SAIKOLOJIA : Unaweza kufanya watu wakuthamini

Muktasari:

  • Moja kati ya mahitaji muhimu ya binadamu baada ya chakula, mavazi na malazi ni kuheshimiwa na kuthaminiwa na jamii. Binadamu ni kiumbe pekee aliye na daraja kuliko viumbe wengine wote. Kinachompandisha hadhi kuliko viumbe wengine ni uwezo wake wa kufikiri ambao umemwezesha kuyatawala mazingira yake na kuyatumia ili kuboresha maisha yake.

Je, unathaminiwa na watu katika jamii? Kama unathaminiwa ni mambo gani yanayokufanya uone kuwa unathaminiwa? Kama hauthaminiwi ni mambo gani yanayokufanya uhisi hivyo?

Moja kati ya mahitaji muhimu ya binadamu baada ya chakula, mavazi na malazi ni kuheshimiwa na kuthaminiwa na jamii. Binadamu ni kiumbe pekee aliye na daraja kuliko viumbe wengine wote. Kinachompandisha hadhi kuliko viumbe wengine ni uwezo wake wa kufikiri ambao umemwezesha kuyatawala mazingira yake na kuyatumia ili kuboresha maisha yake.

Maendeleo yetu na maisha yetu kwa jumla yanawategemea watu. Tunachokihitaji kutoka kwao ni kututhamini, kutujali na kutupenda. Watu watatuthamini kutokana na matendo yetu na jinsi tunavyoonekana kwao. Hii ni kwa sababu imethibitishwa kuwa watu wenye muonekano wa hali ya juu mara nyingi huwa ndiyo mwenye mafanikio katika maisha.

Licha ya muonekano wetu kufanya tuthaminiwe na watu, unadhifu pia huwa na uhusiano na fikra zetu. Ndiyo maana viongozi wa dini, masheikh, mapadri, makasisi na wachungaji huvaa mavazi maalumu ambayo huwafanya wapate hisia fulani za mamlaka katika nafsi zao. Inasemwa kuwa askari hufikiri na kutenda kama askari anapokuwa amevaa sare za jeshi.

Niliwahi kusikia kisa cha ofisa na dereva wake siku waliyokwenda kwenye sherehe, walipofika waliegesha gari mbali na ukumbi. Hivyo, watu hawakuwaona jinsi walivyokaa kwenye gari, lakini kwenye ukumbi kulikuwa na msichana aliye andaliwa kumvisha mgeni shada la maua. Ofisa na dereva walipofika mlangoni yule msichana alikwenda kumvisha shada la maua dereva kutokana na jinsi alivyoonekana nadhifu na mwenye hadhi kuliko bosi wake. Kwa hakika siyo sahihi kumthamini mtu kwa mavazi na muonekano wake pekee, kwa sababu kuna mambo mengine muhimu kama vile akili, ujuzi na tabia. Lakini, pia tukumbuke kuwa siku zote watu hutupangia thamani kutokana na jinsi tunavyoonekana kwao hasa wanapotuona mara ya kwanza. Muonekano ndicho kitu cha kwanza ambacho hudumu zaidi katika fikra za mtu anayetuona mara ya kwanza. Aidha, muonekano huo huwa na taathira hata katika sifa zetu nyingine ambazo mtu huweza kuzigundua baada ya kutuona mara ya kwanza. Mara ngapi tumewahi kuwasikia watu wakisema, “mtu kama yule hawezi kutenda jambo la kijinga kama hili” kipimo wanachokitumia hapa huwa siyo kingine isipokuwa anavyoonekana.

Je, umewahi kuchunguza ni watu wa aina gani ambao huonekana wanaheshimika sana kwenya mkusanyiko wa watu kama vile kwenye kituo cha basi, sokoni au mkutanoni. Utagundua kuwa wanaoheshimika zaidi ni wale walio nadhifu. Kwa kawaida watu huamini kuwa mtu aliye nadhifu ni mtu wa maana, aliye mwenye akili, msomi, anaye aminika na aliyefanikiwa katika maisha. Mtu asiye nadhifu anayeonekana mchafu watu humchukulia kama mtu asiye na maana, siyo mwerevu, siyo makini na hajendelea kimaisha.

Lakini, mtu mwingine anaweza kukata tamaa kuwa hawezi kuonekana nadhifu kwa kuwa hana fedha za kuweza kununulia mavazi ya thamani.

Hata hivyo, ikumbukwe kuwa ili mtu aonekane nadhifu siyo lazima avae nguo ghali. Unadhifu ni kuvaa nguo safi na kuutunza mwili mzima katika hali ya usafi. Hakika ili tuwe nadhifu tunahitaji nguo nyingi zitakazotuwezesha kuwa nadhifu kila siku. Tukinunua nguo za bei nafuu tunaweza kupata nyingi na kuonekana nadhifu siku zote.

Hatuna budi kukumbuka kuwa unaadhifu haushii katika manufaa ya kuwavutia watu wanaokutazama, bali hata kwako. Kadri unavyojishughulisha kujiweka katika hali ya unadhifu ndivyo kadri unavyojijengea hali ya kujithamini. Unapojithamini ndipo na watu wengine wanapokuthamini. Kwa hakika unapojifikiria ni duni na mtu wa hali ya chini atakuona vivyo hivyo na utajipunguzia nafasi ya kuthaminiwa.

Kulikuwa na kijana mmoja ambaye hakusoma shule, lakini hakupenda kabisa watu wajue hakusoma . Hivyo, alikuwa akijiweka katika hali ya unadhifu wa hali ya juu siku zote. Alikuwa akiweka kalamu mbili hadi tatu kwenye mfuko wa shati lake. Alipotembea katika mkono mmoja alishika gazeti na upande mwingine alibeba mkoba wa mkononi. Siku moja aliingia posta kumsalimu rafiki yake anayefanya kazi hapo. Alipoingia tu alikutana na mzee mmoja kutoka mtaani kwao aliyemuomba amjazie fomu. Kijana aliona huo ni mtihani mkubwa ambao ungefichua siri yake. Lakini, alifikiri haraka akaweza kuvuka mtihani huo, alimwambia mzee ana haraka sana kisha akachukuwa kalamu moja katika mfuko wa shati akampatia mzee na kumuomba atafute mtu amjazie fomu yake.

Kila ninapoikumbuka hadithi hii huzidi kuamini kuwa mtu anaweza kujitengenezea hadhi anayoipenda na kuwafanya watu wamthamini. Hata hivyo, pamoja na kuwa nadhifu bado kuna mambo mengine ambayo mtu anapaswa kufanya ili watu wakuthamini kikamilifu. Watu wanakuthamini kikamilifu iwapo utaishi nao kwa maelewano ushirikiano staha na adabu. Huna budi kuwatendea mema uwe mwaminifu na mvumilivu. Uepuke maneno ya karaha, jeuri wala usiwe na choyo, chuki na hasira pamoja na yote ni lazima uthamini watu.