SAIKOLOJIA : Fahamu siri ya furaha katika maisha

Muktasari:

  • Kinachonishangaza ni kuwa kila ninapokutana naye huonekana hana furaha na ninapomuuliza kipi kimsikitishacho huwa hakosi jambo la kuniambia. Siku moja hutaja matatizo ya kazini, siku nyingine ya nyumbani kwake na mara nyingine hutaja changamoto zinazotokana na mambo ya kijijini kwake.

Nilijaribu siku moja kuuliza kila mtu niliyekutana naye kama ana furaha katika maisha au hapana. Wengi walinijibu kuwa hawana furaha. Hapo nikamkumbuka rafiki yangu anayeitwa Masumbuko. Hili siyo jina lake bali amepachikwa na watu kutokana na tabia yake ya kulitumia neno hili kila mara. Kinachonishangaza ni kuwa kila ninapokutana naye huonekana hana furaha na ninapomuuliza kipi kimsikitishacho huwa hakosi jambo la kuniambia. Siku moja hutaja matatizo ya kazini, siku nyingine ya nyumbani kwake na mara nyingine hutaja changamoto zinazotokana na mambo ya kijijini kwake. Kila anaposalimiwa na kuulizwa hali yake hujibu kwa kusema; maisha yangu ni masuumbuko tu wala sina furaha.

Siku moja nikamuuliza “Unafikiri masumbuko yako yataisha lini?” Alinijibu,“Bwana nimekata tamaa”. Kuna wakati niliwaza kuwa yatakwisha nitakapojenga nyumba yangu, au wakati watoto wangu watakapomaliza shule na kuanza kazi au wakati nitakapostaafu na kujiajiri mwenyewe kwa kuendesha miradi. Lakini kila nilililoliwazia linapotimia bado maisha yangu yanaendelea kuwa ya masumbuko.

Huenda kuna watu wengine wengi wenye mawazo kama ya rafiki yangu Masumbuko. Kwao nina ujumbe huu “Kila mtu ana haki ya kuwa na furaha”. Wala hakuna sababu yeyote inayostahili kumfanya mtu adumu katika hali ya kukata tamaa. Huenda ni kweli kuwa kuna baadhi ya watu wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha ambayo wanashindwa kujitanzua nayo. Lakini hakuna sababu ya kukata tamaa. Siku zote maisha yanaweza kufanywa yakawa mazuri mradi tu mtu awe na dhamira ya kuyafanya hivyo.

Furaha hainunuliwi dukani au sokoni wala hatuwezi kuiazima kutoka kwa jamaa zetu. Huwa inatokana na mtazamo wa fikra zetu. Baadhi ya watu huwa wahuzunikaji wazoefu. Hawa hawana furaha kwa sababu hawajajifunza au kujizoeza tabia au mwenendo uliotofauti na huu.

Kila wakati wao hufikiria kuwa maisha yamekuwa siyo rafiki kwao na kwamba yanawaonea. Wao huwa wanakataa kuyakubali mambo ya ulimwengu kama yalivyo. Wanakuwa na mtindo wa kuyaona mambo yote ni mabaya na wala hayana matumaini. Huu ni mtazamo ulio adui wa kwanza wa furaha katika maisha. Hii ndiyo hisia aliyokuwanayo yule rafiki yangu Masumbuko.

Hisia tofauti na hii ni ile ya kuyatazama mambo kwa upande wa uzuri. Nakumbuka siku moja nilishuhudia ugomvi kati ya mume na mke. Mwanamke alikuwa ameamua kupanda maua ya waridi kwenye kiwanja mbele ya nyumba yao. Alikuwa anayapenda maua ya waridi kwa sura yake inayopendeza na harufu yake nzuri.

Lakini mwanaume alikataa akidai kuwa mimea ya waridi siyo mizuri kwa kuwa huwa na miba mikali inayoweza kumchoma mtu anapokuwa anapunguza matawi au anapokata vitawi vyenye maua kwa ajili ya kupamba.

Huu ni mfano wa mitazamo miwili tofauti kwa kitu kimoja. Mke alikuwa analitazama ua la waridi kwa upande wa uzuri ambao tunaweza kuuita mtazamo chanya. Lakini mumewe alikuwa akilitazama kwa upande wa ubaya ambao ndiyo mtazamo hasi.

Tabia ya kuyatazama maisha kwa mtazamo chanya ndiyo yenye maslahi katika maisha. Humpatia mtu amani ya nafsi na hali ya kuridhika na vitu tulivyonavyo na tunavyovipata katika maisha. Mawazo chanya huweza kubadili masononeko kuwa furaha, huzuni kuwa shangwe, hali ya mtafaruku kuwa hali ya maelewano na hali ya kukata tamaa kuwa ya matumaini. Mtu mwenye tabia ya kuyatazama maisha kupitia jicho la uzuni huweza kubadili hisia zake kuhusu maisha na kuyafanya kuwa mazuri. Ni mtu mwenyewe na hisia zake ndiye anayeweza kuyafanya maisha yake yawe ya furaha au ya huzuni. Tunalazimika kujua jinsi ya kujenga hisia za furaha.

Tumejifunza kuwa tunaweza kuwa na furaha katika maisha iwapo tutakuwa na hisia za furaha. Hivyo hatuna budi kujifunza jinsi kujenga hisia za furaha.

Jinsi kujenga hisia za furaha

Hatua ya kwanza katika kujenga furaha ni kuchunguza jinsi maisha yako ya nyuma yalivyokuwa. Jiulize kama katika miaka iliyopita maisha yako yalikuwa ya furaha au hapana. Kama hayakuwa ya furaha jiulize ni mambo gani yanayofanya sasa au wakati ule afikirie kuwa maisha yake hayakuwa ya furaha. Kama hivyo ndivyo itakavyokuwa utafakari kwa dhati jinsi hali ilivyokuwa na kilichosababisha hali hiyo. Uchunguzi wa kina wa hali ilivyokuwa na sababu zake itamsaidia kutambua jinsi ya kubadilisha hisia za mtazamo wa maisha yake ya sasa. Wala haitakuwako hoja ya kuhuzunika kwa yale yaliyopita ila kuyatazama maisha yajayo huku ukijiandaa kuyachukulia kama yalivyo na kufanya juhudi za pekee kuhakikisha haitokei hisia ya yale mabaya yaliyotokea zamani.

Jambo ambalo hutokea mara kwa mara ni kuweka lawama kwa watu wengine kwa changamoto zinazotutokea. Mtu anapojitambua udhaifu au makosa yake siyo rahisi kujenga hisia potofu kuwa matatizo yake yanasababishwa na watu wengine. Mara nyingi tumewahukumu watu wengine kutokana na mtazamo wetu ulio hasi.

HITIMISHO

Tutakapoweza kujitambua tutaweza kuyatazama maisha yetu katika mtazamo mpya. Mtazamo huo ni ule utakaotusaidia kusahau masumbuko ya zamani na kujijengea wenyewe maisha mema ya furaha. Kadri tutakavyofanya hivyo tutaanza kugundua siri ya maisha ya furaha tunayotarajia.

Maisha yetu yaliyokuwa ya huzuni na yasiyo na maana yataanza kutoweka huku yakituletea fikra mpya za furaha na matumaini. Tutakuwa na matumaini kuhusu maisha yetu ya baadaye na kuwa na amani na wale tulionao karibu. Tunapokuwa na imani na watu wengine ndivyo kadri tutakavyogundua furaha mpya ya kushirikiana na wenzetu. Hiki ndicho kichocheo cha kuwa na furaha tele katika maisha yetu.