto miaka miwili iliyopita.

Mwinshehe akiwa binti wa miaka 23 tu anasema miaka miwili ilimfungua kujua changamoto mbalimbali wanazopitia wanawake katika malezi na ukubwa wake.

“Nilipata wazo la kuanzisha umoja huu baada ya kupitia changamoto mbalimbali, sikujua wazo langu lingepokelewa kwa ukubwa huu, katika muda mfupi tumejikuta katika jumuiya kubwa tukibadilishana uzoefu,” anasema Mwinshehe.

Anasema kuwa ndani ya umoja huo kumemfungua kujua kuwa wanawake hawa wana maisha yanayofanana kwa namna nyingi na hivyo kujikuta wakizungumza lugha moja.

“Kwa mfano changamoto zetu zinafanana, kati ya wanawake 120 tulioungana, labda 110 watakwambia wazazi wenzao hawataki kutoa matunzo ya watoto, na wengine watakwambia wazazi wenzao wamewakataa kabisa,” anasema Mwishehe.

Matatizo yao ni yapi?

Mbogo anasema malezi ya mtoto siyo magumu lakini mzazi mwenzake kugoma kutoa matunzo ya mtoto ni kikwazo katika maendeleo ya ukuaji wa mtoto.

“Kamwe siwezi kusema mtoto wangu ni mzigo lakini baba yake anapaswa kunisaidia gharama za mahitaji muhimu kama vile mavazi, madawa na chakula, cha kushangaza sasa hata ukienda Serikalini itaishia kumaliza nguvu zako bure,”

“Kwa kweli Serikali itusaidie tuondokane na hii hali, yaani ninakwenda kumshtaki mzazi mwenzangu halafu ninapewa barua nimpelee sijui anaitwa kwenye mashauri lakini asipoenda hachukuliwi hatua yoyote,” anasema Mbogo.

Mwishehe anasema utaratibu uliopo sasa unamkandamiza mwanamke kwa sababu wanaume hufanya wanavyotaka ikiwamo kudanganya kuhusu vipato vyao ili watoe fedha kidogo za matunzo ya mtoto.

Naye Mmakasa anasema sheria ibadilike, badala ya kumwamuru baba amletee mtoto peke yake, iseme na mama kwa kuwa muda mwingi anautumia kumlea mtoto na hivyo kupunguza nafasi ya kufanya kazi.

Husabaisha matatizo ya kisaikolojia

Mtaalamu wa Saikolojia na Uhusiano na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Chris Mauki hakuna madhara ya kiafya anayoweza kupata mtoto lakini inaweza kumtokea mzazi.

“Ni kweli kabisa malezi ya mzazi mmoja wakati wote ni yenye changamoto kwa mzazi mwenyewe. Utafiti ulioandikwa katika mojawapo ya makala za afya ya jamii umeonyesha kwamba kuna uwezekano mkubwa wa wanawake wanaolea watoto pasipo waume zao kupata changamoto za kiafya na kisaikolojia,

“Ingawa changamoto hizi zinaweza kutofautiana kutokana na maeneo au mazingira ya maisha wanayoishi. Baadhi ya changamoto hizi ni kama vile magonjwa na matatizo ya afya ya akili ambayo yanauwezekano mkubwa wa kusababisha ugonjwa wa sonona,” anasema Dk Mauki.

Anasema katika utafiti huo wanawake 25,000 kutoka nchi tofauti duniani waliulizwa maswali tofauti yakiwemo maswali yahusuyo hali zilivyokuwa ndoa zao, hali za watoto wao na changamoto za malezi wanazo kumbana nazo kila siku, sababu zinazokwamisha utendaji kazi wao wa kila siku. Wanawake hawa waliulizwa pia kuhusu hali za afya zao.

Ingawa utafiti huu ulihusisha wanawake wa nchi tofauti ulimwenguni, asilimia zaidi ya 38 wa nchi za Denmark na Sweden walionyesha kuanza malezi ya mzazi mmoja wakiwa chini ya miaka 50.

Asilimia zaidi ya 33 ya wanawake waishio nchini Marekani pia walielezea kuanza kuishi maisha ya malezi ya mzazi mmoja wakiwa chini ya miaka 50. Hali kama hii ilionekana kwa wanawake wa nchi za Uingereza kwa asilimia 22.

Kufuatia utafiti huo ilibainika kuwapo kwa uhusiano mkubwa baina ya malezi ya mzazi mmoja wa kike na kuongezeka kwa matatizo ya kiafya na kisaikolojia ukilinganisha na wanawake wanaowalea watoto wao wakisaidiana na waume zao.

Wanawake walioonyesha kuwa kwenye hatari kubwa ni wale walioanza malezi ya mzazi mmoja mapema zaidi, hususani wakiwa katika umri ya 20 au chini ya miaka 20.

Wengine ni wale walioendelea kulea watoto peke yao kwa zaidi ya miaka minane na wale wanaolea watoto wawili au zaidi ya wawili wakiwa peke yao, hapa namaanisha pasipo uwepo wa mzazi wa kiume.

Ukubwa wa matatizo haya umeonekana kutofautiana kutoka sehemu moja hadi nyingine. Kwa mfano, uhusiano baina ya malezi ya mzazi mmoja na matatizo ya kiafya na kisaikolojia yameonekana kuleta athari kidogo zaidi kwa wanawake wa nchi za Ulaya tofauti na wanawake wa nchi nyingine.

Hali ilionekana kuwa mbaya zaidi kwa wanawake wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, nchi zinazoendelea au nyingi zilizo maskini, ikiwamo Tanzania.

Mtaalamu Bella DePaulo ambaye daktari wa falsafa amesema kuwa baadhi ya wanawake wanaolea watoto peke yao wanaumizwa au kusumbuliwa na ule unyanyapaa “stigmatization” ya kwamba, ameachika, ameshindwa kuishi na mume, hajaolewa, aliza kabla ya ndoa, watoto wake wameharibika, atawezaje kulea mwenyewe na maswali yanayofanana na hayo.

Pamoja na tatizo hili ambalo limewaathiri wakina mama wengi kisaikolojia, bado wapo wanawake wachache walioweza kustahimili na kuishi wakiwa na furaha na kuwapa watoto wao pia.

Pamoja na kwamba athari za kisaikolojia zinaweza kuwakumba wanawake wengi, tena waishio katika maeneo tofauti ulimwenguni, tafiti zimeonyesha kuwa athari za kiafya zinasababishwa zaidi na tofauti za kipato.

Anasema kama wanawake wote wangeweza kuwa na kipato sawa, wale wanaoishi na watoto wao peke yao na wale wanaolea pamoja na waume zao basi athari za kiafya zingepungua kwa kiwango sawa au kutoonekana kabisa.

Tofauti na suala la athari za kiafya, unyanyapaa na athari zake zinaweza kumuathiri mama yeyote anayewalea watoto wake peke yake bila kujali ana uwezo au hana uwezo kifedha.