MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Profesa Mukandala ameonyesha mfano, aigwe

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala

Muktasari:

  • Miongoni mwa mambo ya dhahiri ni pamoja na kuifanya lugha hiyo kuwa rasmi ya mawasiliano chuoni kwa kuipa nafasi ya kutumika katika vikao mbalimbali vya utawala chuoni.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala, amekuwa akionesha uzalendo mkubwa katika kuienzi lugha ya Kiswahili. Daima amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha Kiswahili kinastawi.

Miongoni mwa mambo ya dhahiri ni pamoja na kuifanya lugha hiyo kuwa rasmi ya mawasiliano chuoni kwa kuipa nafasi ya kutumika katika vikao mbalimbali vya utawala chuoni.

Taasisi nyingi za kitaaluma zimekuwa zikibeza baadhi ya tamaduni za asili hususan Kiswahili, lugha ambayo baadhi ya wasomi huipiga vita na kuiona haina uwezo wa kutumika katika kubeba majukumu mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. Dhana hiyo hupingana na hali halisi ilivyo. Ndiyo maana Profesa Mukandala kwa kutambua nafasi na dhima ya Kiswahili kitaifa na kimataifa, amekuwa mstari wa mbele kuonesha kwamba Kiswahili kinaweza na hivyo kuruhusu kibebe majukumu mazito ambayo wasomi wengine katika baadhi ya taasisi hususan za elimu wamekuwa wakiona hakiwezi.

Fikra za baadhi ya wasomi zimeathiriwa na kasumba kwa kuona kuwa, kujua lugha za kigeni ndiyo usomi au uanataaluma. Suala hili hupingwa vikali na baadhi ya wasomi wanaotambua nafasi ya tamaduni zao. Profesa Ngugi wa Thiong’o kutoka nchini Kenya ni miongoni mwa wasomi hao. Kupitia baadhi ya kazi zake andishi, anabainisha kwamba hatuna budi kuvienzi vilivyo vyetu. Katika utangulizi wa kitabu chake cha “Shetani Msalabani” anasema: “…Mcheza kwao haachi hutuzwa. Tusipozisitawisha lugha hizi zetu sisi wenyewe, ni mgeni gani atakayejitokeza kuja kuzisitawisha?”

Swali hilo la Profesa Ngugi wa Thiong’o linatoa changamoto kubwa kwetu hususan kwa watumiaji wa Kiswahili. Profesa Mukandala kwa nafasi na uzalendo wake, anajiona anawiwa kukiendeleza Kiswahili hivyo kuchukua hatua hizo za kukistawisha Kiswahili.

Wakati akitunukiwa tuzo ya Kiswahili iliyokuwa imeandaliwa na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) chuoni hapo mwishoni mwa mwaka jana, na Balozi wa Heshima wa Kiswahili, Mama Salma Kikwete kama ishara ya kutambua mchango wake katika kukikuza na kukieneza Kiswahili; alionesha utayari wa kuridhia baadhi ya kozi zinazofundishwa kwa Kiingereza kufundishwa kwa Kiswahili chuoni hapo. Mintarafu uandishi wa vitabu vya kitaaluma, alieleza kuwa chuoni hapo wapo wahadhiri ambao wanaweza kuandika vitabu vya kitaaluma kwa Kiswahili, yeye akiwa mmoja miongoni mwao.

Ufundishaji kwa Kiswahili ni suala ambalo lipo katika mjadala siku nyingi na utoaji wake wa maamuzi umekuwa wa kusuasua. Profesa Mukandala kwa kuonesha mwelekeo huo, anatambua kwamba, hakuna uhusiano kati ya lugha ya kufundishia na elimu au maarifa. Maarifa huweza kutolewa kwa lugha yoyote ambayo anayefundishwa anaielewa vyema. Wataalamu wa masuala ya ya elimu wanasisitiza kuwa, lugha bora ya kutumika kutolea maarifa ni ile ambayo apewaye maarifa hayo anaifahamu barabara na aghalabu lugha hiyo huweza kuwa ya kwanza kwa mtumiaji wa lugha au lugha nyingine anayoifahamu vizuri zaidi.

Aidha, Profesa Mukandala alieleza kuwa miaka minne iliyopita alipofuatwa na mwanafunzi aliyekuwa akisoma shahada ya umahiri katika Kiswahili, ambaye alitakiwa kuwasilisha kwa Kiingereza, akiomba kuwasilisha kwa Kiswahili, alishangaa tasnifu hiyo kuwasilishwa kwa Kiingereza, hivyo kumruhusu kuwasilisha kwa Kiswahili.

Hayo ni matukio machache miongoni mwa mengi ambayo Profesa Mukandala ameonesha uzalendo katika Kiswahili. Wasomi na viongozi wengi katika nchi zao, hupigania lugha zao kuenziwa katika nyanja mbalimbali. Uzalendo na mchango wa Profesa Mukandala katika kukiendeleza Kiswahili hauna budi kuigwa na wasomi wengine kulingana na nafasi na nyadhifa zao. Shime, Profesa Mukandala.