Rangi ni muhimu kuitambulisha bidhaa, huduma yako

Muktasari:

  • Wengi hawafahamu uwapo wa haiba ya rangi na namna inavyoweza kukujenga au kukubomoa kwenye uchumi binafsi.
  • Namna mtu anavyoonekana kutokana na mavazi, mtindo wa nywele, mapambo au vitu vingine alivyonavyo hutoa ujumbe usio wa maneno. Kwa hakika muonekano huo huweza kuwa na mawasiliano yenye nguvu.

Mwanasaikolojia wa Uingereza, Dk Edward de Bono alipata kusema: “Rangi ina mawasiliano ya haraka zaidi kwa ufahamu wa binadamu kuliko maumbile, sauti au ishara ya mwili. Rangi inazungumza bila maneno.”

Wengi hawafahamu uwapo wa haiba ya rangi na namna inavyoweza kukujenga au kukubomoa kwenye uchumi binafsi.

Namna mtu anavyoonekana kutokana na mavazi, mtindo wa nywele, mapambo au vitu vingine alivyonavyo hutoa ujumbe usio wa maneno. Kwa hakika muonekano huo huweza kuwa na mawasiliano yenye nguvu.

Ingawa wanaona na kuzitambua baadhi ya kampuni kubwa ndani na nje ya nchi kwa rangi, hawafahamu siri iliyo nyuma ya pazia. Wengi wanafahamau rangi ya bluu inatumiwa na baadhi ya kampuni za simu nchini wakati zingine zikitumia nyekundu.

Mashabiki wa klabu za Simba na Yanga hutofautiana kwa rangi zao. Simba ni nyekundu ilhali Yanga ni njano. Pia, vyama vya siasa viko hivyo. Hata bendera za mataifa mbalimbali zina rangi zenye maana.

Kwenye utamaduni; vikundi vya ngoma na kwaya au bendi za muziki huwa na rangi zinazoipendelea zaidi. Kwenye shughuli kama vile maombolezo, rangi nyeusi na nyeupe hutawala.

Kuna utafiti uliodhihirisha kuwa umaridadi huweza kuhusishwa na uaminifu, uungwana au utu. Watu wengi wamewahi kudanganyika wakathamini watu wasio na mbele wala nyuma kutokana na namna walivyovaa kama mamilionea.

Hebu jiulize; huwa unavaa nguo kutokana na hisia zako asubuhi unapotoka nyumbani au unavaa tu bila kufikiria jambo lolote?

Je, unafikiria watu wanaokuona huwa wanapata ujumbe gani kutokana na namna unavyovaa na unavyoonekana? Je, katika jamii wewe unaonekana kama wanavyoonekana marafiki zako au unaofuatana nao?

Kuna usemi maarufu; ‘mavazi humfanya mtu kuwa mtu.’ Licha ya umaridadi kumfanya mtu apate hadhi, lakini nywele huweza kufanya mtu akawekwa katika kundi fulani. Wapo watu ambao humkumu mtu kutokana na muonekano wa nywele zake.

Kuna siri ya mafanikio kwenye rangi. Wachambuzi wa saikolojia wanatambua kuwa rangi hutoa aina fulani ya ishara, hilo limethibitishwa na wataalamu mbalimbali akiwamo mwandishi wa makala haya kwenye kitabu chake cha ‘Jitambue’ alimoandika nguvu za rangi katika ujasiriamali.

Kutokana na hilo na utafiti mbalimbali uliowahi kufanywa, tutazungumzia baadhi ya rangi na siri zake katika matumizi mbalimbali ili kujenga mtazamo na mvuto wa muonekano katika shughuli za kila siku.

Bluu

Ipo siri iliyojificha ndani ya rangi ya bluu ambayo mara nyingi inaelezwa kuwa na maana nyingi, ikiwamo uaminifu, uadilifu na uongozi. Rangi hii inapendwa na wengi, hasa wanaume.

Katika dhifa mbalimbali utakuta wanaume wamevaa suti hasa za bluu iliyokoza. Lakini suti ya rangi hii imekuwa ikipendwa zaidi na baadhi ya viongozi, kampuni za teknolojia ya mawasiliano, vifaatiba au taasisi za fedha.

Mara nyingi, rangi hiyo huelezwa kuwa ina nguvu kimataifa kwani hutumika katika matukio yoyote. Licha ya kuwakilisha anga na bahari, inaelezwa kuwa rangi ya uhakika na salama zaidi.

Mwanasaikolojia wa Marekani, Kendra Cherry anasema rangi hii inakumbusha hisia za utulivu, amani, salama na utaratibu. Rangi ya bluu pia inasaidia kushusha joto la mwili hasa linaposababishwa na hofu.

Ni muhimu kujua wapi na kwa nini rangi ya bluu hutumika zaidi jambo litakalokujengea kujiamini katika shughuli zako za uchumi. Ukitafakari kwa nini watu au taasisi wanapenda rangi ya bluu unaweza ukaelewa umuhimu wa rangi hii.

Nyekundu

Kuna kitu fulani ndani ya rangi nyekundu ambacho huwa kinajitokeza kumuimarisha mtu, taasisi au bidhaa na kuipa mvuto wa kipekee. Rangi nyekundu ni njia bora ya kuonyesha mamlaka, uwezo na hamasa.

Rangi nyekundu huamsha shauku au msisimko na mara nyingi hutumika zaidi kwenye malipo ya bidhaa, vitani na sehemu za hatari kwa ishara ya kuchukua tahadhari.

Pia, hutumika kwa mapenzi ya wapendanao wakati kwa mahitaji ya kinywaji na chakula huwa ni ishara ya muunganiko na mahitaji au hisia zako.

Nyekundu huongeza hamasa ya kufanya jambo vilevile huvutia macho ya watu wengi. Hutumika katika migahawa, maduka, maeneo ya mauzo sehemu za vinywaji. Tafakari, ni watu au taasisi za aina gani zinapendelea au zinatumia zaidi rangi ya nyekundu.

Nyeusi

Rangi hii ni miongoni mwa zinazoonyesha utanashati, ubora, mamlaka, umakini na umahiri wa jambo. Ingawa kuna baadhi wanaziweka katika kundi la ujeuri au kutokuwa na utani na jambo fulani, hususan inapovaliwa na watendaji.

Wanasheria, walinzi na watu wa masoko hupendelea kuvaa suti au mavazi ya rangi hii kwa lengo la kuongeza mvuto na mwonekano wao.

Bidhaa zilizowekwa kwenye boksi au kasha lenye rangi nyeusi, maana yake ni kitu ghali, kwa mfano komputa nyeusi, simu nyeusi au magari mweusi ni ghali kuliko ya rangi nyingine. Watu na taasisi wanapenda rangi ya nyeusi kutokana sababu hizi.