Roho ya kujitolea kusaidia Watanzania yajionyesha kikao alichohudhuria Balozi Migiro

Muktasari:

Kikao hufanywa kila mwaka kuzungumzia maendeleo ya wanachama, kazi walizozifanya na matazamio. Zipo jumuiya mbili.

Jumamosi iliyopita Balozi wetu Uingereza, Dk Asha Rose Migiro alialikwa kuhutubia jumuiya ya Watanzania na Waingereza, London.

Kikao hufanywa kila mwaka kuzungumzia maendeleo ya wanachama, kazi walizozifanya na matazamio. Zipo jumuiya mbili. Ya kisiasa jamii na ya kibiashara. Hapa tunazungumzia ya kijamii siasa. Zimekusanya raia wa nchi hizi mbili zenye historia iliyoanza baada ya vita vikuu vya kwanza ya dunia. Waingereza walichukua Tanganyika baada ya kuwachapa Wajerumani zahama zilizosababisha vifo milioni 17 na majeruhi milioni 20. Inakadiriwa Waafrika milioni moja na nusu walishiriki (mkuku). Ugomvi wa kugombania makoloni na mali. Ukoloni hauna adabu. Hadi 1961, TANU iliponyakua usukani.

Mwaka 1975 Balozi wetu Uingereza marehemu Amon Nsekela na Waingereza Askofu Trevor Huddleston na Roger Carter walianzisha Jumuiya ya Waingereza na Watanzania. Madhumuni yalikuwa urafiki na kuendeleza miradi ya kimaendeleo..Njozi zingali zikiendelea. Mlezi wa BTS ni Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.

BTS hukaribisha wageni wastahiwa kuzungumza na wanachama. Kikao cha mwaka huu kilielezwa mathalan kuwa miradi 46 imetimizwa katika miezi 12 iliyopita. Upo ? Arobaini na sita.

Miradi huwa ya kielimu na kibinadamu. Kwa miaka kadhaa sasa kitengo cha Tanzania Development Fund (TDF) kinachosimamiwa na wanajumuiya kimepigania kuondokana na ukeketaji. Kutoka 2014, Janet Chapman aliongoza kampeni ya kuchanga fedha kujenga nyumba ya kuwahifadhi wasichana wanaokimbia ukeketaji. Adha hii inayowatesa wanawake takriban milioni 200 duniani, huanza kila Novemba katika baadhi ya mikoa ya Tanzania. Kukamilishwa kwa jumba mkoani Mara wanaotoroka ni kheri tupu. Hapo watapata mafunzo mbalimbali ambayo wasingemudu kama wangetorokea porini au kuuawa wakikataa kukeketwa. BTS imechangia sana kuufahamisha ulimwengu adha hii. Maiti za wasichana wanaokimbia hutupwa mbugani na kutozikwa kama wanyama pori.

Sasa basi Balozi Migiro alisikiliza na hatimaye kuhutubia BTS. Baada ya hotuba fupi isiyokuwa na mbwembwe au maneno mengi aliuweka muda mrefu kujibu maswali. Maswali yalihusu katiba, uchaguzi wa Zanzibar 2015, tatizo la uraia pacha na umilikaji ardhi kwa Watanzania wakazi Ughaibuni, nk. Balozi aliulizwa pia kwanini malipo ya viza huwa ya juu sana kwa baadhi ya wanachama wa BTS wanaojitolea Tanzania. Mfano mzuri ni wahudumu wa mpango unaosimamiwa na Mtanzania Aseri Katanga (“Computers 4 Africa”) ambapo hupeleka tarakilishi nchi tano za Kiafrika ikiwapo Tanzania. Tarakilishi husaidia watoto shuleni hasa vijijini. Balozi aliahidi kufuatilia tatizo na kulisuluhisha.