Rais Magufuli, vyama vya upinzani ‘wanapigana vita’ wasivyoshinda

Muktasari:

  • Tafakuri yake ni kwamba mtoto anashangazwa na busara za watu kuingia vitani kupigana kwa maelezo kwamba ndiyo wanatatua matatizo. Tangu lini matatizo yakatatuliwa kwenye vurugu, damu inapomwagika au tatizo gani linatatuliwa kama siyo kulikuza.

Mwanzoni mwa miaka ya tisini, msanifu maarufu wa katuni ambaye ni raia wa Marekani, Bill Watterson alichora, katika mfululizo wa kazi zake za Calvin & Hobbes, mchoro wenye nukuu ya mtoto akimuuliza baba yake: “Baba kwa nini wanajeshi wanauana ili kumaliza matatizo ya dunia?”

Tafakuri yake ni kwamba mtoto anashangazwa na busara za watu kuingia vitani kupigana kwa maelezo kwamba ndiyo wanatatua matatizo. Tangu lini matatizo yakatatuliwa kwenye vurugu, damu inapomwagika au tatizo gani linatatuliwa kama siyo kulikuza.

Haihitaji jicho la kifalsafa kutambua kuwa nyakati za vurugu na machafuko huwa vigumu busara kutumika, bali hasira huamsha hasira, damu huchochea damu, kisasi huzaa kisasi, kifo husababisha vifo.

Askari anapokuwa vitani kisha kushuhudia mwenzake akiuawa, hupata athari kubwa ya kisaikolojia ambayo humfanya apate matokeo ya aina mbili; ama aogope kisha akimbie au aingiwe na roho ya kimapambano azidi kusonga mbele pasipo kuhofia.

Tafsiri ni kuwa anayeogopa na kukimbia husababisha vita ikome. Anayepandwa na hisia za mapambano kwa kumuona mwenzake ameuawa, huyo anakuwa na roho ya kisasi, vitendo vyake kama mnyama mwituni hahofii kitu. Mtu huyo anaweza kufanya chochote.

Yupo ambaye anaweza kuogopa baada ya kuona mapambano ni makali na wenzake wanauawa, lakini akashindwa kukimbia kwa sababu ya kuona hamna sehemu ya kukimbilia. Vilevile anahofia kujisalimisha kwa adui kwa sababu atateswa na hata kuuawa kinyama, anaona bora apambane; liwalo na liwe.

Tuseme ukweli. Ni kwamba mapigano, kutunishiana misuli na malumbano ya pande mbili ni matokeo ya kushindwa kutumia vizuri busara japo kidogo. Palipo na machafuko huibua tafsiri kuwa kuna uhaba mkubwa wa hekima.

Mwanafalsafa aliye pia mwanaharakati na raia wa India, Hayati Mahatma Gandhi aliwahi kusema: “Jicho kwa jicho huigeuza dunia yote kuwa kipofu.”

Ni hekima za Gandhi kwamba sera na misimamo ya jino kwa jino havisaidii, badala yake inatakiwa mmoja ajifanye kipofu ndipo itasaidia dunia nzima kuona. Ikiwa kila mtu anajiona ngangari na hataki kushuka chini, dunia itapofuka.

Unataka mapigano, je, unajua ushindi wake ni nini? Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kipo kwenye harakati za kile ambacho wanakiita Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta).

Rais John Magufuli ameshasema hana msalia mtume. Maneno yake ni kuwa Chadema waujenge huo Ukuta wao waone, akasema yeye ni wa tofauti na hajaribiwi.

Chadema waliahirisha kile ambacho kiliaminika kuwa ni maandamano ya nchi nzima kuanzia Septemba Mosi. Kalenda yao mpya ni Oktoba mosi. Sababu ya kuahirisha ni kutoa nafasi kwa viongozi wa dini kuzungumza na Rais Magufuli kutafuta mwafaka. Jambo zuri.

Sakata la Ukuta

Kuelekea Septemba mosi, askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wa Jeshi la Polisi walishuhudiwa wakifanya mazoezi mitaani, wakiwa na silaha. Tafsiri ikawa vitisho kwa Ukuta.

Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), nalo likatangaza Septemba mosi kuwa maadhimisho yake ya kutimiza umri wa miaka 52. Tafsiri ya upande wa pili ikawa ni hila dhidi ya Ukuta, kwamba Rais Magufuli anatumia vyombo vyake kuwanyong’onyesha wapinzani.

Sasa, kuelekea Oktoba mosi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametangaza tarehe hiyo kuwa siku ya kupanda miti kwenye mkoa wake. Hivyo, ndiyo kusema sinema inaendelea.

Tusimame kwenye kitovu kisha tuulizane maswali; Je, Chadema wanalenga kushinda nini kupitia Ukuta? Ushindi wao ni nini? Je, wanaamini wanaweza kushinda? Ushindi wao una gharama gani?

Je, Rais Magufuli shabaha yake nini anapodhamiria kuvunja Ukuta mara tu Chadema watakapoujenga? Lengo lake hasa ni kushinda nini? Ni mkuu wa nchi na anamiliki dola, sina shaka anaweza kushinda lakini je, ushindi wake ni nini? Gharama ya ushindi wake itakuwa nini?

Chadema wanakusudia kumlazimisha Dk Magufuli kusalimu amri na awaruhusu kufanya shughuli za kisiasa pamoja na mambo mengine wanayoyalalamikia. Je, ikitokea mpaka mwisho akiendelea kukataa na kutumia nguvu kuwadhibiti, gharama ya mapambano hayo ni nini? Rais Magufuli anataka wapinzani wanyooke na watii amri kama ambavyo mamlaka zake zimekuwa zikielekeza. Ikiwa wapinzani hawatatii na kuendelea kumpinga, kisha Oktoba mosi wakamwagika barabarani, naye akaamrisha dola kutumia nguvu kudhibiti, gharama ya udhibiti huo ni nini?

Mazungumzo yanahitajika

Ulimwengu wa leo unataka ustaarabu na mazungumzo kuliko kitu chochote. Tupo kwenye wakati ambao tayari visa vingi vya kisiasa vilishashuhudiwa, sasa haitakiwi tena shuhuda wa machafuko ya kisiasa awe mwanzisha machafuko.

Mapambano kati ya polisi na wafuasi wa Chadema, baada ya Uchaguzi Mkuu 2010, nani aliyeathirika? Ni nguvu kazi ya nchi kupotea kwa vijana wawili wa Kitanzania waliouawa. Vilevile, matumizi mabaya ya rasilimali za nchi. Risasi badala ya kutumika kudhibiti ujambazi na uhalifu mwingine, zikaua wakereketwa wa kisiasa.

Hata baada ya Tanzania kushuhudia machafuko na kupokea wakimbizi kutoka Burundi, Rwanda, DRC, Kenya, Msumbiji na kwingineko, bado wapo wenye kuamini katika jino kwa jino?

Muhimu zaidi ambacho kila upande unatakiwa utambue ni kwamba jeuri na kutunishiana misuli kati ya wapinzani na Rais Magufuli, haina mshindi kati yao. Matokeo yoyote yale ni kushindwa kwao kuruhusu busara ichukue nafasi, hivyo kuichafua nchi.

Januari 26 na 27, 2001 katika kutunishiana ubavu kati ya Chama cha Wananchi (CUF) na polisi, hakuna aliyeshinda. Wote waliingia kwenye kashfa ya kuharibu nchi, kisha raia wasio na hatia walipoteza maisha na wengine kugeuka wakimbizi.

Mhubiri wa amani, Mmarekani Gales Fraser amekuwa akiishutumu nchi yake kusababisha machafuko ya kidunia kuliko kujenga amani kwa sababu hukimbilia kutumia nguvu badala ya mazungumzo.

Kwa miaka 15 sasa, tangu Marekani ilipotangaza kuweka mguu na kusambaratisha popote pale ambapo magaidi wapo, baada ya kushambuliwa kwenye majengo yao ya World Trade Center (WTC) na Pentagon Septemba 11, 2001, taifa hilo linatumia gharama kubwa na halishindi.

Ndani ya hiyo miaka 15, Marekani imejikuta ikitengeneza magaidi wengi duniani, hususan Mashariki ya Kati kwa sababu anayeshuhudia mwenzake akiuawa, naye anapandwa wazimu wa kupambana zaidi, matokeo yake badala ya kuwamaliza, imesababisha waongezeke.

Kinachosababisha Marekani ishindwe si kingine. Ni kwamba inaona kufanya maridhiano ni jambo la aibu kwa taifa kubwa kama hilo. Magaidi nao wanaona bora tu wapigane; liwalo na liwe. Matokeo yake dunia inaumia, watu wasio na hatia wanauwa na wengine kuwa walemavu.

Inawezekana hata Rais Magufuli anaona ndiye Amiri Jeshi Mkuu, sasa kukaa na kubembelezana na wapinzani ni kutotumia vizuri mamlaka yake. Hata hivyo, namshauri kuzingatia kuwa matumizi bora ya nguvu ni kujizuia kuzitumia na kuruhusu mazungumzo yenye kutengeneza mwafaka bila kupigana.

Rais Magufuli na wapinzani, wasiishie kwenye kuwaza Ukuta na vunja Ukuta, athari zozote zitaumiza wasiohusika. Tanzania ya wastaarabu hii, haitakiwi kutumia watu wasio na hatia kwa mtaji wa kisiasa. Ni heshima kubwa kuchukua nchi, kuongoza kisha kuikabidhi kwa anayefuata bila kuiingiza kwenye machafuko.

Mwandishi wa makala haya ni mwandishi wa habari, mchambuzi wa siasa, jamii na sanaa. Ni mmiliki wa tovuti ya Maandishi Genius inayopatikana kwa anuani ya www.luqmanmaloto.com