Patoranking kumrudisha Q Chillah

Muktasari:

Akizungumza na Starehe, Q Chillah ambaye amepanga kuachia video ya wimbo wake uitwao ‘Sungura’ amesema matengenezo ya video hiyo ilikuwa sababu kwa yeye kukutana na mkali huyo wa muziki nchini humo.

Msanii mkongwe wa muziki wa kizazi kipya, Q Chillah keshokutwa anatarajia kutoa wimbo aliomshirikisha msanii wa Nigeria, Patoranking.

Akizungumza na Starehe, Q Chillah ambaye amepanga kuachia video ya wimbo wake uitwao ‘Sungura’ amesema matengenezo ya video hiyo ilikuwa sababu kwa yeye kukutana na mkali huyo wa muziki nchini humo.

Anasema alikuwa kimya kimuziki, kwani baada ya kutoa kazi yake ya mwisho alikuwa anasoma ramani ili kuangalia wapi alikosea ili aweze kusimamia tena.

“Nilipata nafasi ya kukutanishwa na mwanamuziki Patoranking na watu niliofahamiana nao nilipokuwa Afrika Kusini kikazi. Hivi sasa tunatarajia kukamilisha video ya wimbo huu mpya, ingekuwa tayari lakini alikuwa amebanwa na majukumu mengine,” anasema Q Chillah.

Anasema wimbo huo ni kati ya zile ambazo anaamini zitamsogeza kutoka hatua moja kwenda nyingine.

“Ni wimbo wangu wa kwanza kufanya na msanii kutoka Nigeria ambaye yupo katika hatua nzuri ya juu namshukuru QS Mhonda kwa kuwa ananisaidia kusimamia kazi zangu na tunaushirikiano mzuri sana kwa sasa,” anasema.

Hata hivyo, anasema amejitahidi kutoa kazi hiyo kimya kimya kama ilivyo kwa utamaduni wa wasanii wa zamani, kuliko ilivyo kwa wa sasa ambao wengi wao wanatumia skendo kutengeneza stori ili kazi zao zivume.

“Ninatoa wimbo lakini sitaki ‘kutengeneza kiki’ ili niweze kutoka kimuziki, siwezi kuingia katika skendo ili niweze kutoa kazi zangu, mimi nakuja kimya kimya naendeleza utamaduni wetu wa wasanii wa siku nyingi,” anasema Q Chillah.

Meneja wa msanii huyo, QS Mhonda anasema wimbo huo utatolewa sambamba na video ya wimbo wa ‘Sungura’ ambao ulishatoka hapo awali.

“Kila kitu kipo tayari na video ya wimbo huu mpya ipo katika hatua za mwisho kukamilisha, kwa sasa tutatoa kwanza audio ya wimbo huo Desemba 5 na baadaye tutaachia video yake,” anasema QS Mhonda.