Rais Magufuli apongezwe kwa ndege alizonunua, kazi iendelee

Nilikuwa natembea barabarani bila mikogo, matembezi ya jioni. Ni siku ambayo ndege moja mpya kati ya mbili za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), aina ya Bombardier Q400, iliwasili mchana, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Mlevi mmoja akawa anapita anapayuka “ooh, ndege mbaya baba yako anayo?” Akawa anarudia “mnasema ndege hazikimbii, baba yako anayo?” Kikapita kimya kidogo kisha akapaza sauti kwa mara nyingine “eti ndege za mapanga boy, baba yako anayo?”

Niligeuka kufuatilia yule mlevi anamsema nani, nikagundua alikuwa anamshambulia mlevi mwenzake ambaye walibishana, mwisho wakataka kupigana. Sasa kwa vile yeye ni mwoga ndiyo akakimbia na kuanza kurusha mashambulizi akiwa mbali “baba yako anayo?”

Maneno yale ya mlevi yalinikumbusha zamani wakati huo kuwa na gari ni utajiri mkubwa, ukiwa nalo ni utukufu kwenye jamii. Mtu mmoja alimiliki gari lake kuukuu, limeungwaungwa, bodi la mbao. Akajua tu watu watasema ni baya, kukomesha wasemaji, akaandika kwa nyuma “baba yako analo?”

Ukiachana na hoja za ubishi wa walevi hao, hivi sasa nchi ipo kwenye mabishano makali kuhusu ununuzi wa ndege mbili mpya aina ya Bombardier Q400. Wapinzani wanazikosoa kuwa Serikali ya Tanzania, chini ya Dk John Magufuli imechemsha.

Vilevile, wapo watetezi wengi tu kuwa bora ndege zimekuja. Hawakosekani wenye kuvuka mpaka na kuhoji, “ninyi mnaoponda Bombardier Q400, za kwenu kubwa na zinazokimbia zipo wapi?” Swali hilo halina tofauti na lile la yule mlevi aliyemuuliza mwenzake “baba yako anayo?”

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini kupitia chama hicho, ndiye mpinzani aliyejitokeza na kumpongeza waziwazi Dk Magufuli kuhusu ununuzi wa ndege hizo, ingawa pia ametilia shaka bei iliyotumika kununua. 

Hongera Rais Magufuli

Rais Magufuli anastahili kupongezwa kwa uthubutu wake. Wakati mwingine kukosolewa ni ishara ya mafanikio, kwamba lipo ambalo limetendeka. Lisingekuwapo wakosoaji wangekosoa nini?

Pamoja na kila sababu ya kiutetezi ambayo imeshatolewa, muhimu kwa sasa ni kwamba ndege zimenunuliwa. Dharau kwa usichokuwanacho ilimponza mzee mtaka makuu.

Enzi za ujana wake mzee Mtaka Makuu alipokuwa anapata fedha alikataa kujenga nyumba, akidai malengo yake ni kuwa na ghorofa, kwa hiyo maisha yake yote yakawa “nitajenga tu, nitajenga tu” mpaka amezeeka bila kumiliki japo kibanda.

Haina ubaya kuanza na kidogo wakati ukihangaikia kutafuta kikubwa. Dhihaka hizi kwa ndege mpya zilizonunuliwa ni sawa na mtoto anayewagomea wazazi wake kuwa bila keki hanywi chai, wakati nyumbani kwao kuna njaa, mkate haupatikani.

Kupongeza ni uungwana na kukubali kilichotendeka. Kupongeza pia ni kumtia moyo aliyetenda ili apate moto wa kufanya zaidi. Upo msemo uliosambazwa na jarida maarufu duniani la Forbes, uliotoka kwa mwanamke mjasiriamali wa Marekani, Amy Rees Anderson, unaosema: “Mtu anayejisikia kuthaminiwa kwa anachofanya hufanya zaidi ya matarajio.”

Ununuzi wa Bombardier siyo kituko

Isije kuonekana kuwa kununua Bombardier Q400 ni kituko. Mashirika makubwa ya safari za anga ulimwenguni ni wateja wa kampuni ya Bombardier Aerospace ya Canada, inayotengeneza ndege za Bombardier. Iweje Tanzania ndiyo ionekane kituko?

Shirika la Ndege la Ethiopia (Ethiopian Airlines), Desemba mwaka jana, ilinunua ndege mbili kutoka Bombardier Aerospace aina ya Bombardier Q400, hivyo kufikisha jumla ya Bombardier Q400 19.

Ethiopian Airlines ina ndege 78, ina safari 101 duniani kote za abiria na 23 za mizigo. Inamiliki ndege 59 kubwa za Boeing na Airbus.  Shirika hilo la ndege linatarajiwa kufikisha ndege zaidi ya 120 mwaka huu. Tanzania na ATC yao wana nini mpaka kuzicheka Bombardier?

Shirika la Ndege la Jazz, Canada linamiliki ndege 115 na hufanya safari zake kwenye vituo 79 kati ya Canada na Marekani. Ndege zote za Jazz zinatokea Bombardier Aerospace. Wanazo pia Bombadier Q400 39, na mwaka jana waliongeza nyingine 13. Wanaratajia kupokea ndege nyingine 10 za Bombardier Q400.

Jazz ni shirika kubwa la ndege, likishika nafasi ya tatu Canada kwa wingi wa ndege. Wanafanya biashara yao kwa mafanikio ndiyo maana wamekuwa wateja waaminifu wa Bombardier Aerospace. Tanzania yenyewe ina nini mpaka kuziona Bombardier Q400 si mali kitu?

Shirika la Ndege la Horizon (Horizon Air) lenye maskani yake SeaTac, Washington DC, Marekani, ndilo linaloshika nafasi ya nane kwa ukubwa miongoni mwa mashirika ya ndege nchini humo. Ndege zake hufanya safari zake kwenye vituo 45, huzunguka majimbo 42 ya Marekani na hufika mpaka Canada.

Horizon Air jeuri yote ya safari zake na ushindani wa kibiashara inaofanya Marekani, ndege zake zote ni Bombardier Q400. Hakuna kituko ambacho Tanzania imefanya kununua Bombardier Q400.

Luxembourg pamoja ustawi wake mzuri wa kiuchumi, shirika lake la ndege la Luxair linamiliki ndege 17, tisa zikiwa Bombardier Q400, halafu Boeing 737-700 mbili, Boeing 737-800 nne na Embraer ERJ 145 mbili.

Unadharau vipi Bombardier wakati wastani wa pato la mwananchi wa Luxembourg (per capita) kwa mwaka ni dola 104,359 (Sh.223 milioni) wakati Mtanzania wastani wa pato lake ni dola 963 (Sh2.1 milioni). Wenye uchumi wao wanatumia Bombardier Q400. 

Jumla ya ndege ambazo zinamilikiwa na ATCL ni tatu, ukijumlisha na iliyokuwepo japo safari zake ni za kusuasua kutokana na ubovu. Shirika hilo la ndege lilianzishwa mwaka 1977 baada ya kuvunjika kwa lililokuwa Shirika la Ndege la Afrika Mashariki, kufuatia pia kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati huo.

Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi wakati ATCL (Air Tanzania Corporation) inaanzishwa, alipata kunisimulia kuwa mapendekezo ya jina hilo yalitoka kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ili ikitamkwa Air Tanzania, lile Tanzania liwe linasikika vizuri kwa sababu linatajwa mwisho.

Hii ndiyo sababu katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati huo, Kenya na Uganda, Tanzania peke yake ndiyo shirika lake la ndege lina jina tofauti. Kenya wana Kenya Airways, Uganda ni Uganda Airlines, lakini kwa utofauti huohuo, Air Tanzania ndiyo shirika ambalo limedoda kuliko yote hayo.

Mwaka 1977, ATCL ilikuwa na ndege tisa, lakini usimamizi wake mbovu ndiyo sababu ya shirika hilo kudumaa. Mwaka 1994, ATCL iliunganisha nguvu na Uganda Airline na lile la Afrika Kusini (South African Airways) na kuunda Shirika la Ndege la Umoja (Alliance Air) ambalo baada ya kufanya kazi miaka sita, mwaka 2000, lilivunjika kwa maelezo kuwa lilipata hasara ya Sh50 bilioni.

Mwaka 2002, Air Tanzania ikachukuliwa na South African Airways (SAA), mwaka 2006, Serikali ya Tanzania ikashtuka kuwa shirika hilo liliendeshwa na SAA kwa hasara katika kipindi miaka minne.

Mwaka 2007, Air Tanzania baada kurudi kwenye mamlaka ya Serikali ya Tanzania, ilianza na ndege mbili kubwa mpya aina ya Boeing 737-200s na Februari 2008 ilinunua ndege mbili aina ya Bombardier Q300. Baada ya hapo yalipita matukio mengi, lakini kufikia mwaka 2011, Air Tanzania ilikuwa na ndege moja aina ya Bombardier Q300 mbovu.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Otouh, mwaka 2012, ilipendekeza mameneja watatu wa Air Tanzania kuchukuliwa hatua za kisheria baada ya kuingia mkataba na kampuni ya Wallis Trading, kwa ajili ya kukodi ndege ya Airbus A320 kwa miaka minne, matokeo yake ilifanya kazi miezi saba tu, huku ikielezwa miezi mingine 41 ilikuwa kwenye matengenezo.

Mambo ambayo yameifanya Air Tanzania ifike ilipo ni mengi lakini kubwa ni watendaji wake. Mfano, mkataba huo kati ya ATCL na Wallis Tranding kwa ajili ya ndege hiyo Airbus A320, iliisababishia Serikali hasara ya karibu Sh100 bilioni.

Kazi iendelee

Kwa kutazama yaliyopita ni kwamba juhudi zilifanywa na usaliti pia ulikuwa mkubwa ndiyo maana ATCL ipo ilipofikia. Hayo mambo yampe moto Rais Magufuli kisha kazi iendelee.

Uzalendo ungekuwapo ATCL ingekuwa imara kama Kenya Airways. Mwaka 2002, Tanzania ilikuwa iingie kwenye aibu ya karne pale Kenya Airways ilipotaka kuinunua Air Tanzania wakati yote yalianzishwa mwaka mmoja. Ni bahati nzuri SAA walishinda zabuni.  Rais Magufuli afanye kazi ya kuiondoa nchi kwenye aibu, maana RwandAir ya mwaka 2002 leo ni shirika kubwa, Somalia yenye vita, Somali Air ina ndege kubwa, Ivory Coast na shirika la Air Cote d’Ivoire lililoanza miaka minne iiyopita, leo lipo mbali. Tanzania je?

Mwandishi wa makala haya ni mwandishi wa habari, mchambuzi wa siasa, jamii na sanaa. Ni mmiliki wa tovuti ya Maandishi Genius inayopatikana kwa anuani ya mtandao www.luqmanmaloto.com