BIASHARA LEO : Punguzo la riba BoT liimarishe biashara ndogo na za kati

Muktasari:

  • Mabadiliko hayo yalifanywa katika kipindi ambacho Watanzania wengi tunalalamika kupungua kwa mzunguko wa fedha hivyo nguvu ya watu kununua na kuuza. Athari zimeanza kuonekana baada ya kusinyaa kwa biashara na baadhi ya huduma za taasisi za fedha na uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Mwanzoni mwa Machi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilitangaza kupunguza riba ya mikopo inayotoa kwa benki za biashara nchini kutoka asilimia 16 mpaka asilimia 12.

Mabadiliko hayo yalifanywa katika kipindi ambacho Watanzania wengi tunalalamika kupungua kwa mzunguko wa fedha hivyo nguvu ya watu kununua na kuuza. Athari zimeanza kuonekana baada ya kusinyaa kwa biashara na baadhi ya huduma za taasisi za fedha na uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Punguzo la riba ya mikopo ya BoT linatoa nafasi kwa taasisi za fedha kukopa kwa gharama rafiki kwenye chanzo hicho na kurahisisha upatikanaji wa mitaji na fedha za kutekeleza miradi mbalimbali kwa wateja wake na kurudisha nguvu iliyokuwa imepotea kwa wengi mtaani baada ya muda fulani.

Taasisi za fedha hususan benki za biashara zipo kwenye nafasi nzuri ya kuitumia fursa hii kutunisha mitaji na kuongeza mzunguko wa bidhaa na huduma zao. Mikopo ya kibiashara kwa kampuni kubwa, kati na ndogo kwa wajasiriamali itakuwa katika nafasi za kufaidika na punguzo hili.

Kando ya kutoa mikopo, zipo huduma nyingine ambazo taasisi za fedha zinatoa kwa wateja wake na zitapata nafasi ya kuongezewa nguvu na mikopo hii kutoka BoT na kuhakikisha wanatimiza mipango na mikakati yao ili kutengeneza faida na kuendelea kusimama kwa nguvu kwenye soko la huduma za fedha.

Mikopo ya riba nafuu kutoka BoT ina maanisha benki za biashara zitakuwa kwenye nafasi ya kukopesha kwa bei nafuu zaidi ukilinganisha na ilivyokuwa siku za nyuma.

Mikopo hii kwa benki kubwa za biashara itanufaisha pia asasi ndogo za fedha ambazo kwa kiasi kikubwa, nyingi zinatumia mikopo kutoka kwenye benki za biashara kutimiza huduma kwa wateja na wanachama wake.

Kwenye hili vipo vyama vya ushirika vya kuweka na kukopa (Saccos) na vile vya kilimo na masoko (Amcos) vinavyotumia huduma na mikopo ya benki za biashara. Kwa mzunguko huu ipo faida kwa kuongeza nafasi na fursa ya watu wa kipato cha chini kupata huduma za fedha katika kiwango kinachotakiwa.

Mikopo hii kutoka BoT na kuingia kwenye mifuko ya benki za biashara na taasisi nyingine za fedha inatumiwa na wafanyabiashara au wajasiriamali wakubwa na wadogo, kundi hili huitumia mikopo hiyo kuongeza nguvu, mitaji na uzalishaji wa bidhaa na huduma bora kwa ujumla.

Fedha hizi zinapotumika kwa wajasiriamali na wafanyabiashara inakuwa rahisi kuonekana kwenye mzunguko wa uchumi kwa sababu shughuli zao zinatoa nafasi kwa idadi kubwa ya vijana kuajiriwa na kufanya kazi kwenye maeneo tofauti.

Kupitia mikopo hii ni rahisi kuona sekta za kilimo, viwanda vidogo, fedha, usafirishaji au madini zinaimarika. Fedha zinazopatikana na wafanyakazi kwenye maeneo haya ndizo zinatumika kuongeza kasi ya mzunguko wa fedha na kuchangamsha uchumi wa nchi.

Benki zinaweza kukopa kutoka kwenye vyanzo vingi vingine kulingana na mahitaji yake ila kwa punguzo la BoT ni moja ya utekelezaji wa upanuzi wa sera za fedha hivyo mategemeo yetu litazifanya benki za biashara kuongeza mikopo kwa wafanyabiashara wote hasa wadogo ambao kwa kiasi kikubwa ndio chachu ya usambazaji huduma mbalimbali kwa watu wengi.

Mzunguko huu utachangamsha uchumi kwa kiasi kikubwa na kurudisha nguvu ya ununuzi iliyopotea kwa muda. Wafanyabiashara wa chini na kati waendelee kujitokeza kuchukua mikopo kwenye taasisi za fedha na kutanua biashara zao ili kustawisha uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja.