Operesheni ya polisi iungwe mkono lakini…

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga

Muktasari:

Operesheni hiyo ya polisi imekuja huku kukiripotiwa kuwa ajali nyingi zimekuwa zikisababishwa na matumizi ya taa hizo hasa nyakati za usiku.

Jeshi la polisi nchini limeanza operesheni maalumu ya kuziondoa taa za ziada zenye mwanga mkali (spotlight) ambazo huwekwa kwenye baadhi ya magari bila kufuata utaratibu.

Operesheni hiyo ya polisi imekuja huku kukiripotiwa kuwa ajali nyingi zimekuwa zikisababishwa na matumizi ya taa hizo hasa nyakati za usiku.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga amekaririwa wiki hii akisema kuwa kulikuwa na ajali 104 mwaka 2015 na nyingine 123 mwaka jana, ambazo zilisababishwa na matumizi ya taa hizo.

Mpinga amesema taa hizo hutumika vibaya nyakati za usiku na kuwa chanzo cha ajali kwa sababu zinapotumika hupoteza uwezo wa mtumiaji kuzitawala kwa maana ya kubadilisha uwakaji wake.

Mpaka Jumatatu wiki hii, tayari taa hizo za ziada 665 zilikuwa zimeondolewa katika magari mbalimbali na operesheni hiyo bado inaendelea maeneo mbalimbali nchini.

Hatuna budi kulipongeza jeshi la polisi kutokana na operesheni hiyo kwa sababu kwa kufanya hivyo litasaidia kupunguza ajali zitokanazo na mwanga mkali wa taa hizo.

Baadhi ya madereva au wamiliki wa magari wamekuwa wakiweka taa hizo za ziada bila sababu za msingi na wengine hufanya hivyo kwa sababu ya mashindano na wenzao.

Matokeo yake ni madhara makubwa kwa madereva wa magari mengine ambao hujikuta wakishindwa kuona mbele kwa sababu ya kupigwa na mwanga mkali hivyo kupoteza mwelekeo na kupata ajali.

Watu wengi wamefariki dunia kwa sababu ya ajali zilizosababishwa na mwanga mkali wa taa za magari wanayopishana nayo jambo ambalo limeacha simanzi kwa familia zilizopoteza ndugu zao.

Ikumbukwe kuwa mtu anapofariki dunia huacha si tu simanzi, lakini watoto ambao hulazimika hata kuacha shule kutokana na kukosa ada baada ya mlezi wao kufariki.

Familia inayopoteza mlezi hukosa mwelekeo na matarajio waliyokuwa nayo hupotea kabisa badala yake maisha hugeuka kuwa ya tabu na kwa namna fulani matarajio mazuri waliyokuwa hupotea kabisa.

Lakini, kama kila mmoja angetambua thamani ya maisha, angeheshimu maisha ya mwingine, na kwa kufanya hivyo mambo yanayosababisha vifo yangepungua pia.

Kila mmoja anapaswa kutambua kuwa kuweka taa za nyongeza katika magari ni sawa na kusababisha vifo kwa watu wengine wasio na hatia.

Kwa kutambua hilo ndiyo maana tunawapongeza polisi kwa operesheni hiyo inayofanyika nchini kote, kwani tunaamini itapunguza ajali kwa namna fulani.

Hata hivyo, tunashauri Jeshi la Polisi lifanye operesheni hiyo kwa kuzingatia maadili, busara na utu, badala ya kuziondoa kibabe na kusababisha uharibifu wa magari husika.

Tunatambua kuwa baadhi ya magari yana taa hizo za nyongeza kutoka yalikonunuliwa ama Japan au nchi nyingine za Ulaya, hivyo inakuwa ngumu kuzitoa kirahisi.

Mtindo wa Jeshi la Polisi hasa katika jiji la Dar es Salaam kukaa na mafundi wa magari barabarani ni mzuri, lakini kwa upande moja una changamoto zake.

Mmoja ya changamoto ni mafundi hao kutokuwa na uwezo wa kuzitoa taa ambazo zimekuja moja kwa moja na gari lenyewe. Wakati mwingine mafundi hao hujikuta wakilazimisha kuziondoa na kuharibu mfumo wa umeme wa gari.

Ni vyema kunapokuwa na changamoto yoyote katika kuzitoa taa hizo kuwe na njia nyingine ya kufanya ikiwezekana hata kulipeleka gari katika gereji kubwa kuzitoa kuliko kuharibu gari.

Tunaamini kuwa katika kila kazi si rahisi kukosa changamoto, lakini polisi wanapaswa kupunguza malalamiko ya watu kuliko kuyaongeza kwa namna yoyote ile.