Ongezeko la hoteli kwenye fukwe za Zanzibar la nini?

Muktasari:

  • Hapo tena hubakia nikijiuliza maswali mengi bila jawabu ya kuniridhisha juu ya jinsi hao waliofanya ujenzi huo hawakuwa na fikra na je, hakuna taasisi ya Serikali iliyoweza kuzuia ujenzi huo ambao haukubaliki kimazingira na kisheria duniani?

Ninapotembelea vijiji mbalimbali vya Zanzibar vilivyopo karibu na bahari huwa nashangazwa na nyumba za kulala wageni, hoteli na kumbi za starehe zilivyojengwa pembezoni mwa ufukwe wa bahari.

Hapo tena hubakia nikijiuliza maswali mengi bila jawabu ya kuniridhisha juu ya jinsi hao waliofanya ujenzi huo hawakuwa na fikra na je, hakuna taasisi ya Serikali iliyoweza kuzuia ujenzi huo ambao haukubaliki kimazingira na kisheria duniani?

Kinachoonekana katika sehemu nyingi ni kama vile yapo mashindano Unguja na Pemba ya kuharibu mazingira ya bahari na kuwazibia wavuvi na watu wengine njia za kwenda na kurudi kutoka pwani.

Wakati fulani utasikia maofisa wa mazingira wakizuia ujenzi wa hoteli za kitalii au nyumba pembezoni mwa ufukwe wa bahari, lakini baada ya muda utaona jengo limekamilika kama vile hapakuwapo hatua ya kuzuia ujenzi.

Hapa unaona wazi kwamba ama sheria za kuhifadhi mazingira ya bahari hazifuatwi kwa sababu mbalimbali au wasimamizi wa sheria hizo hawako makini.

Wakati mwingine utaona kazi ya ujenzi wa hoteli unaendelea kwa mwaka au zaidi na baadaye ndio unasikia umesimamishwa.

Hapa inafaa kujiuliza, hawa wanaoitwa wakaguzi wa ujenzi au masheha ambao ni wawakilishiwa wa Serikali katika mitaa na vijiji wanakuwa wapi hata ujenzi huo ukaendelea kwa muda wote bila ya kusimamishwa?

Tatizo hapa ni kwamba wanaokiuka hizi sheria hawawajibishwi na wenye mahoteli hayo wanaelewa kwamba hata wakisimamishwa kujenga baadaye wataambiwa basi endeleeni.

Miaka michache iliyopita ujenzi wa hoteli moja iliyopo Pemba ulikuwa umekamilika na kusubiri kufunguliwa rasmi, ndio tukasikia ujenzi umesimamishwa. Huu ni uzembe wa hali ya juu.

Kilichokuwa wazi na hakina ubishi ni kwamba baadhi ya wamiliki wa hizi hoteli na mabwana wakubwa wenye fedha, wanaonekana kuringia uwezo wao wa kifedha na hivyo kuamua kufanya watakavyo.

Ujenzi wa aina hii upo katika vijiji vingi vilivyopo kwenye fukwe za bahari za Unguja na Pemba na inaonekana pamejengeka utamaduni unaokua kwa kasi wa wafanya biashara kutojali mazingira ya fukwe za bahari.

Si jambo la ajabu kuona wanaovunja sheria wanasamehewa ati kwa kisingizio cha kwamba si vizuri kuwabughudhi wawekezaji. Kuwapa watu hawa heshima ya kuwa wawekezaji si sahihi kwani hawa ni wavurugaji.

Watu wa aina hii hawasaidii hata kidogo kuchangia maendeleo ya nchi na badala yake wanatuharibia. Si vizuri kuwavumilia hata kidogo.

Ni vizuri Serikali ikakataa katakata wawekezaji wa kutupanda vichwani na kufanya mambo yanayotuharibia bahari na kusumbua wananchi, hasa wavuvi.

Kwa jinsi walivyokuwa na jeuri na kibri, baadhi ya hawa wawekezaji wenye mahoteli makubwa wameamua hata kuajiri wafanyakazi bila ya mikataba ya kazi na wafanyakazi wamekuwa wakibadilishwa kama nguo ili pasiwepo malipo ya mafao.

Kwa bahati mbaya Idara ya Kazi inaonekana haifuatilii kwa umakini suala hili na hata wafanyakazi wanapotoa malalamiko, huoni madai yao kushughulikiwa.

Pengine ndiyo sababu kukawapo lawama na minong’ono ambayo sina uhakika nayo ati kuna watu wenye mamlaka wanaokula sahani moja na wawekezaji.

Mara nyingi pia tumesikia mazingira machafu ya kazi na udhalilishaji hasa wa akina dada katika baadhi ya hizi hoteli. Mambo yanayofanyika ni kinyume cha sheria na hayakubaliki katika mila, utamaduni na desturi za watu wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Nimetolea mfano mara nyingi tukio la kishenzi lilioelezwa ndani ya Baraza la Wawakilishi la mmiliki mmoja wa hoteli alivyojiamini na kuwa na jeuri na kibri cha kulazimisha wasichana wanaohudumia hapo wavae nguo fupi na nyepesi.

Sababu ya kutolewa maelekezo hayo ati upepo mwanana wa bahari ukivuma nguo zao zitapeperuka na kuwafurahisha watalii watakapoona maumbile ya ndani ya mwanamke wa Zanzibar.

Huu ni uhuni na ushenzi na ningelitarajia waliohusika wangewajibishwa ili iwe somo kwa wengine wanaotaka kugeuza wasichana wa Tanzania kuwa watumwa mamboleo walioajiriwa kuonyesha maungo yao ya ndani.

Lakini, kwa bahati mbaya yule mwekezaji aliyetoa amri ile hakuguswa na ungelitarajia sheria kumuandama na kumsweka jela kama alivyofanya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwa mwekzaji jeuri wa Kigiriki aliyesema nchi yetu ilikuwa mfukoni mwake.

Ni kweli nchi yetu ni maskini, lakini watu wake ni tajiri katika kulinda utu na heshima yao.

Mara nyingi, pamoja na waandishi wengine wa habari tumekuwa tukifuatilia malalamiko mengi yanayotolewa juu ya mwenendo wa baadhi ya hoteli za kitalii ziliopo Zanzibar. Tunachogundua ni kukithiri vitendo vya kihuni katika baadhi ya sehemu na wamiliki na viongozi wa hoteli hawaguswi.

Kwa mara nyingine nasema kwa kinywa kipana kuomba Serikali na taasisi zake za kisheria kuchukua hatua madhubuti za kulinda fukwe zetu za bahari ambazo zinachafuliwa kila siku na kusimamia sheria za kazi ili utalii usiwe sekta ya kutupotezea heshima yetu na utamaduni wetu.

Huu mtindo wa baadhi ya wageni na hata wenyeji, kutokana na kuwa na fedha nyingi, kutupanda vichwani na kufanya watakavyo lazima ukomeshwe na tuseme sasa basi.

Wageni wanaoitaka kufanya uhuni wafanye huko kwao walikotoka na wakija hapa kwetu waishi na kufanya kazi kwa heshima na adabu. Fedha zao zisiwe juu ya sheria za nchi yetu.

Tusikubali hata kidogo kwa mtu yeyote yule, mwenyeji au mgeni, kutumia vibaya upole na ukarimu wetu.

Tuwaheshimu wanaojiheshimu na tuwafunze kujiheshimu wawekezaji wasiokuwa na heshima.