AJIRA&KAZI: Nyumba za ibada zinavyojenga kizazi cha watu wavivu nchini

Friday September 15 2017

Biblia inasema asiyefanya kazi na asile,

Biblia inasema asiyefanya kazi na asile, haikusema asiyeombewa na asile. Maombi yana umuhimu lakini waumini wanatakiwa wakumbushwe kumtumikia Mungu, kuanzisha biashara zao, kufanyakazi kwa bidii na kuwa na maadili. 

By Kelvin Mwita, Mwananchi

Asilimia kubwa ya Watanzania ni waumini wa dini na dhehebu fulani.

Idadi ya wanaoingia sehemu za ibada ni kubwa kuliko ile inayoingia shuleni na vyuoni.

Hii inatoa picha kuwa viongozi wa dini wananafasi kubwa ya kushawishi na kufanya mageuzi ya kifikra na kimtazamo.

Tanzania kama nchi nyingine zinazoendelea duniani, ina changamoto mbalimbali ikiwamo ya ukosefu wa ajira kutokana na ukweli kwamba Serikali inatoa nafasi chache zisizotosheleza mahitaji ya wanaotafuta ajira.

Pamoja na hayo, mmomonyoko wa maadili maeneo ya kazi pia ni changamoto ya muda mrefu huku rushwa ikitajwa kuwa moja ya matatizo makubwa nchini.

Hii imesababisha watu kuonewa na wengine kukosa haki na mahitaji yao ya msingi.

Nyumba za ibada zinaweza kuchangia katika kutengeneza kizazi cha wazembe na wavivu au wachapakazi na wenye juhudi.

Miujiza na mahubiri ya mafanikio

Sehemu kubwa ya mahubiri hasa makanisani yamekuwa ni ya kupata mafanikio ya fedha, nyumba, magari na vitu vingine vya thamani.

Wahubiri wanaegemea zaidi upande wa mambo ambayo waumini wao wanapenda kuyasikia.

 Mahubiri ya kuwataka wafanye kazi kwa bidii, waanzishe biashara na kutafuta mali kwa njia zilizo halali hayapewi nafasi kubwa.

Mchungaji Hosea Magelenga wa Kanisa la First Love Discipleship la jijini Dar er Salaam anakiri kuna tatizo katika mafundisho ya makanisani, kwani mengi  yanatengeneza kizazi kivivu na kizembe.

Mchungaji Hosea anasema wapo watu wanaoacha hata ajira zao kwa ushawishi wa wachungaji wanao watabiria mambo makubwa zaidi ya kile wanachopata kwenye ajira zao.

Anasema tamaa ya fedha na umaarufu kwa wachungaji wa baadhi ya madhehebu umesababisha mpaka waanze kutengeneza shuhuda za uongo za mafanikio na miujiza ili kuvuta waumini wengi katika makanisa yao.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro na Mkufunzi wa Dini ya Kislam, Bilal Ramadhani anasema misikiti haina shida kama ilivyo kwa makanisa mengi kuhusiana na mafundisho juu ya kufanya kazi kwa bidii.

Anasema Mtume Muhamad pamoja na mitume wengine walikuwa wakifanya kazi na wengine walikuwa wafanyabiashara.

Lakini anasema nguzo ya tatu ya Uislam inahusu zaka na hauwezi kutoa zaka kama haujafanya kazi na kupata kipato halali.

Anasisitiza Sala pekee haitoshi kukuongezea kipato bila kuvuja jasho na mafundisho misikitini huegemea zaidi kwenye juhudu ya kazi ili mtu ajipatie kipato.

Hassan Mnyone, muumini wa Dini ya Kiislam anasema kuna aya nyingi kwenye Msaafu ambazo zihimiza watu kufanya kazi.

Mnyone ametolea mfano Surat Al-Jumua: Ayat 10 inaeleza wazi:  “Na itakapokwisha sala, tawanyikeni katika ardhi mtafute fadhila za Mwenyezi Mungu na  mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi (ili msipate kufanya mabaya), ili mpate kufaulu”.

Anaongeza kuwa Dini ya Kiislam inapinga njia za mkato za kupata fedha hivyo ni vema watu kuvuja jasho ili kupata kipato halali.

Padri, Calistus Msuri wa Jimbo Katoliki la Moshi anasema tabia ya wahubiri wengi kutoa mahubiri yanayoweza kusababisha watu kutozingatia bidii ya kufanya kazi yanatokana na sababu kuu mbili.

Mosi, kuwa na wahubiri watafuta fursa za kujipatia kipato, hivyo kuacha kuhubiri misingi mingine ya kiimani na kuhubiri kile waumini wanachotaka kukisikia ili wawashawishi kutoa fedha zinazonufaisha mahubiri na kuwatajirisha huku waumini wakibaki na ufukara.

Sababu nyingine ni wahubiri kutokuwa na elimu ya kutosha ya teolojia.

Anasema Kanisa Katoliki limejiwekea mfumo mzuri wa kupata wahubiri wake wanaozingatia taaluma na weeledi.

Anasema kuna baadhi ya makanisa hasa ya kipentekosti yanaanzishwa na watu wasio na elimu ya kutosha ihusuyo teolojia.

Hata hivyo, padri huyo anasema  hali hiyo inasababisha makanisa yawe ya kibiashara zaidi badala ya  kiimani.

“Biblia inasema asiyefanya kazi na asile, haikusema asiyeombewa na asile. Maombi yana umuhimu lakini waumini wanatakiwa wakumbushwe kumtumikia Mungu, kuanzisha biashara zao, kufanyakazi kwa bidii na kuwa na maadili.”

“Haya ni mambo ya kiroho, lakini yapo makanisa mengi yanawataka waumini watoe fedha ili wapate miujiza ya fedha, kazi, magari, nyumba, ndoa na menginyeyo, hii si sahihi,” anasisitiza Padri Msuri.

Nini Kifanyike?

Nyumba za ibada zina nafasi kubwa ya kufanya mabadiliko ya kifikra kwa jamii.

Ni vema viongozi wa dini wakahakikisha pamoja na maombi, waumini wao wanahamasishwa kuchukua hatua za kufanya shughuli mbali mbali zinazoweza kuwaingizia au kuwaongezea kipato.

Siyo kitu cha ajabu wala cha kushangaza kwa nyumba za ibada kuratibu semina kwa waumini wao zenye lengo la kuwaongezea maarifa ya jinsi ya kuongeza vipato vyao kupitia biashara na ujasiriamali.

Hii itaonyesha zinajali maendeleo ya kimwili na kiroho ya waumini wao.

Yapo makanisa nchini yaliyoamua kuwaiunua waumini wao kwa kufungua vyama vya Akiba na Mikopo (Saccos) na kuendesha mafunzo ya ujasirimali ili waweze kuwa na maendeleo ya kiuchumi.

Hakuna imani yoyote ya dini inayoruhusu uvivu na uzembe; wahubiri watumie fursa ya kuwa na ushawishi kwa jamii, kwa kukemea uzembe, uvivu na matendo mengine yanayosababisha mmomonyoko wa maadili kuliko kuhubiri miujiza pekee.

Waumini nao wawe makini na kujua wapo viongozi wa dini wanaoutumia mianya ya umasikini, ukosefu wa ajira na matatizo mengine kama fursa ya kujiongezea umaarufu na kujitajirisha.

Pamoja na umuhimu wa sala na maombezi katika kutatua changamoto, bidii nayo inanafasi kubwa katika kutatua changamoto. Hakuna haja ya kubweteka nyumbani ukisubiri muujiza wa fedha wakati una nguvu, uwezo, rasilimali na maarifa.

Kelvin Mwita ni Mhadhiri Msaidizi Chuo Kikuu Mzumbe, 0659 081838, [email protected], www.kelvinmwita.com

Advertisement