Oxford: Tunaridhika na msaada wa Serikali sekta ya vitabu

Meneja wa kampuni ya uchapishaji vitabu ya Chuo Kikuu cha Oxford, Fatuma Shangazi (kushoto), akikabidhi vitabu vilivyochapishwa na kampuni yake  kwa mmoja wa wanafunzi. Na Mpigapicha Wetu

Muktasari:

Mwalimu anachomoa maarifa kutoka kwenye vitabu mbalimbali, mwanafunzi naye anapokea maarifa kutoka kwa mwalimu.

Sekta ya uchapishaji wa vitabu ina mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu nchini. Kwa muda mrefu kampuni binafsi za uchapishaji vitabu, zimekuwa mhimili mkubwa wa kuisaidia Serikali katika azma yake ya kusimamia sekta ya elimu.

Katika makala haya, mwandishi wetu amefanya mahojiano na Meneja wa kampuni ya Uchapishaji ya Chuo Kikuu cha Oxford, Fatuma Shangazi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya uchapishaji vitabu nchini.

Swali: Ipi historia yenu ya kufanya kazi Tanzania?

Jibu: Kwa hapa Tanzania tulianza mwaka 1967 wakati huo tulikuwa tunauza  vitabu ambavyo vimetengenezwa kutoka matawi mengine ya Oxford mfano vitabu kutoka  Kenya.

Swali: Kama kampuni, historia yenu ni ya muda mrefu, kwa sasa unaitazamaje sekta ya vitabu kwa jumla?

Jibu: Sekta ya vitabu miaka kama mitano iliyopita ilikuwa inafanya  vizuri lakini sasa hivi kidogo mambi siyo mazuri.

Hata hivyo, sisi kama Oxford hatuachi kutoa mchango wetu ambao tunaamini hata Serikali ikisema inaenda kwenye uchumi wa viwanda, sisi mchango wetu utakuwa ni  kuchapa vitabu bora, kwa sababu tunatengeneza rasilimali watu  ambao wataweza kuendesha hivyo viwanda.

Swali: Ipi nafasi ya vitabu katika maendeleo ya taaluma kwa wanafunzi?

Jibu:  karne na karne vitabu ndiyo njia pekee ya kuhamisha maarifa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.

Mwalimu anachomoa maarifa kutoka kwenye vitabu mbalimbali, mwanafunzi naye anapokea maarifa kutoka kwa mwalimu.

Swali: Mna mchango upi katika kuendeleza sekta ya elimu nchini?

Jibu: Sisi kama wachapishaji huwa tunatoa bidhaa ambazo zinasaidia katika utoaji wa elimu kwa sababu tunachapa vitabu vinavyoendana na utoaji wa elimu bora.

Tukisema elimu bora sio mwalimu pekee  bali hata vitabu bora,  mazingira mazuri  ya kufundishia na kujifunzia.

Kwa nafasi yetu tunatoa vitabu ambavyo vina ubora hata ukimuuliza mwalimu yeyote kuhusu Oxford atakuambia  ubora wa bidhaa zetu na tunaamini ubora huo unaendana na mitalaa.

Hatuchapishi vitabu kwa sababu tu tumeona kuna  soko; huwa tunakwenda katika shule mbalimbali kuzungumza na walimu wa somo husika.

Tunazungumza nao kujua vitu gani wanahitaji kuona. Pia tunawauliza  wanataka kuona nini kwenye vitabu, kisha tunaita jopo la wataalamu waliobobea  kwenye somo husika ili wavichambue kabla havijapitishwa.

Tunafanya haya yote ili kitabu kikifika shuleni,  kimsaidie mwalimu wakati wa kufundisha na mwanafunzi apate fursa nzuri ya kujifunza.

Kingine cha kipekee katika vitabu vyetu vya sekondari tunaelewa shida ya uhaba wa walimu hasa wa masomo ya sayansi , kwa hiyo tunajaribu kuweka katika mpangilio ambao hata mwanafunzi akiwa bila mwalimu anaweza kujifunza na kuelewa.

Hata hivyo, elimu bora ni pamoja na zana bora za kufundishia kwa hiyo kama Oxford mchango wetu ni kuchapisha vitabu bora, kwa sababu Serikali hata ikisema inajenga viwanda bado watahitajika vijana wasomi wa kuendeleza viwanda hivyo.

Swali: Mbali ya uchapishaji vitabu, mna mchango mwingine katika kukuza taaluma?

Jibu:Kingine huwa tunawapatia walimu mafunzo hasa katika lugha ya Kiingereza, mafunoz haya  mara nyingi tunafanyia ofisini kwetu. Tangu tuanze kufanya hayo tumewafikia walimu 100, na tunatarajia kuwafikia walimu zaidi ya 200 katika mikoa mbalimbali ikiwamo Arusha na Kilimanjaro

Pia tunaweka mambo ambayo yatawafanya wale wanaofundishwa kutoa mchango, badala ya kuwa wapokeaji tu.

Swali: Kuna suala la vitabu kuwa na makosa, Oxford  mnayaepuka vipi makosa hayo?

Jibu: Vitabu vyetu vinapitia mchakato mrefu ndiyo maana huwa hatutoi vitabu vingi kwa wakati mmoja.

Kitabu ili kiwe bora  kinatengenezwa kwa miezi tisa, kwa sababu kinapitia njia nyingi, kuanzia mwandishi, msanifu na mchapishaji.

Baada ya hapo kinajaribiwa katika shule mbalimbali kuona kama kinakidhi haja. Pia, pia kitachambuliwa na wataalamu wetu,  na kutoa maoni yao ambayo pia tunayazingatia.

Tunapotoa vitabu vinapitia mchakato ambao tunaamini vitakidhi haja ya wanafunzi kwa asilimia zaidi ya 95.

Hata hivyo,  kwa sababu hizi ni kazi zinafanywa na binadamu, siwezi kusema hakuna makosa kwa asilimia 100.

Pia, Tumekuwa tukijaribu kuepuka yale makosa ambayo yanaweza kuharibu maana husika ya neno.

Swali: Nini kinatofautisha Oxford na kampuni nyingine za uchapishaji?

Jibu: Kila kitabu kinajitofautisha na vingine kuanzia muonekano wa nje na kutokana na kubadilika kwa mtalaa. Sisi hatutoi vitabu vya masomo mengi.

Pia, tuna namna ya kipekee ya uwasilishaji wa maarifa yaliyomo kwenye vitabu vyetu ambayo ni tofauti na wengine. Kama ilivyo katika magazeti kila kampuni ina namna yake ya kipekee ya uwasilishaji taarifa inayojitofautisha na wengine.

Kwa mfano, katika vitabu vyetu hata michoro tunayotumia  kuanzia ukurasa wa mbele hadi kurasa za ndani ina hakimiliki.

Swali: Je Serikali inawaunga mkono kama wachapishaji?

Jibu: Siwezi kusema moja kwa moja kuwa haituungi mkono  kwasababu kazi ya Serikali yenyewe sio kumsaidia mtu mmoja mmoja.

Kwa kuwa imetujengea mazingira ya kufanya biashara na kuwekeza,  kwetu sisi  huku ni kutuunga mkono.

Swali: Nini mchango wenu katika kukuza lugha ya Kiswahili Tanzania?

Jibu: Katika kukuza Kiswahili tunashirikiana na Taasisi ya  Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Tataki)

Kuna kamusi ya Kiswahili sanifu wao Tataki wameitunga na sisi tumechapisha. Kamusi hiyo tumeiweka kwenye mtandao, inapatikana kupitia programu yetu ya Oxford inayoitwa (oxford global languages) na ilizinduliwa  rasmi mwaka jana.

Katika kamusi hiyo tunaweka lugha zote ambazo zinaongelewa na watu wengi lakini hazipewi kipaumbele.