Ongezeko la watu ni fursa ya kuharakisha maendeleo

Watu wengi wamekuwa wakimiminika kupata mahitaji katika soko la Kariakoo jijini Dar esSalaam lakini bidhaa nyingi zinazouzwa zinatoka nje ya nchi. Wawekezaji wa hapa nchini bado hawajagundua kuwa hii ni fursa wanayoweza kuitumia ili kupata faida kubwa. Picha ya Maktaba.

Muktasari:

Takwimu za Umoja wa Mataifa (UN) zinaonyesha kuwa China ndiyo nchi inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu duniani ikiwa na wastani wa watu zaidi ya bilioni 1.3. Licha ya kuwa na idadi hiyo, taifa hilo limekuwa moja ya yale yanayoongoza kwa kuwa na uchumi uliokomaa. China kwa sasa ni tishio kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia mbele ya mataifa ya Magharibi.

 Suala la ongezeko la watu limekuwa gumzo duniani kote na kumekuwa na hisia tofauti kama ongezeko hilo la watu lina athari hasi au chanya katika maendeleo. Makala haya itajaribu kuchanganua namna Tanzania inavyoweza kutumia ongezeko la watu kama fursa ya kuharakisha maendeleo na kukuza uchumi wa taifa.

Takwimu za Umoja wa Mataifa (UN) zinaonyesha kuwa China ndiyo nchi inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu duniani ikiwa na wastani wa watu zaidi ya bilioni 1.3. Licha ya kuwa na idadi hiyo, taifa hilo limekuwa moja ya yale yanayoongoza kwa kuwa na uchumi uliokomaa. China kwa sasa ni tishio kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia mbele ya mataifa ya Magharibi.

Vita baridi ya kiuchumi baina ya China kwa upande mmoja dhidi ya Marekani na washirika wake kwa upande wa pili, inadhihirisha kwamba, kumbe kuwa na idadi kubwa ya watu, siyo kikwazo katika maendeleo ya taifa lolote duniani, bali kikwazo ni namna idadi hiyo ya watu inavyotumika katika uzalishaji na kuwa fursa ya maendeleo.

Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile, ni mmoja kati ya wanaharakati wa masuala ya idadi ya watu. Wakati akizungumzia suala hili la idadi ya watu, anasema taifa lolote lisipojiandaa, linaweza kujikuta likiwa na matokeo hasi yanayoletwa na ongezeko la watu. 

       “Ongezeko la watu siyo jambo baya hata kidogo. Lakini unalitumiaje hilo ongezeko la watu, hapo ndipo penye tatizo na hatimaye unaweza kujikuta ukilalamika kuwa idadi kubwa ya watu ni kikwazo kwa maendeleo,” anasema Dk Ndugulile.

Ni kwa namna gani basi kama taifa tunaweza kutumia ongezeko la watu ili kupata matokeo chanya? Mchumi mmoja kutoka Asasi Isiyo ya Kiserikali ya DSW, Steven Mlali, anasema jambo la msingi ni kuangalia fursa zinazopatikana nchini na kuzitumia ipasavyo kwa ajili ya kuleta maendeleo.

“Wenzetu China wanaitumia idadi kubwa ya watu kwanza kama nguvu kazi katika uzalishaji. Wana viwanda vingi vidogo na vikubwa na wanatumia watu wao wenyewe katika viwanda hivyo ili kuzalisha bidhaa mbalimbali,” anasema Mlali.

Pia, China imekuwa mzalishaji mkubwa wa bidhaa nyingine zikiwamo za mashambani zitokanazo na kilimo, ufugaji na hata uvuvi.

Uzalishaji wote unaofanywa unalenga wateja ama watumiaji wa ndani na nje ya nchi hiyo. Hapo ndipo linapokuja suala jingine la kutumia idadi kubwa ya watu kama fursa ya masoko kwa bidhaa zinazozalishwa.

Unapokuwa na idadi kubwa ya watu, ndivyo uhitaji wa bidhaa mbalimbali nao unavyoongezeka. Wachumi hutumia falsafa yao kwamba kunapokuwa na mahitaji makubwa ya bidhaa sokoni, bei ya bidhaa hupanda na kulazimisha uzalishaji kuongezeka kwa lengo la kukidhi mahitaji ya soko husika na kupata faida zaidi.

Mlali anasema China inatumia watu wake zaidi ya bilioni moja kama soko la kwanza la bidhaa wanazozalisha ndani ya nchi.

“Wanaofanya kazi za viwandani, wanahitaji chakula na ndipo hapo wanapohitaji bidhaa zilizozalishwa na wakulima ili kukidhi mahitaji yao.

“Ukichukua watu bilioni 1.3, hili ni soko kubwa sana ambalo likitumika ipasavyo, matokeo yake kwenye nchi ni makubwa na uchumi lazima utakuwa kwa kasi kubwa. China wametumia soko lao ‘effectively’ (kikamilifu) kwa muda mrefu na ndiyo maana taifa hilo haliyumbishwi hata kidogo na wababe kama Marekani na washirika wake,” anafafanua Mlali.

Tanzania kwa sasa ina watu milioni 45, kwa mujibu wa Sensa ya idadi ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2012.

Wapo ambao wamekuwa wakiona kama idadi hiyo ya watu na kwa kadiri ongezeko linavyozidi kupaa, huenda ikawa kubwa na yenye matokeo hasi miaka ijayo.

Lakini ukichukulia mtazamo wa Dk Ndugulile pamoja na Mlali, ni wazi kwamba Tanzania tunaweza kulitumia ongezeko hilo la watu kwa kuharakisha maendeleo. Jambo la msingi hapa ni mipango ipi tuliyojiwekea na tunaitekelezaje.

Endapo Tanzania itakuwa nchi ya viwanda katika kipindi cha miaka mitano ijayo kama zilivyo ndoto za Serikali ya Awamu ya Tano, hakutakuwa na tatizo la ukosefu wa wafanyakazi kwenye viwanda vyetu hivi na hivyo hatutahitaji kuagiza nguvukazi kutoka nje ya nchi.

Zipo nchi kadhaa duniani ambazo hulazimika kuagiza nguvukazi kutoka nje kwa ajili ya sekta mbalimbali kama yalivyo mataifa ya Kiarabu. Kwetu, hatutakuwa na tatizo hilo.

Uzalishaji kutoka katika viwanda vyetu na hata sekta nyinginezo kama kilimo, uvuvi na ufugaji, unaweza kuleta bidhaa ambazo zina uhitaji ndani na hata nje ya nchi.

Taifa linaloweza kuzalisha bidhaa za kutosheleza mahitaji ya ndani bila kuhitaji kuagiza kutoka nje. Ni wazi kwamba uchumi wake utakuwa kwa kasi huku sekta za uzalishaji kama viwanda zikiimarika.

Idadi kubwa ya Watanzania inaweza kutumika kama soko la kwanza kwa bidhaa zetu zitakazotoka kwenye viwanda vyetu vya ndani. Uhakika wa kuwapo kwa soko hili ni mwanzo wa ustawi mzuri wa viwanda hivyo na chachu ya kuongeza uzalishaji.

Hebu tuchukue mfano wa mahitaji ya nguo ama viatu hapa Tanzania. Bidhaa hizi zinahitajika kwa kila Mtanzania. Tunalima pamba kwa wingi huku tukiwa wazalishaji wazuri wa ngozi itokanayo na mifugo tuliyonayo.

Endapo tungekuwa na viwanda vya kutosha vya nguo na viatu, vinavyozalisha bidhaa zenye ubora unaotakiwa, leo tusingehangaika kuagiza mitumba ya nguo na viatu nje nchi. Viwanda vyetu vingekuwa na uhakika wa soko la ndani na vingeendelea kuimarika siku baada ya siku huku kukitengezwa pia ajira kwa Watanzania.

Katika maelezo yake, Dk Ndugulile, anashauri wadau wote wa maendeleo kutumia suala la idadi ya watu kama fursa ya kuweza kuinua uchumi wetu na kuharakisha maendeleo ya Taifa.

Harakati hizo zimekuwa zikifanywa pia na mtandao wa asasi zinazojihusisha Idadi ya Watu na Maendeleo ya Tanzania (TCDAA), mtandao ambao umekuwa ukiiasa Serikali kuwa makini na suala hili la idadi ya watu ili liendane na mipango ya maendeleo katika nchi.

Endapo tutaitumia vyema idadi ya watu waliopo nchini, upo uwezekano wa kupata matokeo chanya ambayo yatasaidia kukuza uchumi wa taifa.