Omary Banda hataki kuzisikia Simba wala Yanga

Muktasari:

  • Dogo huyo, 16, ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto watano ya nguli wa zamani wa Simba, Banda ambaye aliichezea timu hiyo mwishoni mwa miaka ya tisini.

Omary Banda ni mchezaji kinda anayechipukia kwenye Kituo cha Azam mwenye ndoto za kufuata nyayo za kaka yake, Abdi Banda anayecheza Baroka FC ya Afrika Kusini.

Dogo huyo, 16, ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto watano ya nguli wa zamani wa Simba, Banda ambaye aliichezea timu hiyo mwishoni mwa miaka ya tisini.

Omary alizaliwa mkoani Tanga anadai alikuja kumtembelea kaka yake jijini hapa na kisha kuanza kimya kimya harakati za kujitafutia timu ya kuichezea ndipo akabahatika kujiunga na Kituo cha Azam.

“Ninacheza namba sita, kaka yangu yeye ni beki wa kati japo na mimi ninaweza pia kucheza kwenye hiyo nafasi.

“Lakini kabla ya kuja Dar nilikuwa nikicheza kwenye kituo cha kulelea vipaji cha Fairplay cha kule kule Tanga, msimu uliopita ndiyo nilipata nafasi Azam,” anasema.

Hata hivyo Omary hakusita kwa kusema anatamani siku moja kucheza soka la kulipwa kama ilivyo kwa kaka yake na kudai hata hana mawazo ya kuzichezea Simba na Yanga.

“Bado ninahitaji muda wa kuendelea kufundishwa mpira ila muda utakapofika wa kucheza mpira kwenye kiwango cha ushindani, nitafurahi kama nitafikia hatua ya kucheza nje ya nchi.

“Naongea mara kwa mara na kaka ambaye yupo Afrika Kusini, huwa ananitaka nisikilize kwa makini yale yote ambayo ninafundishwa kwenye hiki kituo cha Azam ili siku za usoni nije kuwa mchezaji mkubwa.

“Kuhusu kucheza nje amekuwa akiniambia ni kitu kinachowezekana hasa kutokana na kipindi hiki kuwa na nafasi za kutosha ambazo zinaendelea kutengenezwa na wachezaji kadhaa wa kitanzania wanaofanya vizuri katika mataifa yaliyoendelea,” anasema Omary.

Mdogo huyo wa Banda amezitaja ligi tatu anazozitamani kwa Afrika ni Ligi Kuu Afrika Kusini ‘PSL’, Morocco ‘Batola Pro’ na Ligi Kuu ya Misri.