SAIKOLOJIA : Fahamu jinsi ya kuepuka mizozo katika ndoa

Muktasari:

  • Kama ndoa yako au ya jamaa yako kukabiliwa na mizozo usistajabu kwa kuwa ndoa nyingi hata zile zilizo bora hukabiliwa na changamoto hii. Ingawa siku hizi changamoto hii husababisha ndoa nyingi kuvunjika hususan za vijana, wataalamu wamebaini kuwa wanandoa wanaweza kudhibiti mizozo wao wenyewe.
  • Kwa kufanya hivyo kunawapata mafanikio ya aina mbili. Kwanza kuifanya mizozo itokee kwa nadra sana. Pia, wataweza kujenga uwezo wa kuihimili na kuikabili ili athari zake zisiwe na madhara makubwa katika ndoa

Je, wewe au jamaa yako husumbuliwa na mizozo katika ndoa? Pengine unaweza kukwama kujibu swali hili kwa kutokuelewa maana ya mzozo. Neno hili lina maana ya mabishano ya maneno makali na kelele. Mizozo ni mojawapo ya changamoyo ambazo huweza kuathiri ndoa kwa kuwafanya wanandoa wagombane, wasielewane na hata kuachana.

Kama ndoa yako au ya jamaa yako kukabiliwa na mizozo usistajabu kwa kuwa ndoa nyingi hata zile zilizo bora hukabiliwa na changamoto hii. Ingawa siku hizi changamoto hii husababisha ndoa nyingi kuvunjika hususan za vijana, wataalamu wamebaini kuwa wanandoa wanaweza kudhibiti mizozo wao wenyewe.

Kwa kufanya hivyo kunawapata mafanikio ya aina mbili. Kwanza kuifanya mizozo itokee kwa nadra sana. Pia, wataweza kujenga uwezo wa kuihimili na kuikabili ili athari zake zisiwe na madhara makubwa katika ndoa

Mara nyingi mizozo hii inapoanza huwa midogo, lakini hukuzwa kwa ushindani kati ya wanandoa na kubadillika kuwa mabishano makali. Mara nyingine wanandoa hupandisha jazba na kutumia maneno makali ambayo huweza kukuza mzozo na kuufanya ukawa mgogoro mkubwa kuliko hali yake halisi. Bwana aliyekuwa akitoka kumchukua mtoto shuleni aliombwa lifti na mchumba wa kaka yake na akamkubalia. Alipofika nyumbani mkewe alimgombeza kwa kufanya hivyo. Alipomwambia yeye hakuona kama lile lilikuwa kosa hasa kwa kuwa huyo msichana hata yeye mkewe anamfahamu ni rafiki yake. Mkewe alikasirika akamtukana na kumwita muhuni mpenda wanawake.

Yule bwana alikasirika kwa kutukanwa mbele ya mwanawe na kumfokea mkewe. Mwanamke akaja juu na kujibu kwa matusi makali. Wakaendelea kugombana kila mmoja akitoa maneno makali hadi mke akahamaki na kusema anaondoka na ukawa mwisho wa ndoa yao.

Mwanamume pia kwa hasira akamjibu kwa jeuri “Kama umeamua kuondoka ondoka” Haya ndiyo madhara ya mizozo katika ndoa. Isipodhibitiwa jambo dogo hulifanya likawa kubwa na kuathiri ndoa. Mara nyingi mizozo kutokea wanandoa wanatofautiana kimawazo.

Nini husababisha mgogoro wanandoa wanapotofautiana

Mabishano yakiendelea baadhi ya wanandoa huchukia na kujikuta wanafanya vitendo kama vile kulalama kwa sauti na kutumia lugha chafu. Mambo haya huleta hamaki, fedheha na mgogoro katika ndoa.

Kwa kiwango kikubwa kutofautiana hutokea wakati mume na mke wanapokuwa na mawazo tofauti jinsi wanavyojadiliana changamoto zinazowakabili. Mara nyingi mwanamke anaweza kuwa anapenda wasijadiliane tu kuhusu kile kilichotokea bali hata kwa nini kilitokea na kilitokea vipi. Mwenzake hususan mwanamume huenda ikawa anapenda wajadiliane kile kilichopo badala ya kurudi nyuma. Wanapokutana wanandoa wenye tofauti hali huwa mbaya kwani wakati mmoja anaposhikilia waendelee kujadili suala fulani mwingine anajitahidi kuliachilia mbali na kuepuka kuendelea kulizungumzia ili kulisahau.

Natumaini unaposikiliza ugomvi wa wanandoa wawili uwewahi kugundua tofauti iliyo dhahiri kati yao. Mmoja anaweza kuwa anapendelea kuendeleza malumbano na mwingine kuepuka kuendeleza majadiliano. Tofauti hizi hutokea kutokana na wanandoa walivyolelewa. Mmoja anaweza kuwa anatoka familia ya ukimya na utulivu na mwingine amezaliwa kwenye watu wasemaji na waliocharupuka sana.

Mbinu za kuepuka mizozo

Baadhi ya njia zifuatazo huweza kusaidia kuepuka mizozo katika ndoa.

Epuka maneno makali, ushindani mnapotofautiana

Wanandoa wanapaswa kudhibiti ndimi zao ili wasiseme maneno makali na matusi wanapokosewa na wenzao. Aidha, kila mmoja anawajibika kudhibiti hasira na hamaki kunapotokea hali ya kutoridhika kwa kitendo au vitendo vya mwenzake. Maneno makali yanapotumika katika kupishana kidogo hufanya mlipuko wa hasira unaoweza kusababisha mgogoro mkubwa.

Inapotokea hali ya kutoelewana, jiulize “Nitapata hasara gani nitakapokubaliana na malalamiko ya mwenzangu”, jambo gani huenda nimefanya likasababisha mtafaruku, kipi kinanizuia nisimuombe msamaha mwenzangu au kumsamehe kama amenikosea.

Epuka kudharau hisia au mawazo ya mwenzako

Kuthamini hisia na mawazo ya wengine hujenga na kuimarisha upendo na kuelewana.

Mwanandoa mwenzako anapohamanishwa na kitendo chako usimshutumu kwa kumwambia kama vile anayakuza mambo bila sababu. Lengo lako linaweza kumfanya atazame tatizo kwa mtazamo tofauti, lakini ni watu wachache wanaoweza kupozwa hasira kwa ushauri kama huo. Mara nyingi wao huona hiyo ni dharau.

Aidha, mwenendo wa majivuno na makuu huweza kumponza mwanandoa mmoja akapuuza hisia za mwenzake na kusababisha mizozo na migogoro ya mara kwa mara katika ndoa.

Epuka kumfikiria mwenzako mawazo mabaya

Mawazo mabaya kwa wenzetu ni sumu kubwa ya mapenzi na uhusiano mwema. Kuna mwanandoa anayekuwa na mawazo mabaya kuhusu mwenzake kila mara. Mathalani mwenzake anapochelewa kazini, badala ya kufikiria huenda amezidiwa na kazi, matatizo ya usafiri au amechelewa kutokana na kutoa msaada kwa rafiki aliyepata shida, yeye atawazia mambo kama vile mchepuko au kushiriki katika shughuli za burudani.

Mwenye tabia ya kumfikiria mabaya mwenzake hata anapotendewa mazuri na mwenzake huwaza anafanya hivyo kuficha mabaya anayomtendea. Bahati mbaya anapoteleza akasema neno linaloudhi yeye anapata wazo amesema hivyo kwa kuwa anamdharau na hamthamini.

Hitimisho

Tuliyoyataja ni baadhi ya mambo yanayoweza kuwafanya wanandoa kudhibiti mizozo na pengine hata kuiepuka kabisa. Muhimu zaidi ni kuzingatia ukweli kuwa mapenzi sio mapofu kama wengi wanavyofikiria kwani yanapaswa kuengwaengwa na kustawishwa. Hayastahili kuwa na unafiki, hasira, ushindani wala visasi. Katika mapenzi bora wakati wote wahusika wanapotofautia, husemezana kwa upendo, wema na ustahimilivu. Daima huwa wanaogopa hasira au chuki ambayo huweza kumong’onyoa mapenzi hadi ndoa ikavunjika.