Rais ni mlezi wa Katiba na sheria, anapovikiuka ni tatizo

Muktasari:

  • Kama sehemu ya kumuenzi Mwalimu Nyerere, nimeonelea nitafakari machache yatokanayo na uongozi wake ambayo ni funzo kwetu viongozi wa sasa, hasa katika nyakati hizi tunazopita. Tafakuri hii itahusu uamuzi wa Mwalimu Nyerere kumteua mzee Chediel Mgonja, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kinyume na Katiba na sheria za nchi, na pia nafasi ya viongozi wenzake katika kuhakikisha Katiba na sheria za nchi havivunjwi, hasa na Rais wa nchi.

Jana ilikuwa ni Siku ya Kumbukumbu ya miaka 18 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, Baba wa Taifa na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwangu Nyerere ni Kiongozi wa mfano, najifunza kwa mazuri na mapungufu yake katika uongozi, na huyatumia mafunzo husika kunisaidia kuwaongoza vizuri wananchi wenzangu walionipa dhamana ya uongozi.

Kama sehemu ya kumuenzi Mwalimu Nyerere, nimeonelea nitafakari machache yatokanayo na uongozi wake ambayo ni funzo kwetu viongozi wa sasa, hasa katika nyakati hizi tunazopita. Tafakuri hii itahusu uamuzi wa Mwalimu Nyerere kumteua mzee Chediel Mgonja, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kinyume na Katiba na sheria za nchi, na pia nafasi ya viongozi wenzake katika kuhakikisha Katiba na sheria za nchi havivunjwi, hasa na Rais wa nchi.

Chediel Yohane Mgonja ni jina ambalo huwezi kuliepuka kwenye kuijadili historia ya Taifa letu, hasa awamu ya kwanza. Mgonja ana historia ndefu, tangu Chuoni Makerere miaka ya mwishoni mwa 1950 mpaka kuwa mbunge na waziri mwenye umri mdogo zaidi mwaka 1965 kwa kumshinda kwenye nafasi ya ubunge “kingunge” Elias Kisenge, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Tanu katika uchaguzi wa Jimbo la Same katika Mkoa wa Tanga (Katika wakati husika Same ilikuwa ni sehemu ya Mkoa wa Tanga).

Mgonja alikuwa pia rafiki wa karibu wa Mwalimu Nyerere, pamoja na kuwa kiongozi mtiifu kwake. Itakumbukwa ni Mgonja aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wakati tukitoa msimamo wetu tata wa “Kuitambua Biafra” mwaka 1968. Na pia ni Mgonja aliyesimamia mapinduzi makubwa ya “Kisomo cha Watu Wazima” wakati akiwa Waziri wa Elimu miaka ya mwanzoni mwa 1970.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1980 kulikuwa na ushindani mkubwa katika nafasi ya ubunge kuliwakilisha Jimbo la Same, pamoja na ushindani huo Chediel Mgonja alishinda uchaguzi ule. Ushindi ule haukuwaridhisha washindani wake, hivyo Mgonja alishitakiwa kwenye kesi ya uchaguzi kuwa aliiba kura za uchaguzi (election irregularities) na kwa hiyo ushindi wake wa ubunge haukuwa halali.

Kesi husika iliunguruma kwa muda wa miaka miwili, kati ya 1980 Mpaka 1982, hatimaye Mgonja alishinda kesi dhidi yake katika Mahakama Kuu Arusha, kwa hoja kuwa wapigakura hawana haki ya kupinga ushindi wa mgombea. Ushindi huo wa kesi dhidi ya Mgonja ukakatiwa Rufani katika Mahakama ya Rufaa nchini.

Katika shauri hilo namba 84 la mwaka 1980 lililofunguliwa na William Bakari na mwenzake dhidi ya Mgonja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mahakama ya Rufaa Tanzania iliamua kuwa, mpiga kura ana haki kufungua kesi mahakamani kupinga matokeo, tofauti na maamuzi ya mahakama ya Arusha iliyosema wapigakura hawana haki hiyo. Na hivyo walalamikaji walishinda kesi husika. Mahakama pia ilimhukumu Mgonja kutokujihusisha na siasa kwa muda wa miaka 10.

Licha ya hukumu hii, mwaka 1983 Mwalimu Nyerere alimteua Mgonja kuwa mkuu wa Mkoa wa Shinyanga hali ya kuwa adhabu yake ya kutojihusisha na nafasi za kisiasa kwa muda wa miaka 10 haijatumikiwa hata kwa mwaka mmoja.

Jaji Warioba amueleza Mwalimu

Mwanasheria Mkuu wa wakati ule, Jaji Joseph Warioba anazikumbuka zaidi nyakati husika, amewahi kuelezea yafuatayo juu ya kadhia hii;

“Na kinyume na wale wanaosema (Nyerere) alikuwa haambiliki, si kweli. Alikuwa anakasirika kama mtu mwingine yeyote yule na aliweza kukufokea. Na wakati fulani alikuwa amemteua mtu (Mgonja) katika nafasi fulani (kuwa Mkuu wa Mkoa). Mimi kama Mwanasheria Mkuu wake nikaenda kumwambia: Mwalimu hapa sheria inakataa, huwezi kumteua huyu.

Nikamwambia kuna kikwazo cha kisheria hapa, kwa kuwa alikuwa yule mtu (aliyepaswa kuteuliwa) alikuwa ameonewa (ameonekana ana) mambo fulani. Mwalimu akakasirika, akaniambia wewe ndiye kikwazo. Wewe umezoea kila ukija hapa ni kuniambia usifanye hivi kwa sababu sheria inakataa, hapana hili sikubali.

Nikamwambia Mwalimu, hili ni suala la Katiba, ukifanya hivi kutakuwa na crisis (mgogoro) kwenye Bunge. Akasema si ndiyo demokrasi? Ngoja iende huko. Nikamwambia kwamba ni suala la Katiba, na yeye ndiye guardian (mlezi) wa Katiba.

Nikaendelea kumwambia Mwalimu kwamba ikitokea crisis na yeye ndiye guardian; yaani imesababishwa na guardian, ni kitu serious (kikubwa). Akasema ndiyo demokrasi, haya mambo ya kufichaficha siyo mazuri; ngoja iende huko.

Jaji Warioba anaendelea kulikumbuka tukio hilo na kusema: Nikatoka pale, nikaenda kwa Waziri Mkuu, Sokoine (Edward) nikamwambia; PM sasa kutakuwa na matatizo kwenye Bunge, boss hataki kubadili msimamo, akasema aah hebu twende bwana tumshauri angalau asimwapishe huyu mpaka tuwe tumetoka bungeni.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, walipokwenda kumwona Mwalimu asubuhi nyumbani kwake, Msasani Dar es Salaam, mambo yakawa tofauti. Alipotuona tu akaanza kucheka, akasema; Edward (Sokoine), nilimfukuza huyu jana; lakini aliniambia kitu kimenisumbua sana usiku. Sasa sijui kimekuleta nini hapa? Waziri Mkuu akaelewa na akauliza, sasa nini kimekusumbua?

Mwalimu akasema nimefuata ushauri wake (nimetengua uteuzi wa Mgonja kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga), Akasema: Joseph, wewe ni stubborn (msumbufu) eeh?”

Masimulizi ya Jaji Joseph Warioba, aliyekuwa mwanasheria mkuu wa Serikali mwaka 1983 wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Nyerere alipomteua Chediel Yohane Mgonja kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kinyume na utaratibu.

Funzo kubwa hapa ni juu ya wajibu wa viongozi kuhakikisha wanalinda Katiba na sheria za nchi, na kuhakikishwa havivunjwi, hasa na Rais wa nchi, kwa kuwa huzusha mgogoro zaidi wa kikatiba. Pia, utayari na busara za Rais kuona makosa yake na kujirekebisha.

Nyerere wangu mie alikuwa Rais mwenye nguvu kubwa. Alikuwa Rais nyakati ambazo Rais ni Rais haswa. Hata hivyo Nyerere wangu mie hakutumia urais huo wenye nguvu kubwa kudharau Katiba. Aliiheshimu. Alipata kutuonya kuwa kwa Katiba yetu akitaka kuwa dikteta angeweza. Lakini, aliamua kutokuwa mtawala bali kiongozi.

Mwalimu Nyerere aling’atuka madarakani 1985. Lakini, kabla ya kung’atuka alimpunguzia (kwa mamlaka aliyonayo kikatiba) mzee Mgonja adhabu yake ya kutojishughulisha na siasa kwa muda wa miaka 10. Mzee Mgonja aligombea ubunge wa Same katika uchaguzi wa mwaka 1985, wananchi wa Same walimpa ushindi, na pia wakamchagua tena kuwa mbunge wao katika uchaguzi wa 1990, kabla ya kustaafu siasa za kibunge mwaka 1995.

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto

Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo Kigoma Ujiji