Oktoba Mosi: Maandamano ya Ukuta au kupanda miti?

Wakazi wa Uvinza mkoani Kigoma wakifuatilia mkutano wa Chadema uliofanyika katika eneo la Polisi Nguruka wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana. Picha ya Maktaba

Muktasari:

Hii maana yake ni kwamba viongozi wa dini hawaoni tena umuhimu wa kuingilia kati ‘nongwa’ za wanasiasa kukamiana au wanafanya juhudi zao upande mmoja (ule wa Serikali na CCM) maana hatujasikia tena vikao baina yao na viongozi wa upinzani.

Oktoba Mosi ni siku ambayo viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliahidi kufanya maandamano waliyoyaita ya Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta) baada ya kuahirisha Septemba Mosi kufuatia juhudi za viongozi wa dini.

Ikiwa imebakia wiki moja sasa, hatuoni pilikapilika za viongozi wa dini kuhakikisha nchi yetu itabaki kuwa tulivu siku hiyo wala hatusikii kauli zile za ‘mikwara’ zilizokithiri kila kukicha kadri siku zilivyokaribia Septemba Mosi.

Hii maana yake ni kwamba viongozi wa dini hawaoni tena umuhimu wa kuingilia kati ‘nongwa’ za wanasiasa kukamiana au wanafanya juhudi zao upande mmoja (ule wa Serikali na CCM) maana hatujasikia tena vikao baina yao na viongozi wa upinzani.

Sambamba na Oktoba Mosi kuainishwa kama siku ya maandamano ya Ukuta wa Chadema, Serikali nayo ilitangaza tarehe hiyo itakuwa ya kupanda miti nchini ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

Hebu piga picha, kule wanafanya maandamano ya ‘kupinga kuminywa kwa demokrasia nchini’ na huku wanapanda miti. Je, yote mawili yanaweza kufanyika siku moja?

Ni wazi kuwa Serikali ilitoa amri ya kupiga marufuku maandamano hayo na polisi kuonya watawashughulikia wale wote watakaokaidi amri hiyo.

Ndiyo maana nauliza, Oktoba Mosi ni maandamano au kupanda miti? Maandamano yanayohusu malalamiko ya vyama vya upinzani kuhusu marufuku ya Rais John Magufuli kuhusu mikutano ya kisiasa hadi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Anadai huu ni wakati wa kuchapa kazi, ‘Hapa Kazi Tu’ na siyo wakati wa kuendeleza siasa. Wapinzani wanasema kufanya siasa katika nchi ya kidemokrasia ni haki yao kikatiba na kibinadamu. Mwamuzi ni nani wa kuondoa mzozo huu?

Hivi karibuni tumeshuhudia vurugu zinazoendelea kule Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kuuawa watu 50 kufuatia malalamko ya wapinzani wa Rais Joseph Kabila kumtuhumu anafanya njama za kung’ang’ania kubaki madarakani kama Pierre Nkrunziza wa Burundi.

Zimbambwe na Afrika ya Kusini nako hali si shwari, maandamano mtindo mmoja. Yote haya wananchi wanadai Serikali za nchi hizo kuminya demokrasia.

Siyo Chadema wanaotishia kukabiliana na marufuku ya JPM ya kuzuia mikutano ya kisiasa. Hivi karibuni chama cha ACT-Wazalendo kilitangaza kufanya Mkutano Mkuu wa Demokrasia Septemba 24 mwaka huu na kuhusisha wanachama, wadau wa siasa na wananchi  kujadili masuala mbalimbali ya nchi.

Chama hicho kilitangaza kufanya mkutano huo licha ya Jeshi la Polisi kupiga marufuku mikutano yote ya inayohusu masuala ya siasa kwa kile kilichoelezwa kuwa inaleta uchochezi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya chama hicho Dar es Salaam wiki iliyopita, Katibu wa Itikadi Uenezi na Mawasiliano, Ado Shaibu alisema mkutano huo ni utekelezaji wa Katiba ya chama na   hautajali kuwapo   zuio aliloliita batili.

Mkwamo wa kisiasa na madhara yake

Mkwamo wa kisiasa ni hali ambayo huikumba nchi panapokosekana mwafaka kuhusu jambo fulani la kisiasa.

Katika nchi za kidemokrasia ni jambo la kawaida ambalo hupelekea watu wenye kujali masilahi ya nchi zao kukaa chini na kutanzua mkwamo huo kwa masilahi ya Taifa.

Katika nchi zilizokomaa kidemokrasia, kwa kutambua kutokuepukika kwa hali hii kutokea pamewekwa hata miundombinu ya kisiasa ya kuwezesha kukwamuliwa mkwamo wa kisiasa unapotokea bila kuleta madhara.

Katika nchi changa kidemokrasia kukosekana kwa miundombinu kama hiyo ni tatizo kubwa kiasi kwamba hata mkwamo mdogo wa kisiasa unaweza kuilipua nchi, mfano mzuri Burundi na sasa DRC.

Zambia na Uganda wanayo miundo mbinu ya angalau ‘kuahirisha’ kama siyo kuepusha mikwamo ya kisiasa. Katika nchi hizo mbili, wapinzani walipinga matokeo ya uchaguzi wa marais.

Kilichotokea ni wapinzani kufungua kesi kupinga matokeo ya urais katika mahakama za katiba ya nchi hizo. Uamuzi wa mahakama hizo ukatoka na urais wa Yoweri Museveni wa Uganda na ule wa Edgar Lungu kwa Zambia ukathibitishwa.

Nchi yetu kwa sasa inapitia kipindi cha mkwamo wa kisiasa ambao kwa mujibu wa andiko ‘Causes and Consequences of Polarization’ ni kila upande kushikilia msimamo wake pasipo na kutaka kufikia mwafaka.

Kukosekana kwa miundombinu ya kukwamua mikwamo ya kisiasa kunathibitishwa na kitendo cha viongozi wa dini kuwa wasuluhishi wa mgogoro uliojitokeza kati ya vyama vya upinzani na Serikali.

Huu ni udhaifu wa mfumo mzima wa kisiasa nchini unaotokana na kuingia kwa  vyama vingi kwa ajili ya kuwaridhisha wakubwa wa dunia wakati watawala hawakuwa tayari.

Kwa mujibu wa andiko nililolitaja hapo juu, moja ya sababu za viongozi wa vyama vya upinzani kuwa na ari ya kuikabili Serikali ni uwapo wa wapigakura wasioridhika na jinsi kampeni, upigaji kura na matokeo yalivyotolewa hadi kutangazwa washindi.

Sababu nyingine ni chama tawala kutaka kudhibiti hali ya ushawishi wa kisiasa kwa kuhofia kupoteza ushindi uchaguzi ujao. Hii ndiyo sababu kubwa ya kuzuia mikutano na shughuli za kisiasa za vyama vya upinzani.

Chama chenye wabunge wengi hufanya mbinu za kudhibiti hata mjadala bungeni kwa lengo la kulinda masilahi ya chama. Tanzania inahitaji mabadiliko ya dhati kisiasa kupitia Katiba mpya, vinginevyo mwendo wa maandamano hautakwisha.

Kutegemea njia za ‘zimamoto’ kutanzua mikwamo ya kisiasa ni sawa na kusubiri meli uwanja wa ndege, kamwe meli haitafika uwanja wa ndege. Kuwaingiza viongozi wa dini katika minyukano ya kisiasa ya vyama ni kuwaweka majaribuni.

Nani atalaumiwa siku viongozi hawa wa dini watakapobadilika na kuwa wanasiasa kwelikweli? Wakati tukielekea Oktoba Mosi, ni vyema tukajiuliza kama Taifa, ni kipi kina masilahi na sisi kati ya maandamano na kupanda miti?

Ni wazi kila moja kati ya kampeni hizi mbili,  ile ya Ukuta iliyotangazwa na Chadema na ile ya kupanda miti iliyotangazwa na Serikali ya CCM zinaweza kufanyika Oktoba Mosi.

Kwa maoni yangu kampeni yenye masilahi na kila Mtanzania bila kujali itikadi yake kisiasa, dini, rangi, jinsia wala kabila ni ya kupanda miti. Ningekuwa na uwezo kampeni hii ndiyo ningehakikisha inatekelezwa.

Katika kampeni ya kupanda miti hakuna damu itakayomwagika labda kwa bahati mbaya mtu akijikata na jembe au kifaa cha kupandia miti na wala nchi haitakuwa katika tahadhari kama ile ya maandamano.

Hatuwezi kufika huko kama bado kuna mkwamo wa kisiasa kati ya vyama vya upinzani na Serikali. Ni wazi mkwamo huu umetokana na kauli ya JPM kupiga marufuku mikutano ya kisiasa.

Mkwamo huu ulikuja kwa kauli ya JPM na utaondoka kwa kauli yake ya kuruhusu tena shughuli za kisiasa za vyama vya siasa ambazo ziko kikatiba na kisheria kupitia sheria ya vyama vya uchaguzi.

Kwa upande wa vyama vya upinzani, hivi jamani bila maadamano hakuna njia mbadala za kupinga hicho mnachokipinga?

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii, anapatikana kwa barua pepe: [email protected]