Thursday, September 14, 2017

Rasilimali za misitu zinavyosukiwa mkakati wa kubeba uchumi wa taifa

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Kwa miaka kadhaa sasa rasilimali za misitu zimekuwa katika hatari ya kuangamia, lakini Serikali imesimama kuhakikisha uendelevu wake unalindwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha maeneo ya kiutendaji na udhibiti dhidi ya waharibifu.

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ni miongoni mwa mikakati ya kuhakikisha rasilimali hizi zinatunzwa kisheria na kukabiliana na uharibifu.

Kuanzishwa kwa TFS kwenye kanda saba za kati yenye mikoa ya Dodoma, Singida na Manyara; Kaskazini inayojumuisha Arusha, Kilimanjaro na Tanga; Kusini ilipo mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma na Mashariki yenye Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.

Nyingine ni Nyanda za Juu Kusini yenye mikoa ya Songwe, Mbeya, Rukwa na Njombe; Magharibi ikiwa na Tabora, Katavi, Kigoma na Shinyanga huku Kanda ya Ziwa ikiwa na Mwanza, Mara na Kagera. Kwa sasa wakala huo unajiandaa kuanzisha kanda nyingine ili kusogea karibu zaidi katika baadhi ya maeneo yenye uhitaji mkubwa wa udhibiti.

Hata hivyo, TFS katika utekelezaji wa majukumu yake imeanza kuzishirikisha mamlaka za Serikali kuwabana wanaoharibu misitu kwa njia mbalimbali ikiwamo ukataji miti, uchomaji mkaa, uchimbaji madini katikati ya misitu, uchomaji moto na ufyekaji wa miti kwa visingizio vya aina tofauti ikiwamo kuanzisha mashamba mapya.

Mtendaji Mkuu wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo anasema Serikali za mitaa zipo karibu zaidi na wananchi.

Akizungumza na wakuu wa wilaya na wakurugenzi watendaji wa halmashauri za mikoa ya Kanda ya Magharibi, Silayo alisema uhifadhi wa misitu unasaidia kubeba baoanuai muhimu kiuchumi kwa nchi yoyote duniani kwa kuwa kila kitu kina uhusiano wa karibu na mimea.

Profesa Silayo aliwaambia wadau waliohudhuria kikao hicho kuwa, maelekezo yote ya Serikali yanapaswa kutekelezwa katika kulinda rasilimali ya misitu ili maisha ya wananchi yasiathirike.

Hata hivyo, anasema misitu inakabiliwa na changamoto kiasi cha kuathirika kwa kasi kutokana na uharibifu unaotokana na tabiachi na shughuli za binadamu kama ukataji wa miti kwa ajili ya nishati, mbao; kilimo cha kuhamahama na kadhalika.

“Tunapaswa kuweka mikakati ya kutokomeza ufugaji na uvamizi wa misitu na uchimbaji madini,” anasema Profesa Silayo. Vilevile, anasema kumekuwapo pia na tabia ya baadhi ya watendaji kuwalazimisha wananchi wanaomiliki misitu vijijini kuifyeka kwa kisingizio cha kuendeleza maeneo yao kupitia kilimo.

“Hili tunapaswa kulikemea kwa nguvu zote na tuchukue hatua maana linachangia kuharibu misitu yetu. Hatuna budi kuilinda maana ndiyo uhai wetu. Na katika kupambana na haya yote lazima tushirikiane, misitu yetu ni ya thamani,” anasisitiza.

Anasema ushirikiano na kujituma kwa watendaji na watumishi wa ngazi mbalimbali wa Serikali ni jambo muhimu kwa kuwa ni jukumu lao katika kulinda rasilimali za Taifa.

Kwa mujibu wa utafiti wa TFS uliofanyika kati ya Novemba 2016 hadi Januari, 2017 Ofisa Leseni za Huduma za Misitu, Ali Maggid anasema bajaji na baiskeli zimekuwa zikitumika kusafirisha mazao ya misitu kupitia njia za panya hasa kwa wanaovuna kinyume na sheria.

Maggid anasema kutokana na hali ilivyo, licha ya kuwa unafanyika kinyume cha sheria ukiathiria mazao ya misitu, Serikali inapoteza ushuru unaofikia Sh1.1 bilioni kwa mwezi au Sh13.5 bilioni kwa hesabu za mwaka jana jijini Dar es Salaam pekee.

Tayari TFS imeanza kupambana na watu wanaotumia vyombo hivyo kwa shughuli haramu kwa kuwakamata na kuwatoza faini.

“Tukiwa karibu na watendaji wakuu wa wilaya mambo yatakuwa mazuri. Mapambano haya yatakuwa na mafanikio,” anasema Profesa Silayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri anawataka watendaji wa halmashauri kutoliona jukumu la ulinzi wa rasilimali za misitu kuwa lipo mikononi mwa TFS pekee, akiwaagiza kuanza kukabiliana na waharibifu wa miti katika maeneo yao mara moja.

Mwanri anawataka wakuu wa wilaya hizo kuongoza harakati za ulinzi wa misitu katika maeneo yao kwa kutenga muda mwingi wa ziada kushughulikia rasilimali hiyo ili iwe endelevu na kwamba, Tabora hatawaacha salama wale wataolitelekeza jukumu hilo.

“Mimi nitazingatia maelekezo ya Serikali na kama kuna mtu anadhani atapona ajue hilo halipo. Niwambie kitu, mikakati ni ile mbinu ya kuwa na mpango wa pamoja, lakini huku nyuma lazima uanze na lengo. Ukiwa na mikakati unaweza kufika mbali katika shughuli zako,” anasema Mwanri.

Anawataka wawakilishi hao wa Rais katika ngazi ya wilaya kuwa na misingi imara ya utendaji katika usimamizi wa rasilimali ya misitu badala ya kufanya kazi katika hali ya mazowea, kwa kuwa hata wale waharibifu wa misitu wataogopa na kisha kuacha.

Pia, Mwanri anawasihi wakuu hao wilaya kutotumia muda mwingi kujadili utunzaji wa misitu kwa kuwa sayansi haihitaji kuijadili, isipokuwa wajielekeze katika misingi na usimamizi wa sheria ili kuhakikisha kuwa wananchi hawaendelei kuiathiri.

“Mnajua nini, misitu ikiharibika maji hayatakuwepo na maji yasipokuwepo hata watu hawatasubiri kufukuzwa, isipokuwa wataondoka wenyewe maana kile kitu muhimu wanachokitegemea hakitakuwepo, hivyo ni wajibu wenu kusimamia hili,” anasema.

Anaongeza kuwa, tatizo la wafugaji kuvamia mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi ni kubwa kutokana na mikoa mingine kuisukumia mifugo hiyo katika mikoa hiyo.

“Si hilo tu, tatizo jingine ni kilimo cha kuhamahama, watu wanahama wakifika mahala wanafyeka misitu wanalima wakiona hakuna wanaondoka, wanahamia sehemu nyingine. Kwa hiyo huku kwetu kuna tatizo,” anasema na kuongeza:

“Nenda Sikonge pale kilimo cha tumbaku kinatuathiri sana, watu wanakata miti (kwa ajili ya ukaushiaji wa tumbaku). Wanakata hata mininga, miti yenye thamani kubwa.”

Hata hivyo, mkuu huyo wa mkoa anaishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza bei ya gesi ili kukabiliana na matumizi ya mkaa, jambo ambalo pia litaipa ahueni jamii.

“Kama misitu inaendelea kuharibika na gesi bado ipo juu, itakuwa ngumu kuwashawishi wananchi,” anasema huku akitoa mfano kuwa wakuu wa wilaya hawawezi kuwa na sauti ya kushawishi wananchi kupunguza matumizi ya mkaa kama nishati mbadala haitakuwapo.

Vilevile anasema, msukumo huo uelekezwe katika majeshi, shule na taasisi zingine zikiwamo binafsi kupunguza matumizi ya mkaa na kuni.

Mwanri anawataka watendaji wa Serikali kuwahamasisha wananchi kupanda miti na kuwafahamisha endapo hawatofanya hivyo basi watakosa kuni za kutumia.

“Na huu ndiyo ujumbe tunaoupeleka kwa watu wa tumbaku, kama hawatapanda miti hakuna kuni. Pia, kwenye vyanzo vya maji tuwaeleze watu wasikae karibu navyo, tuwaambie hawapaswi kukaa kwenye chanzo chochote cha maji,” anasema mkuu huyo wa mkoa.

Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Queen Mlozi anasema maeneo mengi ya mkoa huo yana misitu, lakini yamekuwa yakivamiwa na wafugaji ingawa hawatakubali hali hiyo iendelee.

“Hatutakubali kwa sababu misitu ni mali na ni uhai wetu, tutailinda ipasavyo,” anasema Mlozi.

-->