MAONI YA MHARIRI: Polisi ifanyie kazi yanayosemwa kwa askari wake

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga

Muktasari:

Ajali ya kwanza iliyoripotiwa na gazeti hili toleo la jana, ilihusisha basi la kampuni ya New Force lililokuwa likisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Songea, mkoani Ruvuma.

Taifa limeendelea kuomboleza misiba inayotokana na mwendelezo wa ajali za barabarani ambazo ndani ya kipindi cha saa tisa, mabasi ya abiria yamesababisha vifo vya watu 25 na majeruhi kadhaa.

Ajali ya kwanza iliyoripotiwa na gazeti hili toleo la jana, ilihusisha basi la kampuni ya New Force lililokuwa likisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Songea, mkoani Ruvuma.

Ajali hiyo iligharimu maisha ya watu 12 na wengine 30 walijeruhiwa, chanzo chake kwa mujibu wa mashuhuda, ni mwendo wa kasi uliomfanya dereva ashindwe kudhibiti basi ipasavyo.

Pia, gazeti hili toleo la leo kuna habari nyingine ya ajali ya barabarani iliyohusisha basi la Super Shem na gari dogo la abiria aina ya Toyota - Hiace na kusababisha vifo vya watu 13 na majeruhi tisa. Ajali hiyo ilitokea saa 11 alfajiri wilayani Kwimba mkoani Mwanza na chanzo kwa mujibu wa mashuhuda ni mwendo wa kasi.

Ajali hizo mbili zimetokea siku chache baada ya Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga kutoa takwimu za ajali kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu, kwamba katika kipindi hicho, watu 1,580 walifariki dunia na wengine 4,659 walijeruhiwa.

Kuendelea kutokea ajali hizo zinazopoteza uhai wa Watanzania wengi na wengine kubaki walemavu, kunaibua maswali juu ya umakini wa madereva na askari wa usalama barabarani katika kudhibiti janga hilo.

Tumeshuhudia mbinu za aina mbalimbali zikitumiwa na kikosi hicho kudhibiti madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani, lakini pamoja na jitihada hizo, bado ajali zimeendelea kutokea. Moja ya mbinu ambazo zimekuwa zikitumiwa na kikosi hicho ni kutumia kifaa kinachoitwa ‘tochi’ kuwanasa madereva wanaoendesha kwa mwendo wa kasi na kuwatoza faini.

Hoja iliyopo ni kwamba kwa nini juhudi hizo hazionyeshi unafuu kwa Watanzania? Je, manung’uniko kwamba askari wa usalama barabarani wamejigeuza wakusanya ‘ushuru’ badala ya kusimamia usalama wa watumiaji wa vyombo vya moto ni ya kupuuza au kuna haja wahusika wakayafanyia kazi kuona kama yana mchango kwenye ajali hizo.

Wanaotoa manung’uniko hayo wanadai kwamba trafiki wanapokusanya faini kuna ‘kamisheni’ wanapewa kulingana na makusanyo na kwamba hiyo ndiyo sababu inayowafanya wakijikite zaidi katika kuadhibu badala ya kutoa elimu au onyo, pale panapostahili.

Pia kuna madai kwamba baadhi ya askari wamegeuza magari mabovu kuwa ‘mradi’ wa kujiongezea kipato kwa kuteua mtu wa kuwakusanyia fedha na kuwapelekea ili yapite bila kusimamishwa. Je, habari hizi nazo zina ukweli gani? Ni tetesi za kuzipuuza na hazifai kufanyiwa kazi na mamlaka husika?

Manung’uniko hayo yaliyoenea mitaani kuhusiana na utendaji wa askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani yanaibuka kila zinapotokea ajali kama hizi, na kwa kuwa zimekuwa zikijirudia mara kwa mara, tunadhani umefika wakati kwa Kamanda Mpinga kuyachunguza na mengine kuyatolea ufafanuzi.

Ongezeko hili la ajali linatugusa sote na linatuathiri wote mmojammoja, familia, jamii na taifa kwa ujumla.

Dhamana ya kusimamia usalama ni ya kila mmoja wetu, lakini zaidi umekasimiwa kwa Jeshi la Polisi, Kitengo cha Usalama Barabarani. Lifanye utafiti wa kina ili lije na majibu yatakayotoa suluhisho bora kukabili janga hili.